Hukmu ya Kuchukua Mshahara kutoka kwa Mwajiri Anaye Amiliana na Riba

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Bismillah Ar-Rahman Ar-Raheem

Mmoja katika ndugu aliniaibisha kwa swali ambalo nadhani yuko sahihi kwalo, licha ya jaribio langu la kuielezea hali tunayoishi ndani yake, lakini bado angali hajakinaika.

Swali linahusu mshahara unao chukuliwa kwa kazi iliyo wasilishwa katika afisi ya umma katika mfumo huu wa kirasilimali, ambao takriban wote au baadhi yake ni riba, tukijua kwamba nchi mfadhili hulipa wadhifa wa umma kwa pesa hizi au kwa baadhi ya pesa hizi kutoka kwa mikopo ya riba iliyo chukuliwa kutoka nchi za kigeni au kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa.

Je, sisi, waajiriwa, kwa badali ya kazi yetu katika utumishi wa umma, tuchukue pesa hizi za riba au la? Na ikiwa jibu ni ndio, basi ni ipi njia ya kuziondoa na kuishi pasi na kazi ambayo tunatumia maisha yetu kusoma na kufanya kazi kwa ajili yake?

Natanguliza shukrani kwa kufahamu kwako na Mwenyezi Mungu akulipe kheri nyingi.

Ndugu yenu Ammar kutoka Tunisia

Jibu:

Wa Alaykom Assalam Wa Rahmatullah Wa Brakatuhu,

Kuhusu mshahara ambao mwajiriwa anapokea katika afisi ya umma kwa badali ya kazi yake, hukmu yake inahusiana na kazi anayoifanya:

– Ikiwa anafanya kazi iliyo haramishwa kama mtu anaye fanya kazi katika ujasusi kuwachunguza Waislamu au anayefanya kazi katika kuwatesa watu na wabebaji ulinganizi nk…, basi mshahara huo utakuwa ni haramu kwa sababu aliuchuma kutokana na kazi ya haramu…

– Na ikiwa kazi anayo fanya ni ya mubah, kama kufanya kazi kama mwalimu, mhandisi, au daktari katika hospitali ya serikali, au kazi nyengine yoyote ya mubah, mshahara wake unaruhusiwa kwake, na hadhuriki endapo pesa hizo za upande unaomlipa mshahara wake zitachanganyika na riba au miamala mengine iliyo haramishwa au miamala iliyo ruhusiwa, uchukuaji mshahara wake kutoka katika mchanganyiko huu wa yaliyo ruhusiwa na yaliyo haramishwa inaruhusiwa kwake, isipokuwa ikiwa mshahara wake utachukuliwa kutoka katika pesa zilizo ibwa, zilizo porwa, au kutoka katika pesa za haramu, kama vile pombe na nguruwe, hivyo endapo mshahara wake ni katika pesa zilizo ibwa au kutoka katika pesa za haramu kwa dhati yake, hairuhusiwi… kama ilivyo fafanuliwa juu:

Pesa zilizo haramishwa ziko aina tofauti tofauti:

– Haramu kwa dhati yake… Ni haramu kuzitoa kama zawadi, hivyo ni haramu kwa mmiliki wa pombe na kwa yule anaye pewa kwazo kama zawadi. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:  

«حُرِّمَتِ الْخَمْرُ بِعَيْنِهَا»

“Pombe (Khamr) imeharamishwa kwa dhati yake.” (Imesimuliwa na an-Nasa’i)

– Haramu kwa kuwa ni katika haki (Haq) ya mwanadamu mwengine iliyo ibwa au kuchukuliwa kwa nguvu… Hii ni haramu kwa mwizi na mporaji, ambapo hairuhusiwi kuitoa kama zawadi kwa kuwa ni haramu kwa yule aliyezichukua pesa hizi na kwa mwenye kupokea zawadi hiyo. Pesa hizi ni haki ya mmiliki wake, na popote alipo, pesa hizi ni lazima zirudishiwe kwa mmiliki halali. Baadhi ya dalili ya hili ni:

Ahmad amesimulia kutoka kwa Samurah kwamba amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«إِذَا سُرِقَ مِنَ الرَّجُلِ مَتَاعٌ، أَوْ ضَاعَ لَهُ مَتَاعٌ، فَوَجَدَهُ بِيَدِ رَجُلٍ بِعَيْنِهِ، فَهُوَ أَحَقُّ بِهِ، وَيَرْجِعُ الْمُشْتَرِي عَلَى الْبَائِعِ بِالثَّمَنِ» 

“Mtu anapoibiwa mali, au kupoteza mali, kisha akaipata mikononi mwa mtu mwengine aliyeinunua, basi ana haki kwayo, na mnunuzi airegeshe kwa muuzaji kwa thamani aliyo nunulia.”

Hii ni nasi inayo onyesha kuwa pesa zilizo ibwa ni lazima ziregeshwe kwa mmiliki wake.

Pesa zilizo chukuliwa kwa nguvu pia zimedhaminiwa yule aliye pokonywa kwa nguvu, hivyo mporaji ni lazima aregeshe chochote alicho kichukua kwa nguvu kwa mmiliki wake.

Imesimuliwa kutoka kwa Samurah kwamba Mtume (saw) amesema:

 «عَلَى اليَدِ مَا أَخَذَتْ حَتَّى تُؤَدِّيَ»

“Juu ya mkono ulio chukua ni dhima mpaka ulipe” [Imesimuliwa na at-Tirmidhi na akasema Hadith hii ni Hasan]

– Haramu kwa sababu ya miamala ya batili kama vile pesa za riba na kamari… Hizi zimeharamishwa kwa yule aliyezipokea pekee, lakini uharamu huu haupanuki hadi yule aliyezipokea pesa hizi kupitia njia ya mubah kutoka kwa yule aliye kula riba au kucheza kamari. Kwa mfano, kumuuzia bidhaa yule anayejihusisha na riba na kupokea thamani yake, mke anayepokea matumizi yake kutoka kwa mumewe anayejihusisha na riba, mtu anayejihusisha na riba kuwaletea zawadi jamaa zake, au miamala mengine yoyote ya mubah. Dhambi la pesa hizi za haramu liko kwa yule aliyejihusisha na riba pekee na sio mtu anaye muuzia bidhaa na kuchukua thamani yake kwake, wala mke anaye pokea matumizi yake, au mtu anaye pokea zawadi kutoka kwake, na hilo ni kwa sababu katika hali hii uharamu hauhusishi dhima ya watu wawili. Baadhi ya dalili juu ya hilo ni:

1. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَلَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ إِلَّا عَلَيْهَا وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى]

“Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe.” [Al-An’aam, 6:164]

2. Mtume (saw) alikuwa akiamiliana na Mayahudi mjini Madina, huku akijua kwamba nyingi ya pesa zao zimetokana na riba. Mwenyezi Mungu (saw) asema:

 [فَبِظُلْمٍ مِنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ لَهُمْ وَبِصَدِّهِمْ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ كَثِيرًا* وَأَخْذِهِمُ الرِّبَا وَقَدْ نُهُوا عَنْهُ وَأَكْلِهِمْ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ]

“Basi kwa dhulma yao Mayahudi tuliwaharimishia vitu vizuri walivyo halalishiwa. Na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na Njia ya Mwenyezi Mungu* Na kuchukua kwao riba, nao wamekatazwa, na kula kwao mali ya watu kwa dhulma.” Mtume (saw) alikuwa akipokea zawadi kutoka kwao.

Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba mwanamke mmoja kutoka katika Mayahudi alimpa zawadi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) nyama ya kondoo yenye sumu, hivyo akatumana kwake aje na akasema:

ورد عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ: أَنَّ امْرَأَةً مِنَ الْيَهُودِ أَهْدَتْ لِرَسُولِ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ شَاةً مَسْمُومَةً، فَأَرْسَلَ إِلَيْهَا، فَقَالَ: «مَا حَمَلَكِ عَلَى مَا صَنَعْتِ؟» قَالَتْ: أَحْبَبْتُ – أَوْ أرَدْتُ – إِنْ كُنْتَ نَبِيًّا فَإِنَّ اللهَ سَيُطْلِعُكَ عَلَيْهِ، وَإِنْ لَمْ تَكُنْ نَبِيًّا أُرِيحُ النَّاسَ مِنْكَ.

“Ni kitu gani kilicho kufanya ufanye uliyo yafanya?” Akasema: “Nilipenda – au nilitaka – ikiwa wewe ni mtume, basi Mwenyezi Mungu angekuelezea juu yake, na ikiwa wewe si mtume, niwapumzishe watu kutokana na wewe.”

3. Baadhi ya Sahaba na Tabi’een walifanya kuwa mubah kupokea zawadi kutoka kwa mtu anaye chukua riba:

A) Mtu mmoja alikuja kwa Ibn Masoud na akasema: Nina jirani mlaji wa riba, na bado hunikaribisha, hivyo Ibn Masoud akamwambia: “kwako wewe ni amali njema, na dhambi ni kwake yeye” [Imesimuliwa na Abdul-Razzaq as-San’ani katika Musannaf yake]

B) Al-Hassan aliulizwa: Je, chakula cha wabadilishanaji pesa chaweza kuliwa? Akasema: “Mwenyezi Munguسبحانه وتعالى  amewaelezeni kuhusu Mayahudi na Manaswara, walikuwa wakila riba, na Akawahalalishieni chakula chao” [Imesimuliwa na Abdul-Razzaq as-San’ani katika Musannaf yake kutoka kwa Ma’mar]

C) Imesimuliwa na Mansour kwamba amesema: nilimwambia Ibrahim: nilikwenda sehemu ya mfanyikazi mmoja, hivyo akanikaribisha na kunipa pesa. Ibrahim akasema: “Pokea”, hivyo Mansour akasema: mfanyikazi huyo anachukua riba. Ibrahim akasema: “Pokea maadamu hukumwamrisha wala kumsaidia katika riba yake” [Imesimuliwa na Abdul-Razzaq as-San’ani katika Musannaf yake kutoka kwa Ma’mar]

4. lakini, ni bora kutoamiliana na wamiliki wa pesa za haramu zinazo tokana na riba, hivyo musiwauzie wala kupokea zawadi kutoka kwao kwa kushajiishwa na uchaMungu; ili muuzaji asipokee faida kutokana na biashara yake iliyo chafuliwa kwa riba, na asipokee zawadi zao ili zisiwe ni kutokana na pesa za riba. Katika njia hii, Waislamu watajiweka mbali na kila kitu kilicho kichafu, na Maswahaba wa Mtume (saw) walikuwa wakijiweka mbali kutokana na vitu vingi vya mubah kwa hofu ya kuikaribia haramu.

Imesimuliwa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwamba amesema:

«لَا يَبْلُغُ العَبْدُ أَنْ يَكُونَ مِنَ المُتَّقِينَ حَتَّى يَدَعَ مَا لَا بَأْسَ بِهِ حَذَرًا لِمَا بِهِ البَأْسُ» 

“Mja hatafikia kuwa miongoni mwa wachaMungu mpaka awachane na vitu visivyo na matatizo (lakini vyenye shaka) kwa kutahadhari vile vyenye matatizo.” [Imesimuliwa na at-Tirmidhi, na akasema Hadith hii ni Hasan]

Kwa kutamatisha, inaruhusiwa kumuuzia mtu ambaye utajiri wake ni mchanganyiko wa riba na halali, na inaruhusiwa kupokea zawadi yake, na inaruhusiwa kuchukua mshahara wako kutoka kwake, lakini ni bora kwako kwamba usimuuzie au kukubali zawadi yake, na usifanye kazi kwake na kuchukua mshahara wako kwake. Kwa hayo, mwajiriwa anaye fanya kazi ya mubah katika afisi ya umma, na kuchukua mshahara wake kutoka kwa mwajiri ambaye pesa zake ni mchanganyiko wa haramu na halali, hivyo mshahara wake ni halali kwake na anaweza kuuchukua pasi na aibu… kwani dhambi la riba haliko kwa mwajiriwa bali liko juu ya mamlaka anayoifanyia kazi.

Nataraji kwamba jibu hili litatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.

Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

9 Dhul Qi’dah 1441 H
Sawia na 30/06/2020 M

Link ya jibu katika Ukurusa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) wa Facebook:
https://web.facebook.com/HT.AtaabuAlrashtah/posts/2677639062482101?__tn__=K-R

Maoni hayajaruhusiwa.