Jee Tuna ‘Uhuru’ Kweli?
بسم الله الرحمن الرحيم
Leo ni kilele cha kumbukumbu za ‘uhuru wa bendera’ ambapo Tanganyika iliupata uhuru huo rasmi tarehe 9 Disemba 1961 kutoka kwa Uingereza, na kusheherekewa kila mwaka kwa shamra shamra na sherehe kubwa kitaifa.
Katika hali kama hiyo ipo haja kubwa ya kuzungumzia kwa kina dhana (concept) hii ya uhuru kwa upana, uhalisia wake, chimbuko lake, na namna madola yenye mifumo walivyoitumia kwa maslahi yao ili kujijengea himaya zao kwa gharama ya maisha yetu.
Uhuru ni ile hali yakujiamulia na kujipangia mambo yako mwenyewe, kujitawala katika vipengele vyote vya maisha, yaani ni ile hali ya kutokuwa chini ya umiliki wa yeyote katika sekta zote ama zikiwa za kisiasa, kiuchumi au kitamaduni.
Asili ya mwanadamu tangu kuumbwa kwake ana hisia ya kimaumbile ya kupenda maisha yake yawe mazuri. Jambo hilo humsukuma kutaka kutawaliwa kiuadilifu ili mambo yake yaendeshwe kwa mpangilio na kuepuka migongano isiyo ya lazima na wanadamu wenzake. Kutokana na ukweli huo, mwanadamu hutaka atawaliwe na anaemuamini, mwenye huruma juu yake na atakaelinda maslahi yake. Katika hali kama hiyo ni wazi kabisa dhana ya uhuru ilipopigiwa debe kwa udhati iligusa sehemu nyeti ya maumbile ya mwanadamu. Kwa sababu walio wengi walihisi ililenga kuondokana na tawala dhalimu za ukandamizaji za kimabavu na kikoloni na kuleta tawala zitakazoendeshwa na kuyatawala na mambo kwa huruma, maridhiano na uadilifu baina ya watawala na watawaliwa, huku raia watafaidika na rasilimali za nchi zao katika kujenga maisha yao. Kwa hiyo kauli mbiu ya uhuru iliweza kwa haraka kuenea kama moto katika nyasi kavu na kuwateka wengi miongomi mwa watu wa nchi katika bara la Afrika, Asia na Marekani ya kusini kutokana na nchi hizi kwa muda mrefu kukaliwa kimabavu na kukandamizwa na ukoloni mkongwe.
Watu wengi waliona dhana hii kwa kuitupia macho na kulinganisha na dola ya Marekani kama kigezo chao, namna huko awali dola hiyo ilivyotawaliwa na Uingereza na kuupata uhuru wake katika mwaka 1776, baada ya mapambano makali ya ‘piga uwa’ na hatimae kuibuka kuwa dola kubwa yenye nguvu kutokana na kujipatia uhuru wake.
Hata hivyo, ukweli wa mambo kwa dhana hii ilipoletwa katika nchi zetu, na ilikusudiwa kutumika kwa maana tofauti na malengo mengine kabisa, tofauti na tulivyodhani. Na hapana shaka yoyote ililengwa kwa maslahi ya madola yenye mifumo.
Baada ya kuibuka kimataifa kwa dola ya Marekani na umoja wa kisovieti hususani mara baada ya vita vya pili vya dunia, na katika harakati zao za kukabiliana kuiondoa himaya ya ‘ukoloni mkongwe’ uliokuwa ukishikiliwa na nchi za ulaya hususani Uingereza na Ufaransa, ili zichukue nafasi hiyo badala yao, walipaza sauti kali ya kauli mbiu hii ya ‘uhuru’ na katika kiwango cha hali ya juu kimataifa kiasi cha kuushawishi mtizamo wa dunia katika kuonesha uovu na ushenzi wa ‘ukoloni mkongwe’ na upande wa pili kuonesha uzuri wa ‘uhuru na kujiamulia mambo’ huku madola hayo yakiwa na malengo ya moja kwa moja kuchukua nafasi katika nchi zitakazokuwa huru kwa lengo la kuimarisha madola yao na kujitanua katika utawala wao ulimwenguni kote hususani katika nchi za Afrika na Asia ambazo zimesheheni kila aina ya maliasili.
Ikumbukwe kwamba madola haya mawili ya Marekani na umoja wa kisovieti yalikuwa mageni katika uwanja wa kimataifa, kwa sababu Marekani licha ya kwamba ilishiriki katika vita vya kwanza vya dunia lakini mara baada ya kumalizika iliendelea kujifunga na mambo ya bara lake tu (isolation). Bila ya kuonyesha shauku yoyote katika uwanja wa siasa za kimataifa mpaka mara baada ya vita vya pili vya dunia. Amma dola ya umoja wa kisovieti iliyoundwa rasmi katika mwaka 1917 kufuatia mapinduzi ya kisoshalisti ndani ya Urusi nayo haikuwa na uzoefu wakutosha katika siasa za kimataifa ukilinganish na madola mazoefu ya kikoloni ya Ulaya. Lakini madola mawili haya yalihisi huu ulikuwa muda muwafaka kwa madola yao nayo kuibuka na kusimama kidete kuwa viranja watakaoiongoza dunia na kufaidika katika kueneza mifumo yao na kunyonya rasilimali zake kwa maslahi ya nchi zao.
Mapema zaidi fikra hii ya ‘Uhuru na kujiamulia mambo’ ilitumiwa na madola yote ya magharibi hususan Uingereza na Ufaransa kwa lengo la kusambaratisha dola ya khilafah Uthmania (Ottoman Caliphate) kwa kuigawanya vipande vipande na kuipoteza nguvu yake. Jambo hili walilifanya kwa kupandikiza fikra hizi kwa watu maalumu wakiwemo ‘wasomi’ na wanaharakati mbalimbali hususan katika waturuki na waarabu wakilenga kutayarisha kundi la ‘wapigania uhuru’ watakao zivua nchi zao na makao makuu ya dola ya kiislamu. Kadhalika madola ya magharibi katika mbinu yao hii waliwatumia wataalamu wa muelekeo wa mashariki (orientalists) na kuasisi vyuo na vituo mbali mbali na huku balozi zao nao zikifanya kazi usiku na mchana katika nchi kama Uturuki, Balkans, Lebanon, Syria, Bara za Arabu n.k kuhakikisha mafanikio katika lengo hili. Wakiwapatia vikundi mbali mbali katika mbinu ya kifikra, mikakati na zana ili wapiganie uhuru wao na kujitenga na Dola ya kiislamu ya khilafah ya Uthmani (Ottoman Caliphate).
Kwa hakika Marekani na Umoja wa kisovieti walipaza mwito wa uhuru mapema, lakini mwito huu ulianza kupata nguvu kiasi fulani baada ya vita vya pili, kumakinika zaidi mwishoni mwa miaka ya khamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini hususan mara baada ya mwaka 1961 kufuatia mawafikiano ya Vienna baina ya Raisi Kennedy wa Marekani na Khrushchev, kiongozi wa Umoja wa kisovieti, wakikusudia kuidhibiti dunia na kugawana uongozi wake baina yao na kuitenga dola ya Uingereza na Ufaransa. Kuanzia hapo walitumia dhana hii ya ‘Uhuru’ kwa msukumo wa aina yake wakitoa kila msaada kila unapohitajika kwa baadhi ya wapigania uhuru, ukiwa kama mpango na mkakati kabambe wa kupunguza kama si kumaliza kabisa nguvu ya Uingereza na Ufaransa kilimwengu kwa kuung’oa ukoloni wao ili badala yao, wao wachukue nafasi yao baada ya madola haya kumeguka meguka milki na athari zao kimataifa.
Kwa kuwa dola ya Uingereza ilijijengea uzoefu muda mrefu na ilikuwa hodari zaidi kisiasa katika uwanja wa kimataifa kuliko Marekani na Umoja wa Kisovieti, hivyo baada ya kushtukia ‘janja hii’ nakuona kwamba wimbi hili la kutoa uhuru halizuiliki tena kwa kuwa limeweza kuiteka dunia yote na haiwezekani tena kuwatawala watu kwa namna ile ile ya ‘ukoloni mkongwe’ kwa miaka yote, iliamua kubuni mbinu kabambe ili kujihami na kuendeleza himaya yake kwa mlango wa nyuma. Wakaandaa kundi la ‘wapigania uhuru’ ndani ya Afrika na sehemu nyingine. Miongoni mwao ni maarufu zaidi ni Nyerere, Kenyatta, Lumumba, Kaunda, Ali Jinnah, Gandhi, Sukarno nk.
Lengo la kuunda watu hao ilikuwa ni kukabiliana na wimbi la kuondoshwa athari yake na ili dola ya Uingereza iweze kulinda na kuhifadhi himaya yake mara baada ya kutoa ‘uhuru wa bendera’. Ilikuwa ni rahisi kuwaandaa ‘wapigania uhuru’ hawa kwa sababu nchi zao zilikuwa katika milki yake kwa mda mrefu, kwa hivyo Uingereza ilikuwa na uelewa wa kutosha wa makoloni yake na zaidi ‘wapigania uhuru’ hao wengi wao kama si wote walililewa chini ya sera ya uingereza. Tofauti na Marekani na umoja wa kisovieti, dola ambazo zilikuwa bado hazijamakinika na kuota mizizi katika makoloni mbalimbali kama ilivyo dola ya Uingereza.
Mmoja kati ya aliyekuwa wasimamizi wa kale wa sera ya elimu ya Uingereza katika makoloni yao Lord Maccaulay alipoelezea harakati za uhuru ndani Misri alitamka wazi kwamba:
“Uingereza haitakuwa tayari kuikabidhi nchi yoyote uhuru mpaka pale itakapoona wapo raia ambao wamesoma katika mfumo wetu, kwa sababu yeyote aliyepitia katika mfumo huu ni tofauti na aliyesoma katika mfumo wa asili” (yaani Uislamu)
Kwa hivyo utaona kwamba katika miaka ya khamsiini na sitini ilikuwa ‘panda shuka’ kuelelekea jumba la Lancaster House, London kwa lengo ati la ‘kudai uhuru’ ambao unatolewa na dola ya Uingereza na ni Uingereza yenyewe ndio iliunda hivyo vyama vya kudai uhuru huo pamoja na katiba za ‘dola huru’ zinazo zifunga dola hizo ‘uhuru na mfumo wa Uingereza mara baada ya ‘uhuru wa bendera’. Kwa hakika ilikuwa ni kiroja cha mwaka, kwa upande mmoja dola ya Uingereza ikiwa mshitakiwa na upande wa pili iliku hakimu.
Tukumbuke kwamba sekeseke la kutaka kupinduliwa serikali ya Mwalimu Nyerere katika mwaka 1963, lilikuwa ni jeshi la Uingereza ndilo lililokuja kuokoa jahazi na kutuliza hali. Kwanini? Kwa sababu bado lilikuwa koloni lao!
Kadhalika utaona hata hayo yanayoitwa mapinduzi ya Zanzibar, ilikuwa ni usanii wa Uingereza wa kumuondoa kibaraka mmoja na kumuweka kibaraka mwingine, na yule wa awali wakaamua kumuhifadhi ndani ya Uingereza.
Kwa hiyo, harakati za kudai uhuru hazikuwa wazo la ‘wapigania uhuru’ tunaowajua na kuwakumbuka, bali ilikuwa ni mbinu ya kubadilisha tu sura ya ‘ukoloni mkongwe’ na kuanza kwa awamu mpya ya ‘ukoloni mpya’ au ‘ukoloni mamboleo’. Ukoloni ambao ni wa hatari zaidi na wenye madhara zaidi kwa sababu waliowengi hata hawaelewi, kwa sababu tu tuna bendera, wimbo wa taifa na sarafu yetu yenye picha ya mlima wa Kilimanjaro na shada la karafuu!
Uhuru wa kweli hujengwa kwa nchi kwanza kujizatiti kwa kubeba mfumo wake wenyewe kitu ambacho nchi changa hazibebi mfumo zaidi ya kuiga tu, kujifungua na utegemezi katika kila Nyanja na kusimama kwa miguu yake wenyewe. Jambo ambalo huwezekana tu endapo nchi itajengwa juu msingi thabiti wa kitikadi. Na hili ni jambo linalopigwa vita na Marekani kwa kuhofia kupokonywa uongozi wake dhalimu ulimwenguni!
Na Hamza S. Sheshe.
Maoni hayajaruhusiwa.