Kuangazia Kushtadi Kwa Joto Bara La Ulaya
بسم الله الرحمن الرحيم
Tabia nchi ni mkusanyiko wa halijoto, unyevuanga, kanieneo ya angahewa, upepo, usimbishaji na tabia nyingine zinazoathiri hali ya hewa katika eneo fulani kwa muda mrefu. Tofauti kati ya tabia nchi na hali ya hewa ni kuwa tabia nchi ni jumla ya halihewa zote zinazoweza kutokea mahali fulani kwa muda mrefu, kwa takribani miaka thelathini(30).
Tabia nchi hubadilika kwa sababu ya athari ya ongezeko la nguvu za miali ya jua ambayo huongezeka kutokana na shughuli za kiuchumi za binadamu kama vile kilimo, viwanda na ukataji miti zinazosababisha gesi zinazozuia miali hiyo ya jua kuwa nzito na hivyo kushindwa kuzuia miali hiyo ipasavyo hii ni kwa mujibu wa Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) katika ripoti yake muhimu, ripoti ya tano ya mwaka 2013. Kwa kifupi hali hii ndiyo hupelekea kuongezeka kwa joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi
Hali ya hewa ya kiangazi katika nchi mbali mbali duniani imepelekea kwa mara nyengine kuongezeka kwa joto kali kupita mipaka na mioto katika mapori na nyika sehemu kadhaa ulimwenguni hususan Bara la Ulaya na kuleta madhara makubwa kiekologia, kiuchumi na kibinadamu.
Ongezeko la joto katika dunia ni hali ambayo joto la mazingira huwa zaidi ya kawaida. Katika hali ya kawaida joto la mwili huwa ni nyuzi joto 98.6F au 37C na joto la mazingira huwa ni nyuzi joto 82F au 28C.
Joto la mazingira linapozidi huathiri joto la mwili na mazingira kiujumla na kupelekea majanga mbalimbali kama tunavyoshuhudia leo katika ulimwengu hasa nchi za Kusini magharibi ya Ulaya kama Ureno, Uhispania, Ugiriki nk. zimeshuhudia madhara na majanga makubwa zaidi kutoka na hali hii ya hewa, kwani joto la mazingira likifika kuanzia 40C na zaidi huweza kusababisha vifo.
Kiwango cha joto katika nchi za Ulaya kiliongezeka katika mwezi wa Julai mwaka 2022. Uingereza imerekodi kiwango kilichovuka 40C kwa mara ya kwanza katika historia yake, miji kama Nantes wa nchini Ufaransa imerekodi kiwango cha joto cha sentigredi 42.
Tarehe 19/07/2022 joto lilifika 47C nchini Ureno na 40C nchini Hispania hali ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Suala hili la kuongezeka kwa joto katika nchi za Ulaya hii si mara ya kwanza kwani Ulaya ilikumbwa na joto kubwa kwa mujibu wa Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO), iliwahi kutokea mwaka 1029, 2003, 2016, na 2019 na limetokea tena mwaka huu 2022. Umoja wa Mataifa unasema kuwa mawimbi ya kuongezeka joto yatajitokeza mara kwa mara kwa sasa hadi kufikia angalau mwaka 2060. Hivyo kinachotarajiwa ni kuendelea kwa mfululizo wa matukio haya Ulaya na duniani kote kiujumla.
Ongezeko la joto husababisha madhara mengi na hata vifo. Kwa mfano, wimbi la joto lililoisibu Ulaya mwaka 2003 lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 70,000.
Nchi za Kusini magharibi ya Ulaya kama Ureno, Uhispania, Ugiriki nk. zimeshuhudia madhara na majanga makubwa zaidi kutoka na hali hii ya hewa.
Mwanzoni mwa mwezi wa Julai joto kali barani Ulaya limesababisha vifo vya watu 1,063 nchini Ureno huku hekta 15,000 za misitu yake ziliangamia kwa moto.
Nchini Uhispania joto lilishtadi na watu 678 walifariki. Joto hilo lilipelekea kuhamisha watu katika baadhi ya maeneo kwa khofu ya moto. Pia nchi hiyo ilitoa kikosi cha cha dharura chenye askari 600 kukabiliana na hali hiyo, na hekta 14,000 za misitu yake ziliteketea kwa moto.
Ndani ya Ufaransa katika maeneo yake ya Kusini Magharibi kikosi cha zimamato chenye askari kama 1,200 na ndege 5 kilipambana na moto ilhali kiasi cha eka 24,700 ziliangamia na watu zaidi ya elfu 35 walihama makazi yao nchini Ufaransa na Ugiriki.
Kwa upande wa Italia, joto liliuwa kiasi cha 11 mwanzoni mwa mwezi wa Julai. Amma upande wa nchi ya Ugiriki moto ulishtadi katika visiwa vyake vya Crete. Pia nchi ya Moroko katika milima yake ya kaskazini ililazimika kuhamisha familia 1000.
Uingereza Baraza lake la mawaziri lilikutana kujadili hali ya joto la kutisha nchini humo kiasi cha kufikia serikali kushauri raia wasitumie usafiri wa Umma ila pakiwa na ulazima.
Ongezeko la joto limepelekea kuongezeka kwa kina cha bahari na kuyeyuka kwa barafu, Antarctic imevunja rekodi ya kiwango kikubwa cha joto nyuzi joto 18.3C, barafu zinazoyeyuka zinaweza kufikia asilimia 91 ya maji katika majiji kama Huaraz. Hali ya ongezeko la joto limepelekea hali ya usalama wa chakula kushuka na ukame.
Chanzo kikubwa cha kushtadi huku kwa joto ni mgogoro wa kimazingira ambao ni tatizo sugu chini ya mfumo wa kibepari.
Umoja wa Mataifa(UN) tangu kuundwa kwake mwaka 1945 umeanzisha mashirika mbalimbali kama vile Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mwaka 1950, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) mwaka 1972 na Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) mwaka 1988.
Kumekuwa na mikataba na makubaliano mbalimbali kuhusu utunzaji wa mazingira duniani mfano; Kongamano la Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC-Framework Convention on Climate Change) wa mwaka 1992, Mkataba wa Kyoto (Kyoto Protocol) wa mwaka 1997, Makubaliano ya Paris (Paris Agreement) wa mwaka 2015, Mkataba wa Vienna wa Utunzaji wa Ozoni (Vienna Convention for the Protection of the Ozone Layer) wa mwaka 1985, Mkataba wa Montreal (Montreal Protocol ) wa mwaka 1987,nk . Pia kuna mikataba na makubaliano ya kikanda zaidi ya 1,300 na makubaliano baina ya nchi mbili yapatayo 2200.
Licha ya mikakati na mashirika yote hayo, bado ulimwengu umeshindwa kutatua mzozo wa kimazingira unaosabanishwa na uharibifu wa mazingira unaopelekea ongezeko la joto duniani kila kukicha.
Amma sababu kubwa ya kushindwa kutatuliwa mgogoro wa mazingira ni kutokana na msingi mkuu wa sera zinazotokana na mfumo unaoendesha ulimwengu leo hii, yaani mfumo wa ubepari ambao msingi wake ni maslahi binafsi ambayo ndiyo huwa muongozo katika sheria na sera zake za kisiasa, kiuchumi na kijamii bila kujali umuhimu wa vitu vingine.
Kipaumbele kikubwa kwa serikali za kibepari imekuwa ni ukusanyaji wa kodi na mapato na kutupilia mbali mahitaji mengine ya binadamu hususan utunzaji wa mazingira. Uharibifu wa mazingira unaopelekea matatizo ya ongezeko la joto duniani na katika nchi za hususan Ulaya ni matunda ya mfumo huu fisidifu.
Masuluhisho yanayotolewa na mataifa makubwa ya kibepari kimsingi yanashindwa kutatua tatizo msingi na hulenga zaidi utatuzi wa athari na si tatizo lenyewe. Ukiangalia kwa makini utaona kuwa matatizo ya kimazingira yanasababishwa na mambo kadhaa yanayohusiana na sera za kiuchumi, kisiasa, kijeshi na maadili binafsi ya kiroho ya mtu mmoja mmoja. Hivyo utatuzi wake ni lazima uwe wa kiujumla wa kimfumo ambao utaweza kubadilisha sera za kiuchumi, kisiasa, kijeshi na maadili binafsi ya kiroho ya mtu mmoja mmoja katika jamii.
Uislamu unatambua mizunguko miwili katika masuala haya ya kimazingira mfano ongezeko la joto na kuzuka kwa moto wa nyika kuwa kuna qadhaa ya Allah (SWT) ambayo hatuijadili, kwani Allah SWT Ndiye anayejua kiasi cha joto, baridi na athari zake na anafahamu kutokea kwa moto, kiasi, muda na athari zake nk. Huu ni mzunguko wa kwanza ambao upo nje na uwezo wa binadamu, na binadamu hawezi kudhibiti.
Amma mzunguko wa pili ni ule unaohusiana na yale ambayo binadamu anaweza kuyadhibiti, na haya huhesabiwa kutokana nayo binadamu mfano uzembe, uvivu, nk . Sera mbovu za kibepari kuhusu mazingira ni katika vitu vinavyoingia katika mzunguko huu ambazo hutakiwa kufutwa na kuondolewa na badala yake kutabikishwa sera za Kiislamu ili kuepusha majanga kama haya.
Ama Uislamu kama mfumo kamili wa maisha una suluhisho la kila tatizo la binadamu, hivyo hata hili la uharibifu wa mazingira pia Uislamu umefafanua suluhisho lake. Uislamu unahimiza uwajibikaji wa matendo kibinafsi na huandaa mazingira rafiki katika hilo, unaruhusu kutumia na kufurahia vitu vizuri lakini umekataza israfu. Hii inamaanisha kutakuwa na uhitaji mdogo wa bidhaa na hivyo itapunguza taka, uchafuzi na uharibifu unaosabanishwa na viwanda.
Aidha, Uislamu unautazama ulimwengu kama ni mali ya Allah (SWT) na Yeye ndiyo mwenye haki ya kutunga sheria zinazohusu nyanja zote za maisha. Hivyo, fikra ya Kiislamu huathiri matendo binafsi ya mtu na hupeleka mambo yao kwa mujibu wa Quran na Sunnah. Hali hii itakuza uchamungu na kufanya watu kujiepusha na mambo yanayoleta madhara, hivyo itaepusha uchafuzi, kulinda vyanzo vya maji, kuweka miundombinu bora na huduma bora za kijamii ili kurahisha shughuli za kimaisha bila kuathiri mazingira, kusitisha shughuli za viwanda zenye kuathiri mazingira na kutafuta njia mbadala za uzalishaji wa bidhaa, kuthaqafisha Ummah juu ya ubaya wa kuwadhuru viumbe na malipo yake ni adhabu ya Allah SWT.
Yametokea majanga mengi katika tarekh ya Khilafah na tumeona ni kwa jinsi gani makhalifa walichukua hatua za dhati, tena majanga mengine yalikuwa nje ya mipaka ya Khilafah. Mfano janga la njaa kwa nchi ya Ireland mwaka 1845, ambako Khalifah alituma chakula na pesa kiasi cha pounds 10, 000 ambacho wataalamu wanasema kwa miaka hii ni sawa sawa na dola 1,682, 280.
Ulimwengu leo una kiu ya uongozi wa Khilafah ili kuja kuunusuru na majanga na kuleta rehma kwa wanadamu wote.
Risala ya Wiki No. 141
10 Muharram 1444 Hijria / 07 Agosti 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.