Hukmu ya Mali Haramu Baada ya Toba

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Mwanachuoni mstahiki Atta ibn Khalil Abu Rashtah, Allah akuhifadhi, Assalamu Alaykmu Warahmatullah Wabarakatuh, ama baada ya hayo:

Nini hukmu ya mali ya haramu baada ya toba, kwamfano, mali iliyopatikana kwa njia ya riba au kwa njia ya wizi au kwa njia ya uimbaji/muziki mporomoko au yasiyokuwa hayo?

Na je kila moja katika hayo kuna hukmu maalum au hukmu ni moja tu?

Ikiwa mali ya haramu hata muhusika akitubia, huenda kuna mtu anataka kutubu lakini anachelea kupotea mali yake…Je huyu hukmu yake ni maalumu na kuwa na matumaini katika toba yake kama walivyosema baadhi ya mashekhe?

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh

Anasema Allah (SWT):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَصُوحًا

“Enyi mulioamini tubuni kwa Allah toba ya moja kwa moja”.

Na anasema (SWT):

إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَاعْتَصَمُوا بِاللَّهِ وَأَخْلَصُوا دِينَهُمْ لِلَّهِ فَأُولَئِكَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ وَسَوْفَ يُؤْتِ اللَّهُ الْمُؤْمِنِينَ أَجْرًا عَظِيمًا

“Isipokuwa wale waliotubu na wakatengeneza na wakashikamana na Allah na wakatakasa dini yao kwa ajili ya Allah, basi hao wako pamoja na waumini na punde Allah atawapa waumini ujira mkubwa”.

Na ametoa Tirmidh kutoka kwa Anas kwamba hakika Mtume (SAW) amesema:

«كُلُّ ابْنِ آدَمَ خَطَّاءٌ وَخَيْرُ الخَطَّائِينَ التَّوَّابُونَ»

“Kila mwanadamu ni mkosaji na wabora wa wakosaji ni wenye kutubu”.

Na ili toba isihi, na Allah (SWT) amsamehe mwenye kutubu kutokana na madhambi, basi ni wajibu kwa mwenye kutubu kung’oka katika maasi, ajute kwa Allah kwa kutenda madhambi kipindi cha nyuma, aazimie azma ya kukata kwamba hatorejea mfano wake katu. Na ikiwa yale maasi yameambatana na haki ya mwanadamu, basi ni sharti kurejesha kile alichodhulumu kwa wenyewe au patokee kujivua nacho (yaani wasamehe). Ikiwa ana mali ameichukua kwa wizi au kwa kupora itakua ni wajibu airejeshe ile mali kwa wenyewe, na ajitenge na chumo ovu kwa njia ya kisharia, kwani hakika kuchuma mali kwa njia ya haramu mwisho wake ni mbaya. Ametoa Ahmad kutoka kwa Abdillah bin Mas’ud amesema: kasema mjumbe wa Allah (SAW):

«…وَلَا يَكْسِبُ عَبْدٌ مَالًا مِنْ حَرَامٍ… إِلَّا كَانَ زَادَهُ إِلَى النَّارِ»

“…wala hachumi mja mali kutoka na haramu …isipokuwa itakua ndio zawadi yake kwenye moto”. Na ametoa Altirmidh kutoka kwa Ka’ab ibn Ajra kwamba mjumbe wa Allah (SAW) amemwambia:

«يَا كَعْبَ بْنَ عُجْرَةَ، إِنَّهُ لَا يَرْبُو لَحْمٌ نَبَتَ مِنْ سُحْتٍ إِلَّا كَانَتِ النَّارُ أَوْلَى بِهِ».

“Ewe Ka’ab ibn Ajra hakika haikui nyama iliyomea kutokana na haramu isipokuwa moto utakuwa ndio bora kwake”

Kwahiyo, vipi anataka mtu huyu unaemuulizia kutubu na aibakishe mali ya haramu katika mikono yake?! Hii itakuwa sio toba bali ni mtu huyu atakuwa anaendelea na uovu. Kwahiyo, mnasihi atubu na aepukane na chumo la haramu kwa njia ya kisharia, na arejeshe mali aliyoiba au kupora kwa mwenyewe, na aombe msamaha wao, na amuombe msamaha Allah mwanzo na mwisho. Na Allah (SWT) ndie Mwenye kuruzuku Mwenye nguvu madhubuti, atampa badili yake akipenda yeye (SWT) mali nzuri yenye baraka Allah amtie nguvu kwayo duniani na akhera. Na Allah (SWT) anapenda toba ya mja wake akiwa mkweli na akafanya ikhlasi na humlipa malipo yenye kutosheleza…

Namuomba Allah (SWT) amuongoze mtu huyo kwenye jambo lake lililonyooka zaidi na atubu toba ya moja kwa moja. Na Allah (SWT) ni mwingi wa kusamehe.

Ndugu yenu Atta ibn Khalil Abu Rashtah

Maoni hayajaruhusiwa.