Kumbukumbu ya Mama Wa Waumini Bi. Khadija Bint Khuwayld (Ra

بسم الله الرحمن الرحيم

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa furaha na majonzi kwa munasaba wa kumbukumbu ya Ummul Muuminin Bi. Khadija bint Khuwayld ra. Mwanamke mtukufu na mke wa mwanzo wa Mtume wetu SAAW.

Katika mwezi huu mtukufu ndipo Mama huyu mtukufu ra. alipoikubali nuru ya Uislamu na kuupata utukufu wa kuwa mwanamke wa mwanzo kuikubali risala ya Uislamu na nyumba yake kuwa mahala pa mwanzoni kushuka wahyi mtukufu kutoka kwa Muumba mbingu na ardhi.

Aidha, ndani ya tarehe 10 ya mwezi huu wa Ramadhan ndipo alipofariki dunia mama huyu mtukufu na kumuacha Mtume SAAW na Waislamu katika majonzi, huzuni na simanzi isiyomithilika hususan kwa kuwa kifo chake kilipishana kwa muda mfupi wa miezi miwili tu na kifo cha ammi yake Mtume SAAW.

Ni umakini na unyenyekevu wa mama huyu ndio uliyompelekea kufikia hatua ya kuikubali nuru ya Uislamu kinyume na walio wengi katika jamii ya Makka. Kwa sababu lau tukisema sababu ya kusilimu kwake ni kuwa kwake mke wa Mtume SAAW, hilo sio sawa kwa kuwa wako wanawake kadhaa katika historia waliokuwa wake za Mitume As. ambao nuru ya tawhid ilikuwa inaangaza ndani ya majumba yao, lakini kamwe wao hawakuikubali. Mfano, ni mke wa Nabii Nuh As. na Nabii Lut As.

Fadhila, utukufu, hadhi na nyota ya bi Khadija ra. ilidhihirika mapema katika maisha yake kabla hata ya kuanza kuamiliana na Mtume SAAW. Kama alivyokuwa Mtume SAAW kabla ya Utume, kiasi cha jamii ya Makka kumpa cheo cha Aswadik ul-amiin (mkweli muaminifu) bi. Khadija nae katika jamii hiyo alikuwa akiitwa Atwahira (aliyetakasika).

Alikuwa bibi huyu na khulka njema na murua wa kupigiwa mfano katika jamii ya Makka. Licha ya umri wake kusonga na kuwa mjane kwa kufiliwa na waume wawili, bado utukufu na haiba yake ndani ya jamii ya Makka ilikua juu, na wanaume mbalimbali walimkabili kumposa lakini alihisi hawakuwa chaguo muwafaka.

Bi Khadija alibakia katika hali hiyo mpaka alipoamiliana na Mtume SAAW katika biashara zake ndipo alipokuja kugundua haiba njema, karama ya Mtume SAAW iliyoambatana na barka katika biashara na uaminifu wa darja ya juu, bi Khadija akaona Mtume SAAW ni mtu muwafaka wa kuwa mume wake, licha ya ukweli kuwa Mtume SAAW alikuwa mtu mwenye kipato cha chini.

Baada ya kupata taarifa za kuaminika kutoka kwa mfanyakazi wake aliyeambatana na Mtume SAAW katika masafara wa kibiashara Sham Bi Khadija alivutika na Mtume SAAW na kumtuma shoga yake Bi Nafisa kumshauri Mtume SAAW juu ya suala la ndoa

Ndoa ya Mtume SAAW na bi Khadija ikawa ufunguo wa kila kheri kwa pande zote mbili. Bi Khadija aliyekulia katika familia yenye mwanazuoni wa Ahlul kitaab Warqa bin Naufal ambae aliwapasha khabari ya ujio wa Mtume, kwa haraka bila ya kufanya kosa bi Khadija alimkubali Mtume SAAW

Kuanzia hapo na katika miaka 25 ya ndoa yao, Bi. khadija akawa msaada, faraja, maliwazo, mfadhili na muhimili mkubwa na muhimu katika kujitolea hali na mali yake kwa ajili ya Mtume SAAW na Uislamu kwa jumla.

Akaambatana bega kwa bega na Mtume SAAW hususan katika kipindi kigumu cha miaka kumi ya ulinganizi bila ya kurudi nyuma wala kutetereka. Akapata hadhi ya kuwa mama wa mwanzo wa Waumini, akawa mama wa kizazi chema na Mtume SAAW atabakia katika nyoyo za Waumini kwa mapenzi makubwa, kwa kuwa alikuwa ni kipenzi cha Mtume wetu SAAW, aliyediriki kusema :

.. Aliniamini mimi , wakati watu wakinikadhibisha, akaniswadikisha mimi wakati wengine wakinikadhibisha, akanishirikisha katika mali yake wakati wengine wakininyima, na mwenyezi Mungu akaniruzuku watoto nae’

12 Ramadhan 1441 Hijri – 05 Mei 2020

Ummu Ammar

Maoni hayajaruhusiwa.