Maamuzi ya Mahkama Juu ya Umri wa Ndoa Yatahamasisha Zinaa na Utovu wa Maadili
Habari:
Mahakama ya Kuu ya Rufani Tanzania imeshikilia uamuzi wake wa mwaka 2016 kuzuiya ndoa kwa wasichana chini ya umri wa miaka 18. Hivyo, kuanzia sasa jambo hilo ni kinyume cha sheria, hatua iliyojiri kufuatia mpambano wa kisheria uliofanywa na taasisi ya utetezi wa watoto na akinamama
Maoni:
Sheria ya Ndoa ya Tanzania (1971) imeweka umri wa chini kwa msichana kuolewa ni miaka 15 kwa kupatikana idhini ya wazazi, na miaka 18 kwa wavulana. Pia inaruhusu ndoa ya wenye miaka 14 ikiwa mahkama itatoa ridhaa.
Ndani ya mwaka 2016 Mahakama Kuu ya Rufaa katika maamuzi yanayochukuliwa ya aina yake ilitamka kwamba vifungu hivi viko kinyume na katiba na kuiamuru serikali kuongeza umri wa ndoa kuwa miaka 18 kwa wasichana na wavulana. Katika hali hiyo serikali ilikata rufaa dhidi ya maamuzi hayo ya 2016. Hatimae ndani ya wiki ya mwisho ya Oktoba mwaka huu, Mahakama Kuu ya Rufani ikatupilia mbali rufaa ya serikali na ikashikamana na maamuzi yake ya awali ya mwaka 2016.
Uamuzi huu wa Oktoba uliopitisha umri wa msichana kuolewa kuwa ni miaka 18 “umepokelewa kwa furaha na azaki zinazodai kutetea ustawi wa watoto na wasichana kwamba ni ushindi mkubwa mno hususan kwa taasisi ya ‘Msichana Initiative’ iliyoongoza juhudi za pingamizi za kisheria.
Taasisi za kisekula zinazodai kutetea haki za wasichana, kinamama na watoto kwa mujibu wa mtazamo wa kisekula zimeenea nchini Tanzania na kila mahala, zikitumiwa na mataifa ya kibepari kusambaza sumu ya usekula bila kujali mila wala dini za watu. Kufuatia maamuzi haya taasisi hizi zinadai kuwa eti Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 iliyoruhusu ndoa katika chini ya miaka 18 inavunja haki msingi za msichana katika kuamiliwa kwa usawa, kupata elimu na kuathiri heshima yake. Ilhali taasisi hizo zinajigubika upofu wa kutotambua kuwa ndoa mara wanajamii wanapofikia balegh ni kilele cha heshima na ulinzi kwa jamii.
Hapana tembe ya shaka kuwa nyuma ya mabadiliko haya kuna mkono wa wakoloni mabepari wakihamasisha fikra za ‘uhuru’, fikra sumu kwa ustawi wa jamii. Na hili linadhihirika waziwazi namna kunavyotetewa jambo la kuchelewa kwa ndoa ilhali hakuna hatua zozote thabiti kumkinga binti na uzinifu na aina nyengine za maasia. Lakini ukweli hapa ni kuwa, kwa mtazamo wa kisekula hayo yote sio muhimu, lillilo muhimu ni kuzuiya binti asiolewe mpaka afike umri wa miaka 18 tu, hiki kwa hakika ni kichekesho !
Kwa mujibu wa tathmini za Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch, wasichana watatu kati ya kumi huolewa kabla ya kutimiza miaka 18. Kitu kinachodhihirisha kuwa wazazi wanachukulia ndoa kama ngao kwa mabinti zao.
Matokeo yaliyotajwa kuweza kutokea endapo ndoa zitakuwa chini ya miaka 18 kama kuathirika afya ya binti wakati akiwa mja mzito, unyanyasaji wa majumbani na mimba kusitisha fursa ya elimu haziingii akilini. Kwa sababu zote huibuka kutokana na kushindwa kwa mfumo wa kibepari kulinda afya za watu, kuzuiya unyanyasaji wa majumbani, kuwa na huduma duni za afya na kuwa na sera dhaifu za elimu. Zaidi ya hayo, kunadhihirika kuchanganyikiwa waziwazi kwa mfumo wa kibepari kwa kutozingatia maumbile ya mabinti na wanadamu kwa jumla.
Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Rufani umepokelewa kwa mikono miwili na serikali kwa kisingizio cha kuheshimu haki za binadamu. Lakini kiuhalisia kunaonekana sura mbili (unafiki) za serikali katika kushikamana na zinazoitwa haki za binadamu. Kuna qadhia nyingi ambazo zinagongana na kinachoitwa haki za binadamu nchini Tanzania kama kushikiliwa kwa dhulma watu wengi hususan Waislamu wakiwemo wanavyuoni kwa miaka mingi bila ya kesi zao kusikilizwa, yote haya hayashughulikiwi na serikali inayodai kuheshimu haki za binadamu.
Kwa kukhitimisha, kwa upande wa Uislamu kila kitu kimewekwa wazi katika fiqhi/ sharia yake. Msichana ni ruhusa kuolewa mara tu anapofikia balegh. Amma kuhusu unyanyasaji majumbani, Uislamu umefafanua haki na mjukumu ya kila mmoja ndani ya ndoa, na pindi mmoja wao anaporuka mipaka yake, qadhi atatoa ufafanuzi wa hukmu baina yao. Pia sera ya Uislamu katika elimu imeweka wazi kuwa utafutaji elimu ni mchakato endelevu wakati wote. Elimu na ndoa huamiliwa tofauti bila ya kuathiriana bali hupatanishwa pamoja, huku kukizingatiwa jukumu la ulezi kwa mama kwa kupewa nafasi maalumu
#MuhammadNuruYetuKigezoChetu
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania.
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir.
Maoni hayajaruhusiwa.