Mkutano wa SADC: Kikao Chengine cha Porojo Barani Afrika

Habari:

Mkutano wa kawaida wa 39 wa wakuu wa nchi na serikali za Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) umefanyika tarehe 17 na 18 Agosti 2019 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania. Kabla yake mkutano huu ulitanguliwa na mikutano iliyoanza tangu tarehe 05 Agosti, 2019.

Maoni :

SADC iliasisiwa mwaka 1980 ambapo awali ilijulikana kwa jina la Jumuiya ya Ushirikiano ya Kimaendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC), baadae mwaka 1992 ikabadilishwa jina na kuitwa SADC. Ilianzishwa kama jumuiya iliyolenga kuimarisha uhusiano wa kikanda baina ya nchi wanachama na kuuondoa umasikini kupitia maendeleo ya kiuchumi na kuhakikisha ulinzi na usalama. Malengo hayo yote hayajafikiwa hata kidogo.

Nchi za SADC zinakabiliwa na matatizo mengi ya kijamii, kichumi, kisiasa, na kiusalama licha ya miaka mingi ya uwepo wake. Kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Dunia nchi hizi zinakabiliwa na uzorotefu wa ukuaji wa uchumi. Ukuaji ilikuwa kwa asilimia 2.3 mwaka 2018, kutoka asilimia 2.5 mwaka 2017 na asilimia 2.8 mwaka 2019, na hivyo kiujumla uchumi ulikuwa chini ya asilimia 3.

Kiujumla ukuaji huu hafifu unaashiria mwendelezo wa hali dhaifu ya kiuchumi inayotokana na misingi dhaifu ya uchumi kikanda na kimataifa. Matatizo kama madeni, kupanda bei, nakisi, kanuni zisizotabirika pamoja na hali tete vimeleta madhara ya wazi na matokeo mabaya kwa ukuaji uchumi katika nchi hizi.

Licha ya kuwa na rasilimali nyingi sana bado nchi hizi zimefungwa na ukoloni mamboleo hususan wa Marekani na China. Hivyo, ni wazi kamwe hazitokuwa na uchumi imara chini ya makucha ya ubepari.

Umasikini umeendelea kuwa moja kati ya changamoto kubwa kwa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ambazo nyingi mingoni mwao ni nchi za SADC. Ripoti zinasema nchi hizi idadi ya wakaazi masikini inakisiwa kuwa asilimia 87, na robo tatu katika nchi 43 zenye kiwango cha umasikini juu ya asilimia 18 zipo katika nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara,ambapo kiwango jumla ni asilimia 41.

Jumuiya hii kwa kiasi kikubwa imeshindwa kuimarisha usalama katika nchi wanachama. Kuna magenge thabiti ya kihalifu, vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vingi vinachochewa na maslahi ya mataifa ya kibepari, ambavyo vimeathiri na kuharibu uchumi na mshikamano wa kijamii. Kupitia propaganda chafu ya vita vya ugaidi, mataifa haya ya (SADC) yameweza kuingiliwa katikati na madola ya kikoloni ambayo huwalazimisha kutesa na kuuwa watu wao kwa gharama duni ya rushwa, kwa jina la msaada wa kupambana na ugaidi

Nchi za SADC zimeshindwa kabisa kuleta maendeleo endelevu, badala yake zimekumbatia uwepo wa mifumo ya makodi inayochagizwa na dhana chafu ya uzalendo, na miundombinu mibovu ya barabara ambayo ni miongoni mwa vipingamizi vikubwa vinavyopelekea kuzorota kwa maendeleo ya nchi hizi.

Jumuiya hii kama jumuiya nyingine nyingi zimethibitisha kushindwa, huku wanachama wake wameamua kujiunga na Jumuiya nyingine za kikanda za kiuchumi, kama Afrika ya Kusini na Botswana ambazo ni wanachama wa Umoja wa SACU, Zambia ni mwanachama wa Jumuiya ya Soko la Pamoja (COMESA) ilhali Tanzania ni mwanachama wa EAC.

Kwa kukihitimisha, SADC kama zilivyo Jumuiya nyingine za kikanda barani Afrika kamwe hazitoweza kuleta maendeleo halisi wala kuwanusuru watu wake na umasikini wa kutupwa, kwa kuwa hazina makali yoyote, zaidi ya kuwa ni nyenzo za ukoloni mamboleo kwa ajili ya unyonyaji

Imeandikwa na Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.