Mafunzo Katika Kuzushiwa Kifo

0

Karibuni mwanasiasa Agostino Mrema katangaza dhamira ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliomzushia na kumtangazia kifo,  akitaka wamfidie kiasi cha shilingi milioni 20.

Kwa mujibu wa Mrema, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, mgombea uraisi wa Jamhuri ya Muungano, Mbunge, aliyewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali nyeti na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha TLP na Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, waliotenda jambo hilo la kumzushia kifo ni maadui wake, ndio maana anaamua kuchukuwa hatua za kuwaburuza katika  mchakato wa kisheria.

Hakuna anayepinga kwamba kuzushiwa kifo sio jambo jema, kwa kuwa huleta usumbufu, taharuki na mtafaruki  kwa ndugu, vipenzi , jamaa na marafiki kutokana na taarifa hiyo ambayo hatima yake huwa ni uwongo,  na kwa udhati uwongo na uzushi ni tabia mbaya katika maadili  ya kidini na hata katika hali ya kawaida tu  kibinadamu.

Hata hivyo, taarifa za kutangaziwa kifo ukizichukulia kwa upande mwengine, kuna mambo ya kujiuliza na kujifunza. Kwa mfano, kwanini kuna watu wakutangazie kifo, kwa tafsiri ya haraka, maana yake watu hao hawana haja ya uwepo wako katika hii duniani, ikiwa kuna watu wamediriki hayo, maana yake wanakuchukia, hapo ndio huja haja ya kutathmini muamala wako na watu mbalimbali.

Lakini kwa upande mwengine, kutangaziwa na kuzushiwa kifo licha ya kuwa si jambo zuri,  lakini huwa ni tanbihi na tahadhari kwa mwenye kutangaziwa ikiwa atazingatia kwa makini.  Ni kweli kuzushiwa kifo huwa ni uwongo,  lakini  kiasili, ni uwongo wa jambo la kweli kwa kila mwanadamu, kwa kuwa kufa huwa ni suala la ukweli ila huwa muda wa kujiri kwake ndio haujafika.

Kifo ni kielelezo cha mambo kadhaa katika maisha yetu ya kila siku, na miongoni mwa mawaidha makubwa ambayo kila mara hupaswa kuzingatiwa kwa umakini wa hali ya juu.

Kifo ni kielelezo cha kuwepo Mmiliki wetu wanadamu kando na wanadamu wenzetu, Mmiliki ambaye huingilia maisha yetu bila ya ridhaa wala matakwa yetu. Na kwa udhati hakuna mwanadamu anayemiliki kifo hata kama atadai hivyo kama alivyodai Namrud, mfalme wa zama za Nabii Ibrahim As na wengine.  Mwenye kuleta madai ya umiliki wa kifo hata yakiambatana na vitisho kiasi gani dhidi ya wengine, mwisho wake naye hufariki. Hiyo ni dalili tosha kwamba yeye sio mmliki wa kifo. Kwa kuwa kama anakimiliki kifo angekizuiya kisimfike.  Na kwa kuwa kifo ndiyo kinachotufanya tuwepo au tusiwepo ulimwenguni, maana yake Mmiliki wa kifo ni Mwenyezi Mungu Mumba ambaye pekee ndiye anajua siri ya kuubakisha uhai au kuuondoa, kwa kuwa Yeye ndie Muumbaji.  Kwa hivyo, uwepo wa kifo unatosheleza kuthibitisha kiakili kwamba kuna Mwenyezi Mungu, Muumba.

Pili, kifo ni kielelezo cha udhaifu wetu wanadamu, kwa kadiri tutakavyokua, kama kuna mwenye nguvu, cheo kikubwa, umaarufu, mali,  hadhi, elimu nk. siku moja kifo kitamchukuwa bila ya matakwa yake, na kuacha kila kitu hapa hapa duniani. Na asili hii ndio tabia ya kimaumbile ya kila kiumbe, kina mipaka maalumu iwe umri au umbo, kinahitajia kiumbe kingine, na mwisho huondoka kamwe.

Tatu, kifo kinatulazimisha kupata muongozo wa Muumba kutumia maishani mwetu. Ukiangalia kwa makini kiakili, ni wazi mmiliki wa kifo ndio mmliki wa uhai, na kamwe haiwezekani kuwepo wamiliki wawili tofauti, kwa kuwa huwezi kuondoa uhai kwa kifo, kama hujui siri ya uhai ulivyo.

Aidha, haiwezekani Muumba ajue siri ya kuumba uhai, kisha Muumba huyo huyo akose kuwa na muongozo wa kumpatia mwanadamu juu ya namna ya kuutumia uhai huo. Hali hiyo inatulazimisha tukiri kuwa mwanadamu katika dunia hii lazima kapatiwa muongozo fulani na Muumba wa uhai juu ya namna ya kuutumia uhai wake, na kamwe hakuachiwa tu bila ya muongozo wowote au kufanywa jambo hilo kuwa jukumu binafsi la mtu kujiafutia muongozo kwa mujibu wa akili yake. Hii ni changamoto ambayo kila mwanadamu awe Muislamu au mwengineo anapaswa kuizingatia kwa makini sana.

Uislamu licha ya kujua mwanadamu atajitahidi kwa kupitia akili yake kujaribu kujibu maswala ya msingi yanaomkabili likiwemo suala la kifo na baada yake, lakini ulitambua wazi kwamba kuna maswala mwanadamu atakwenda kombo katika majibu yake.  Kwa kuwa majibu ya maswala hayo yanahitaji chanzo kingine cha elimu, kando na maarifa ya kawaida ya kuhisika ya mwanadamu.  Chanzo hicho ni wahyi, ambayo ni mawasiliano ya Allah Taala kupitia Mitume As. Kwa kupitia wao Mitume As. wanadamu hupata ufafanuzi juu ya maswala ya msingi ambayo yakifunguka, kila kitu kitakuwa wazi kwa mwanadamu. Maswala kama chanzo cha mwanadamu, lengo la kuumbwa kwake na nini kinafuatia baada ya maisha ya duniani.

Kwa ufupi, Uislamu umekuja na majibu rahisi na fafanuzi, kwa kufungamanisha maisha ya mwanadamu duniani na maisha ya kabla.  Yaani, nyuma ya mwanadamu kuna Muumba aliyeumba uhai na mwanadamu, pia Uislamu umefungamanisha maisha ya dunia na maisha ya baada. Yaani, kila anachokitenda mwanadamu katika maisha haya mafupi ya ulimwenguni kitahesabiwa na kuwajibishwa mwanadamu katika maisha yajayo ya akhera.

Kifo sio suala la mjadala kwa kuwa kipo tu, suala hapa ni kujitayarisha nacho kwa kufungamanisha matendo ya maisha yetu katika dunia hii na maisha yajayo kwa mujibu wa muongozo wa  aliyetupa uhai wake.

قُلْ إِنَّ الْمَوْتَ الَّذِي تَفِرُّونَ مِنْهُ فَإِنَّهُ مُلاَقِيكُمْ ثُمَّ تُرَدُّونَ إِلَى عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَيُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ (الجمعة: 8

“Sema hakika ya mauti mnayoyakimbia, bila ya shaka yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kujua yaliyofichikana na yaliyowazi. Hapo atakujuzeni mliyokuwa mkiyatenda.”

(TMQ 62:8)

20/01/2018

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.