Khilafah na Al Mahdi

بسم الله الرحمن الرحيم

Husema baadhi ya watu ambao waliochanganyikiwa na uhakika wa Uislamu na Twabia za hukmu zake kua “Khilafah hitakuja ila kupitia mikono ya imam Mahdi wala haina haja ya kuifanyia kazi” Kihakika ufahamu huu ni ufahamu wa kimakosa na upotoshaji ufahamu ambao umewafanya wengi kuacha kubeba jukumu la ufaradhi wa kusimamisha  khilafah, jambo ambalo limewatia katika dhambi, na kuhakikisha lengo la makafiri katika kuchelewesha kusimamisha khilafah na kumakinisha usekula (ilmania) katika miji ya waislamu, na kwa kuyarudi hayo Nasema wabillahi attawfiq:

Hakika kazi ya kusimamisha dola ya kiislamu; dola ya khilafah ambayo ni chombo cha utekelezaji wa hukmu za kiislamu, utawala wa waislamu wote kwa ajili ya kuhukumu na uislamu ndani ya mipaka ya dola  na kuubeba  ulimwenguni kwa njia ya Daawah na Jihad, Hakika kazi hii ni faradhi kubwa ambayo imethibiti ufaradhi wake katika kitabu, sunnah na ijmaa-swahaba radhi za Allah ziwaendee, na hakuna hata mmoja aliyesema kinyume na hivyo, kama asemavyo imam qurtubiy rahimahullah ila alie kuwa ni kiziwi kwani yeye ni kiziwi juu ya Sheria, na faradhi haina budi iwe na njia (Twariqah) ya kivitendo laa sivyo mwanadamu atakua ni mwenye dhambi, faradhi katika sheria haisubiriwi ifike Bali hufanyiwa kazi kama ambavyo sheria iliamrisha na matokeo yake huwa ni mikononi mwa Allah subhanah.

Njia ya kutekeleza faradhi hua inatokana na sharia kwa namna madhubuti namna ya kutekelezwa kwake, kwa mfano utekelezaji wa zaka Ni kutoa 2.5% katika Mali baada ya kufika (Nisab) kiwango cha kutolea zaka na kuzungukwa na mwaka (Al hawl), na kusimamisha Swala ni kwa namna ambayo tunasimamisha swala, na ufaradhi wa kusimamisha khilafah njia yake imebainishwa katika sheria nayo ni njia ya Mtume s.a.w katika kusimamisha dola ya kwanza ya kiislamu katika mji wa Madinah munawarah.

Faradhi hii haiwezi kusimama ila kwa njia yake ya kisheria, Na ambaye ataswali na kufunga akahiji na kutoa zaka atakua ameporomosha faradhi iliyo mabegani mwake, ama faradhi hii laaa (faradhi ya khilafah itakua bado imo mabegani mwake), kama ambavyo utowaji wa zaka utekelezaji wake hautoshelezi kwa kuswali, basi pia utekelezaji wa faradhi zote hakutoshelezi faradhi ya kusimamisha khilafah ila kwa njia yake ya kisheria, na pia kama ambavyo jihad haitoshelezi swala basi pia jihad haitoshelezi faradhi ya kusimamisha khilafah.

Njia ya kisheria ya kusimamisha khilafah ni njia ya Mtume s.a.w katika kusimamisha dola ya kiislamu ndani ya Madinah tukufu, na mtu ambaye anayo dalili kinyume na njia hii basi ailete, kwa sharti iwe njia hiyo inatokana na kitabu na sunnah na sio kwa mujibu wa matamanio ya nafsi (hawaa). Na yoyote ambaye atasema khilafah ni faradhi basi hoja imemlazimu kuifanyia kazi.

Khilafah itakaposimama itasimama katika eneo moja kisha itaanza kujitanua na wala haitosimama Mara Moja katika maeneo yote, Khilafah ni dola itakayotabikisha sheria na kuibeba kwa ulimwengu, kwa namna itakavyokua jina lake na laqabu ya mtawala wake, Tatizo sio katika namna ya kuiita ama jina la mtawala wake, awe khalifah au Raisi au imamu au amirul muumunina, kinachozingatiwa ni manhaj ya utawala na nidhamu (mfumo wa maisha) za maisha na kuhakikisha sharti za kisheria katika eneo ambalo itasimama dola ya kiislamu

Khilafah haitoteremka juu ya mbawa za malaika, Bali watapatikana watu ambao wataisimamisha, nayo ni Qadhia ya ummah na sio Haki ya kiungu kwa mtu maalum, Na hii yamaanisha kwamba kuifanyia kazi khilafah ni wajibu na dharura-lazima.

Imam Mahdi ikiwa yeye ndie mwenye kuisimamisha khilafah, Basi naye ni mtu na hatopigwa chapa kwenye paji la uso wake kua yeye ni Khalifah. Bali watu hawatojua kua yeye ndie aliyemaanishwa kua khalifah isipokua baada ya yeye kuhukumu kwa uislamu na kutabikisha uislamu vizuri kwa namna ambayo itahakikisha uadilifu na kuondoa dhulma, na watu hawatomfuata kirahisi hivyo, kwani watu walimkadhibisha (walimpinga) yule aliyekua mbora zaidi yake Mtume wetu mtukufu Muhammad s.a.w., Al mahdi sio mbora kwa Allah kuliko Mtume, Bali hapana budi kuwepo na ufahamu wa ndani kwa ummah na kuungana ahlul quwwah kuunusuru

Sharia haikuzitundika Hukmu za kiislamu kwa ajili ya kupatikana mtu maalum Bali Huku ni kuibeza  Dini Na Sheria, ni kama kusema kwamba kusimamisha faradhi ya khilafah na kutabikisha Dini inaambatana na kudhihiri kwa Mahdi ama kabla ya hapo Sio Faradhi!! Kwa ajili kama hiyo Ndio Sisi Tunaifanyia kazi Faradhi mpaka tuweze kuziweka mbali nafsi zetu Na dhambi, hata kama Imam Mahdi ndie atakayesimamisha khilafah, Basi Sisi Tumekusudiwa kuifanyia kazi na sio Kumtafuta Al Mahdi, Jukumu letu Sio Kumtafuta mtu Anayefaa kwa khilafah kwani khilafah haijasimama kamwe, Qadhia ( jambo la msingi) ni Kujenga dola Na mwamko wa ummah, je kweli fikra hizi za kuegemea zitaweza kuamsha ummah niambieni Wallah!!!?.

Hakika kukaa na kutegemea ghaibu (elimu iliofichikana) na kuwacha kazi inayotakiwa kisheria haijuzu kwa muislamu, na Halikuwaangamiza watu ila kutegemea qadari na ghaibu ambayo imewafanya kuzembea na kuwacha kusimama na mambo ambayo ni wajibu kwao, je kufikiria kwetu kumekua kama hali ya watu wenye kuangalia mambo kijuu juu na madarweshi? Je hazikua fikra hizi zisizoulizwa wala kupewa majukumu fikra zilizovunja khilafah uthmania!!?

Kama ilivyo katika usuli kua hadithi zinazotoa khabari zisipodhamini qarina (kiunganishi) inayotoa amri (Twalab) basi hubakia mujaradi wa khabari Na wala hailazimu kuifanyia kazi, na hadith za Al Mahdi zilizosahihi hazikudhamini qarina yoyote inayotoa amri (Twalab) isipokua tu kumfuata Mahdi na kumtii na hili limefunganishwa na kudhihiri kwake.

Zipo hadith kutoka kwa Mtume s.a.w zonazobainisha kua Al Mahdi atakuja baada ya kufa khalifah na hii yamaanisha khilafah itakua imesimama kabla ya Mahdi na kua sio yeye atakayesimamisha wa kwanza, amepokea ummuh salama radhi za Allah zimwendee asema:

“Nimemsikia Mtume s.a.w akisema: ( kutakua na ikhtilaf wakati wa kifo cha khalifah atatoka mtu kutoka bani hashim, atakuja makkah, watu watamtia nyumbani  akiwa hapendi watampa bay’ah akiwa kati ya Nguzo (Rukni) na Maqam, ataandaliwa jeshi kutoka sham mpaka wakiwa wamefika baydaai watazamishwa katika ardhi, watamjia makundi kutoka iraqi, na watu kutoka sham, atazuka mtu sham, na wajomba zake ni kalb ataandaliwa jeshi, Allah atawashinda, na hii ndio siku ya Al kalb, Mwenye khasara ni yule aliyekosa ghanima ya kalbi, atafungua mahazina, na atagawa mali, uislamu utamuangusha jirani yake chini, na ataishi kwa miaka saba au akasema: miaka tisa)”

amepokea twabarani katika Awsat, na ameitaja al haythamiy katika maj’mau’ azzawaid, na akasema (wanaume wake ni wanaume swahih) na hadith hii wameafikiana wapokezi wake na wenye kusherehesha kua khalifah aliyetajwa katika hadith hii ni Al Mahdi. Mwanzo wa hadith anasema (ikhtilafu wakati wa kifo cha khalifah) na hii yamaanisha kua khilafah itakua imesimama kabla ya kudhihiri Al imam Mahdi.

Hakika neno (khalifah) katika hadith iliyotangulia… Ina mustalah wa kisheria ambayo huwezi kuenda kwa istilahi nyengine ila Kwa qarinah, na huu mustalah wa kisheria hufanya maana ya khalifah kua yeye ndie mtawala ambaye anasimamia uongozi jumla juu ya waislamu wote kwa bay’ah ya kisheria kutoka wa waislamu ili awahukumu kwa Uislamu na kuubeba kwa ulimwengu kwa njia ya daawah na Jihad.

Na sio sahihi kile ambacho wanakidai baadhi kua kifo cha khalifah maana yake ni kufa mtawala miongoni mwa watawala wa leo ambao hawahukumu kwa uislamu na hawana bay’ah ya kisheria wala madaraka jumla juu ya waislamu.

Kumsubiri Mahdi kunachelewesha kudhihiri kwa khilafah na kunawapatia makafiri na madhalim maelfu ya nafasi ya kuweza kuushambulia uislamu na watu wake, ndio maana makafiri wanafiq na madhalim wanaunga mkono fikra hii kua khilafah haitosimama ila katika zama za Al mahdi, Na huu ni ufahamu wa upotoshaji na uleweshaji ambao umeweza kuwalemaza wengi katika waislamu mashia na masunni!!

Mashia Wanasubiri Mahdi Atoke pangoni na baadhi ya Masunni wanasubiri Mahdi atokee baina ya Nguzo na maqam!!!,

Anayekaa bila kuifanyia kazi hii faradhi huyu atakua anawahakikishia makafiri-kwa kujua ama kutojua- utumishi ambao siku nyingi wameuendea mbio kuujenga kwa waislamu, anasaidia kusihi kauli yao kua Usekula (Ilmaniyah) ndio Suluhisho, Bali anakwenda sambamba na maneno yao kua khilafah ni dola ya kidini na cheo chake ni cha kiuungu!!

Zimekuja Hadith nabawiyah zinazomaanisha kwamba khilafah itakua kwa manhaj ya utume na itasimama biidnillah hadith hizi zinawajibisha kusadiki. Na miongoni mwa hadith hizo:

  1. Kutoka kwa thawban radhi Za Allah zimwendee asema: asema Mtume s.a.w: “Hakika Allah alinikunjia Ardhi, nikaona mashariki yake na magharibi yake, na hakika umma wangu utafika utawala wake sehemu niliyokunjiwa..”

Amepokea Muslim na Ahmad na Abu daud na tirmidhiy na ibni maajah.

Kauli ya hadith: (Hakika umma wangu utawala wake utafika sehemu niliyokunjiwa) haijatimia mpaka sasa, kwani waislamu hawamiliki mashariki ya ardhi wala magharibi, na hili litakua hapo Mbeleni, hadith inaashiria kusimama kwa dola ya waislamu ili ifungue ardhi mashariki yake na magharibi yake,

  1. Kutoka kwa ibnu Omar radhi za Allah zimwendee asema nimemsikia Mtume s.a.w akisema:

“Mtakapouziana kwa ribaa, na mkashika mikia ya ng’ombe (Ukulima), na mkaridhia Na ukulima, mkawacha jihad, Allah atawasalitishia Udhalili ambao hatouondoa mpaka mutakaporudi kwa dini yenu”

 Amepokea Abu Daud.

Kauli yake (Mpaka mtakaporudi katika dini yenu) maana yake ni mpaka mtakaporudi kuifanyia kazi dini na kuitawalisha katika nyanja zote za maisha yenu, hii ni bishara kutoka kwa Mtume s.a.w kua waislamu watarudi kwa dini yao baada ya kuwacha kuhukumu nayo.

  1. kutoka kwa abi qabil asema: “Tulikua kwa Abdillah bin Amru ibnil Aasw, akaulizwa: Kati ya miji Miwili Ni upi utafunguliwa mwanzo: Qustantinia ama Roma? Abdullah akaitisha Sanduku lenye silaha, akasema: Akatoa Kitabu ndani ya lile sanduku, akasema: akasema abdullah: (Tulipokua Pambizoni mwa Mtume S.a.w tunaandika, Mtume s.a.w akaulizwa: ni mji gani utafunguliwa mwanzo kati ya miji miwili: Qustantinia na Roma? Akasema Mtume s.a.w : Mji wa Hirkali utafunguliwa mwanzo akimaanisha Qustantinia)”

Amepokea Ahmad.

Mtume s.a.w alipoulizwa kuhusu ufunguzi wa miji miwili Qustantinia na Roma- Ambayo ni mji mkuu wa Italy- hakukataa ufunguzi wa Roma Bali alisema kua qustantinia utafunguliwa mwanzo, na hii yamaanisha kuwa  Roma utafungukiwa baadae, na kwakua Roma haijafunguliwa na waislamu mpaka Leo, hii hadith ni bishara kua waislamu wataufungua mji mkuu wa italy, na haileti picha kua waislamu wataifungua Pasi na kurudi kwa khilafah ambayo itarudisha jihad katika njia ya Allah na kufungua miji.

4- kutoka Kwa Nuuman bin Bashir kutoka kwa Hudhaifa radhi za Allah zimwendee asema: amesema Mtume wa Allah s.a.w:

“Utakua utume kwenu kwa muda atakao Allah, kisha Allah atauondoa anapotaka kuondoa, kisha itakuja khilafah kwa Njia ya utume, itakua kwa muda atakao Allah kisha Allah ataiondoa anapotaka kuindoa, kisha utakuja ufalme wa kukandamiza, utakua kwa muda Atakao Allah, kisha Allah atauondoa anapotaka kuondoa, kisha utakuja utawala wa kibepari, utakua kwa muda atakao Allah kisha Allah atauondoa anapotaka kuondoa, kisha itakuja khilafah kwa njia ya utume kisha akanyamaza”

Hii hadith inabainisha kua khilafah Itasimama baada ya utawala wa kibepari, na kwamba itakua kwa njia ya utume, yaani imesifiwa kwa Sifa ileile ambayo imesifiwa khilafah ya makhalifah waongofu, na inshaAllah itakua khilafah ya Uongofu kwa manhaj ya utume.

Khilafah ni Faradhi Kisheria na ilikua ni waqiah na imejaza pembe za tarekh, na Mmagharibi anaogopa Isirudi Anafanya bidii ichelewe, na twaona ni namna gani ambayo zinatabiri Idara za uchambuzi za kimagharibi kua khilafah iko karibu na umma wanaiendea, ilihali waislamu wameghafilika na wamevunjika moyo… Jamani Allah Allah.. tusiwache kufanya kazi ili tusije tukaangamia huku tukiona!!

#UislamuNiHadharaMbadala

Imetafsriwa na Ustadh Mahdi
https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=227125144867409&id=100027097741781

Maoni hayajaruhusiwa.