Mkataba wa Kibiashara Kati ya Amerika na Uchina

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Raisi wa Amerika amesema: “Awamu ya Kwanza ya Mkataba wa Kibiashara na Uchina huenda ikatiwa saini hivi punde tu” Januari 15, tarehe aliyoitangaza mwezi jana kuwa ndio tarehe ya utiaji saini. Trump akaongeza: Ningependa kukamilisha awamu ya pili ya mkataba huo na Uchina baada ya uchaguzi wa urais katika muktadha wa juhudi za kumaliza vita vya kibiashara vinavyo endelea kwa miezi baina ya nchi kuu mbili hizi kiuchumi duniani, vilivyo pelekea vurugu katika soko na kuathiri ukuaji wa kiulimwengu …” (Bawabit Al-Ain, 10/01/2020). Na Wizara ya Biashara ya Uchina imethibitisha rasmi kuwa “Makamu wa Waziri Mkuu Liu He atakwenda Washington ili kutia saini awamu ya kwanza ya makubaliano hayo ya kibiashara. Hii ndio taarifa ya kwanza kuthibitishwa rasmi iliyotolewa na Uchina juu ya utiaji saini huo, ambapo nyuma Trump alisema kuwa atazuru Beijing baada ya kutiwa saini makubaliano hayo ili kuanza mazungumzo juu ya Awamu ya Pili …”(Trade Captain, 10/01/2020). Je, hili lamaanisha kuwa uhasama wa kibiashara kati ya Amerika na Uchina umekwisha?

Jibu:

Ili kuliweka wazi jibu la maswali hayo ya juu na kufahamu asili ya vita hivi vya kibiashara kati ya Amerika na Uchina, tutatathmini yafuatayo:

Kwanza: Asili ya Kadhia Hii:

1- Anayefuatilia sera ya Amerika kwa Uchina anaamini kuwa Amerika inatafuta ubwana katika eneo la Eurasia (Ulaya na Asia), na haikubali Uchina kuipitia mbele yake, kwa sababu Eurasia ni eneo muhimu ambalo kwalo Amerika imetumia sera imara ya kigeni ili kuhakikisha utawala wake juu yake, ambalo hadi leo linaendelea kutumikia maslahi ya taasisi za Amerika. Tangu kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti mnamo 1991, hali ya kisiasa nchini Amerika iligawanyika sehemu mbili kuu kuhusiana na muundo wa sera ya Amerika kwa Uchina:

Kwanza: inajumuisha kuamiliana au kushirikiana na Uchina ili iwe mshika dau na muhusika katika nidhamu ya kimataifa inayoongozwa na Amerika.

Pili: Kuyakinisha kuwa nia za Uchina haziwezi kuaminiwa, na kwamba pasi na shaka yoyote ni nguvu ya kiushindani inayo simama dhidi ya mfumo wa kimataifa wa Kimagharibi unaoongozwa na Amerika.

Katikati mwa miaka ya tisini, uundwaji sera ya kigeni ya Amerika ulisimama juu ya kuiorodhesha Uchina kama nguvu hasimu na kutabanni sera ili kuzuia kuinuka kwa Uchina. Katika enzi ya idara ya kisiasa ya Clinton na Obama, sera ya kuidhibiti Uchina ilitabanniwa, na katika enzi ya idara za chama cha Republican za Bush mwana na Trump, zilichukua sera kali zaidi ya kuidhibiti Uchina. Trump amehamasisha kuwepo kwa vita wazi vya kibiashara juu ya Uchina. (Financial Times)

2- Sera ya udhibiti ya Amerika ilikuwa na malengo makuu mawili: kwanza, kuepusha kuibuka kwa Uchina kama dola kuu ya kieneo, na pili, kuizuia kutokana na kubadilisha kipengee chochote cha mfumo wa Kimagharibi wa kimataifa. Ili kutimiza malengo haya, Amerika imetabanni hatua kadhaa, ikiwemo [kuibua ukiukaji wa haki za kibinadamu wa Uchina eneo la Tibet, Turkestan Mashariki, na Hong Kong … kuifanya Uchina ijishughulishe na mgogoro wa kinuklia wa Korea Kaskazini na mizozo ya kieneo katika Bahari ya Uchina Kusini … kuzitumia India, Japan, na Australia kuzuia matarajio ya Uchina ya kijeshi na ukuaji katika eneo la Asia-Pasifiki … kuzuia njia ya Uchina kufikia teknolojia za kisasa … na kujiondoa katika Mradi wa Ukanda wa Uchina].

Taasisi ya kisiasa ya Amerika imejifunga kikamilifu na sera hii ya kudhibiti huku kukiwa na mabadiliko madogo katika baadhi ya hatua za kupambana na matarajio ya kimamlaka ya Uchina. Lakini, baada ya mgogoro wa kifedha wa kiulimwengu wa 2008 na vita vibaya vya Amerika nchini Afghanistan na Iraq, Amerika ilitambua kuwa sera ya kuidhibiti Uchina haitoshi na kuamua kuitilia nguvu. Lengo la mkakati wa Obama katika kile kinacho julikana kama (Mkakati wa Asia) lilikuwa ni kuhamisha vifaa vya kijeshi na wanajeshi kutoka Ulaya hadi Asia na Pasifiki, na kukabiliana na uwezo wa kijeshi wa Uchina. Kisha Trump akaanza kulenga uchumi wa Uchina moja kwa moja, na idara yake ikaipa Uchina lakabu ya “mpangaji njama za kisarafu” na kuanzisha vita vya kibiashara na Beijing, na hili likaendeleza juhudi za kuidhibiti Uchina katika nidhamu iliyojengwa juu ya kanuni za kimataifa. (Shirika la habari la BBC).

Pili: Vita vya kibiashara kati ya Amerika na Uchina:

1- Kama tulivyo taja awali, Amerika ilianzisha vita vya kibiashara na Uchina ili kudhibiti kuinuka kwa Uchina, na vita hivi vya kibiashara baina ya nchi hizi mbili kuu kiuchumi vilipamba moto kutokana na uhaba wa kibiashara ambapo Amerika huagiza bidhaa na huduma zenye thamani ya dolari bilioni 558 kutoka Uchina, na upande mwingine, Uchina huagiza bidhaa na huduma zenye thamani ya dolari bilioni 179 kutoka Amerika (Afisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Amerika). Lakini, hivi karibuni umeonekana mwafaka baina yao ili kwanza kutimiza maslahi yao mtawalia!

2- Amerika na Uchina zimefikia makubaliano nusu ya kibiashara katika miezi ya hivi karibuni, “ambayo yatamaliza kukolea kwa vita baina ya nchi hizi mbili kuu kiuchumi ulimwenguni tangu mwaka jana. Trump nyuma alisema kuwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kibiashara yatafikia asilimia 60 ya makubaliano jumla, na kutokana nayo inadhaniwa kuwa itajumuisha kujitolea kwa Uchina katika kununua bidhaa zaidi za ukulima za Amerika, kwa badali ya Amerika kupunguza ushuru wa forodha unaotozwa bidhaa za Uchina …” (Al-Arabi Al-Jadeed, 05/01/2020 M). Mtandao wa Al Arabi mnamo 15/12/2019 ulikuwa umechapisha yafuatayo: “miezi 21 baada ya kuanza kwa vita vya kibiashara kati ya nchi mbili hizi kuu kiuchumi ulimwenguni, Amerika ilifikia awamu ya kwanza ya makubaliano ya kibiashara na Uchina lakini hayatatiwa saini kabla ya Januari mwakani. Chini ya makubaliano hayo, Amerika inathibitisha kuwa itapunguza ushuru wa forodha wa asilimia 15 hadi nusu kwa bidhaa zinazo agizwa kutoka Uchina zenye thamani ya dolari bilioni 120, lakini itadumisha ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zinazo agizwa kutoka Uchina zenye thamani ya dolari bilioni 250. Na Amerika ikaachana na mipango ya kutoza ushuru mpya wa asilimia 15 kwa bidhaa za Uchina zenye thamani ya dolari bilioni 160 ambao ulipangwa kuanza utendakazi wake hivi leo, ambapo inajumuisha vidude vya kuchezea watoto na simu. Beijing pia ilikubali kuagiza bidhaa na huduma zaidi za Amerika zenye gharama ya takribani dolari bilioni 200 katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Uchina pia itafutilia mbali utozaji wa ushuru ziada juu ya bidhaa zinazo agizwa kutoka Amerika uliopangwa kuanza leo kama ambavyo watafutilia mbali utozaji ziada wa ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwa magari na asilimia 5 kwa vipuri vya Amerika. Uchina imeweka wazi kuwa itaendelea kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa za Amerika zenye kugharimu takriban dolari bilioni 126, ikiongezewa na ahadi yake ya kuongeza ununuzi wa bidhaa za ukulima za Amerika kwa zaidi ya dolari bilioni 50 kwa mwaka.” Trump amekuwa makini kutafuta soko linalokuwa kwa usafirishaji nje wa bidhaa za ukulima kwa sababu anagombea uchaguzi mkuu mwaka huu 2020 na hataki kupoteza kura za wakulima wanaosubiri pakubwa malipo ya fadhila kwa kukosekana masoko ya kutosha kwa usafirishaji bidhaa zao. Kabla ya hilo, tovuti ya Habari ya Al Bayan ilichapisha: “Wizara ya Biashara ya Uchina ilisema – katika taarifa mnamo Ijumaa jioni – kuwa makubaliano hayo yalijengwa juu ya msingi wa usawa na kuheshimiana na yanajumuisha sura tisa: utangulizi, haki za milki ya kifikra, uhamishaji wa teknolojia, chakula na bidhaa za ukulima, huduma za fedha, kiwango cha ubadilishanaji wa sarafu na uwazi, upanuzi wa biashara, tathmini ya pamoja baina ya pande hizo mbili na utatuzi wa mzozo, na masharti ya mwisho.” (Al-Bayan News, 13/12/2019).

3- Lakini, hii haimaanishi kuwa makubaliano haya juu ya vita vya kibiashara yatamaliza hali ya uhasama wa kiuchumi baina ya pande hizo mbili, kwa sababu vita hivi vya kibiashara sio lengo halisi la kuidhibiti Uchina, bali kuna kitu cha kina na hatari zaidi nyuma yake kwa uchumi wa Amerika na kipaumbele chake cha kimataifa. Uchina ni kiongozi katika uvumbuzi wa teknolojia ya kizazi cha tano, uvumbuzi wa kizazi kijacho cha mawasiliano yasiyounganishwa kwa waya, na muhimu zaidi, mlango wa kufikia akili ya bandia. Bodi ya Uvumbuzi wa Kujihami ya Amerika inayo jumuisha mwenyekiti wa Alphabet Eric Schmidt, muasisi wa LinkedIn Reid Hoffman na Walter Isaacson, mwandishi na afisa mkuu mtendaji wa zamani wa Taasisi ya Aspen aliandika: “Kiongozi wa 5G atafaulu kupata mabilioni ya dolari kama mapato katika muongo mmoja ujao, huku kukibuniwa na nafasi nyingi za kazi katika sekta nzima ya teknolojia isiyokuwa na waya … Nchi inayo miliki 5G itamiliki uvumbuzi aina nyingi na kuweka udhibiti kwa dunia yote. Kutokana na sababu zinazofuata, nchi hiyo kwa sasa haitarajiwi kuwa Amerika.” (ZDNet).

4- Kwa taarifa hiyo, kizazi cha tano cha uvumbuzi “G5” kiko kasi mno, huku watafiti wakitangaza kuwa vipimo vya kasi ya mawasiliano kupitia teknolojia ya G5 vimerekodi kasi ya hali ya juu, terabyte 1 kwa sekunde, ikijulikana kuwa kasi hii ni mara 200 zaidi ya kizazi cha sasa. Kwa mujibu wa vipimo vilivyo fanywa na timu ya utafiti kutoka Kituo cha Uvumbuzi wa 5G katika Chuo Kikuu cha Surrey nchini Uingereza, faili moja ambayo ni kubwa mara 100 kuliko filamu nzima yaweza kupakuliwa kwa sekunde 3. Kasi hii mpya ni ya juu zaidi kwa mara takriban elfu 65 kuliko kasi wastani ya upakuaji katika mitandao ya 4G. Idadi ya ala zinazo unganishwa na angavu mwaka huu inatarajiwa kuwa kati ya ala milioni 50 na 100, hivyo ipo haja ya kuwepo kwa nyuzi bendi mpya na tofauti ili kukidhia mahitaji haya mapana kwa ajili ya uunganishaji wa angavu. Ama kuhusu ni vipi G5 inavyo fanya kazi kiufundi, teknolojia inayojulikana kama “MIMO” inayo maanisha “multiple-input multiple-output” itacheza dori kuu katika oparesheni ya viwango vya nyuzi za mitandao ya 5G, teknolojia ya MIMO inatumia antenna kadhaa ndogo ndogo ili kuhudumia mtiririko binafsi wa habari ‘data’. Samsung imetegemea teknolojia hii ili kutoa kasi za hali ya juu za upakuaji, na mitandao ya 5G inatarajiwa kutumia vituo zaidi vya upeperushaji”. (Al-Arab 13/08/2017).

5- Mnamo 2017, Schmidt alifichua katika Kongamano la Kiuchumi la Kiulimwengu “haitachukua muda mrefu kabla ya Uchina kuipiku Amerika katika uundaji wa akili ya bandia ilioendelea” (World Economic Forum). Akili ya bandia inajitokeza katika:

– Matumizi ya chatbots za akili ya bandia ili kufahamu kwa haraka matatizo ya mteja na kutoa majibu yaliyo barabara zaidi.

– Matumizi ya wasaidizi walio na akili ya bandia ili kutathmini habari muhimu kutoka katika mfumo mkubwa ulio na habari nyingi ili kuimarisha upangiliaji.

Wataalamu wanaelekeza katika maslahi na uwekezaji mkubwa katika akili ya bandia katika miaka michache ijayo, na Deloitte inakadiria kuwa dolari bilioni 57.6 zitatumiwa kwa ajili ya akili ya bandia na usomaji kupitia mashini kufikia 2021, mara tano zaidi kuliko mnamo 2017.

6- Haishangazi kwa Trump kuipinga hadharani Huawei, ambayo inazalisha G5, na ametaja katika matukio kadhaa tishio linaloletwa na kampuni hiyo ya Uchina. Trump alisema katika mkutano wa mwisho wa NATO, “Sidhani ni tishio kwa usalama, ni hatari kwa usalama”.

(Business Insider) Kwa sababu hii, Amerika imezishinikiza nchi nyingi za Kimagharibi (Italia, Uingereza, Ujerumani, nk.) kuiondoa Huawei kutokana na utafutaji zabuni au kuweka G5 nchini mwao, yote haya ni chini ya kisingizio cha kirongo cha ukiukaji wa usalama. Amerika vilevile imeiomba Canada kumkamata Meng Wanzhou, afisa mkuu wa fedha wa Huawei kwa madai ya kukiuka vikwazo vya Amerika dhidi ya Iran. Inachotaka Amerika ni kupiga tu marufuku mtandao wa G5, na Trump vilevile amezuia mauzo ya vipande (chips) vya silicone kwa Uchina.

7- Wachina kwa muda mrefu wamefanya kazi kuwa huru kiteknolojia chini ya mpango wa Uchina 2025, lakini jinsi Waamerika walivyoingiliana na Huawei na kampuni nyinginezo za Uchina imeongeza juhudi za Uchina za kupata uhuru kamili katika teknolojia muhimu. Wachina walikuwa wametangaza mipango ya kuunda nidhamu yao ya uendeshaji (OS) kufikia 2022, lakini mlango huu ukafungwa ila kwa IBM, Microsoft, Dell na kampuni nyinginezo za Amerika. Zaidi ya hayo, Uchina inapanga kuunda vipande vya silicone vyake mwenyewe. Imeongeza mshahara maradufu kwa maelfu ya wahandisi wa vipande vya silicone kutoka Taiwan na ambao wamekuwa wakihamia Uchina tangu miaka michache iliyopita. Wachanganuzi wa Amerika wanatarajia kuwa ndani ya miaka mitano hadi saba, Uchina itapata uhuru katika sekta ya vipande. Kupitia kufuata hatua hizi, Beijing itatengeza mapato makubwa kutokana na uchumi mpya wa akili ya bandia.

8- Amerika inafanya kila iwezalo kuuzuia uwezo wa Uchina wa kuchukua usukani katika mfumo wa “G5” na akili ya bandia, kwa sababu teknolojia hii ni muhimu kama ambavyo mashini ya mvuke, umeme na vipande vya silicone ni muhimu. Teknolojia hizi ndio injini ya uzalishaji na ukuaji wa kiuchumi. Hivyo basi, vita vya sasa vya kibiashara ni zaidi kuliko kuwa ni vita tu vya kibiashara vya kukabiliana na mizani ya kibiashara kati ya Amerika na Uchina, lakini fauka ya hayo, ni vita vya kiteknolojia, hususan G5, na kuna uwezekano, kwa mujibu wa habari zilizoko kwa sasa, kuwa ulimwengu utakuwa na mfumo wa kiteknolojia wa kambi mbili; Magharibi ikiongozwa na Amerika, na ulimwengu uliosalia ukiongozwa na Uchina. Na iwapo mfumo wa kiteknolojia wa Uchina utatawala Eurasia, uwezekano wa Uchina kuvitishia vipaumbele vya Amerika katika ulingo huu utaongezeka.

Hivyo basi, makubaliano ya kibiashara kati ya Amerika na Uchina, hata kama yatakamilishwa na kisha kutiwa saini katika awamu zake zote mwaka mmoja baadaye, kama alivyosema Trump: “Idara yake hivi punde itaanzisha majadiliano ya Awamu ya Pili ya makubaliano ya kibiashara kati ya Amerika na Uchina bali huenda akasubiri kukamilisha makubaliano yoyote hadi baada ya uchaguzi wa uraisi wa Novemba … (Bawabat Al-Ain 10/01/2020). Hivyo basi, hata kama yatatiwa saini katika hatua zake za mwisho, inatarajiwa kuwa haitakuwa zaidi isipokuwa tu mapumziko ya mpiganaji, hususan katika uwanja wa kizazi cha tano cha teknolojia kwa sababu Amerika kamwe haikubali kuwa mshindani wa Uchina; hata kama Uchina inakubali, kiburi cha Amerika kinaizuia kukubali!!

17 Jumada I 1441 H

Jumapili, 12/01/2020 M

Maoni hayajaruhusiwa.