Hata Ramadhani bado Wanawake mna Malipo Makubwa.

2

Suala la malipo kwa mwanadamu ni suala ambalo halina shaka kwa mwenye imani thabiti mbele ya Mola wake. Lakini kuna suala la kujiuliza hasa kwa akinamama na madada zetu kwa kuwa wao muda mwingi huwa na majukumu ya ndani ya nyumba zao tofauti na waume zao. Aidha, inadhihirika kuwa wanaume hupata muda mwingi zaidi wa kufanya ibada ziada jambo ambalo laweza likawapandisha daraja mbele ya Allah Subhanahu Wataala. Ilhali wanawake wakaona, wao ni wenye nafasi ndogo tofauti na daraja kama za waume zao au makaka zao.

Asma bint Yazid Answari (r.a) anatuelezea juu ya suala hilo. Siku moja alikwenda kwa Rasulullah Sallallahu Alaihi Wasallam na akamwabia:

“Ewe, Rasullullah! Wewe ni kipenzi kwangu mimi kuliko wazazi wangu. Wanawake wa kiislamu wamenituma kama mwakilishi wao ili nije nizungumze nawe kwa niaba yao. Bila shaka wewe ni Rasulullah kwa wanawake na wanaume pia. Sisi hupitisha wakati wetu zaidi baina ya kuta nne za majumba yetu. Tumefungika katika wajibu wetu wa kutosheleza shahawa za waume zetu, kuwazalia watoto na kuwatunzia majumba yao. Licha ya haya yote, wanaume wanatushinda katika kupata thawabu kwa mambo ambayo sisi hatuwezi kuyafanya. Wao huenda msikitini wakaswali swala zao kwa jamaa kila siku na pia swala ya Ijumaa kila wiki, wao huwazuru wagonjwa huwenda mazishini, wanakwenda hajj baada ya hajj na juu ya hayo yote wao hupigana katika njia ya Allah (s.w).Wanapokwenda Hajj au katika Jihad, sisi huwatunzia mali zao tukawalea watoto wao na tukawashonea nguo zao. Je nasi hatupati sehemu katika thawabu zao?”

Mtume SAAW aliwaelekea Maswahaba waliokuwa pamoja naye, akasema:

Je, mumewahi kumsikia mwanamke akiuliza swali bora kuliko hili ?”

Maswahaba R. A walimjibu:
“Ewe, Rasulullahi! Hatukufikiria kamwe kuwa anaweza kuuliza swali kama hili.”
Rasulullah Salallahu Alaihi Wasallam akwambia Asma :
“Sikiza kwa makini halafu nenda ukawaambie hao wanawake waliokutuma ya kuwa mwanamke akitafuta radhi za mumewe, na akazitekeleza kazi za nyumbani kwake mpaka mumewe akaridhika, anapata malipo sawa sawa na mume kwa ibada zote anazozifanya huyo mume.”

Nasaha hizi za Mtume SAAW ziondoshe hisia za unyonge wa akinamama juu ya uhafifu wa amali zao hususan ndani ya mwezi huu wa Ramadhani. Aidha, nasaha hizi zisiwe kisingizio cha wanaume kuwatwisha makazi mengi wake zao kiasi cha kuwakosesha fursa kujihusisha na ibada kwa kadiri inavyowezekana. Ni muhimu kuzipokea nasaha hizi kwa uzani na sio kuufanya mwezi huu ni wa kupikapika muda wote.

Tunamuomba Allah Subhanahu Wataala Atupe maghfira Yake, Atuokoe na moto na Atuingize katika pepo kwa Rehma zake , tuwe pamoja na wema waliotangulia na Mashahidi. – Amiin

#UislamuNiHadharaMbadala

Kutoka Gazeti la Khilafah- Ramadhani 1434 AH/ Julai 2013 Miladi

2 Comments
  1. sklep online says

    Wow, incredible blog layout! How lengthy have you been blogging
    for? you made running a blog look easy. The entire look of
    your site is wonderful, let alone the content material!
    You can see similar here sklep

  2. Delanie says

    Stunning story there. What occurred after? Take care!

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.