Funzo la Hijra na Mwaka Mpya Wa Kiislamu

Tumeingia mwaka mpya wa 1440 Hijria. Waislamu yatupaswa kwa dhati kulitizama suala hili kwa kina na kujifunza kivitendo kuhusu mwaka mpya, historia yake na mazingatio yake, kwa kulipa uzito na umuhimu unaostahili.

Kalenda ya Kiislamu ilikuwa ni makubaliano ya masahaba Allah awaridhie (ijmaa) katika Ukhalifa wa Umar bin Khatwab (ra.) kukubaliana kuihesabu kutoka tukio la Hijra. Licha ya kuwepo matukio mengi matukufu kama uzawa wa Mtume saaw kupewa Utume, safari ya Isra na Miraji nk, Masahaba walikubaliana kuasisi kalenda yao kupitia tukio la Hijra ya Mtume saaw kutoka Makka kwenda Madina na masahaba wake ndani ya mwaka wa 13 wa Utume.

Hii ni kwa sababu Hijra ni tukio adhimu lililoleta mwanzo mpya kwa Ummah wa Kiislamu. Linawakilisha kuhama Ummah wetu mtukufu kutoka jitihada ya kikundi cha watu mpaka kuwa jamii kamili yenye serikali yenye nguvu. Linawakilisha kutoka mahubiri mpaka utekekezaji wa kimatendo katika siasa, itikadi, uchumi, kijamii, kidiplomasia na kijeshi. Aidha, linawakilisha kuhama kwa Ummah kutoka Dar al Kufr mpaka Dar al Islam.

Katika kipindi chote cha ulinganizi wa kikundi katika Makka ulibakia kuwa ulinganizi wenye lengo la kuwezesha kutekelezeka kivitendo, ndiyo maana baada ya kupatikana nusra kutoka kwa Answar iliyopelekea kuasisi serikali ya mwanzo ya Kiislamu katika Madina, Uislamu ulianza kutekelezeka kwa ukamilifu wake, kwani kiuhalisia hakuna sheria na nidhamu inayoweza kutekelezeka bila ya uwepo wa serikali kusimamia utekelezaji huo.

Mara baaada ya kuasisiwa dola hiyo ilibakia mpaka mwaka 1924, ilipoangushwa na wakoloni na vibaraka wao. Wakati tukiingia ndani ya mwaka huu mpya wa Kiislamu tuzingatie uwajibu na umuhimu wa kuirejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah. Tunawajibika kuirejesha dola hiyo kama tulivyoamrishwa na sheria kwa kupitia njia ya Mtume saaw ya kifikra na kisiasa, ikilengwa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu, kisha kuenea nuru na uadilifu wake ulimwenguni kote kupitia ulinganizi (daawah) na jihadi.

Tunamuomba Allah SW Awape malipo makubwa walinganizi wa Uislamu, wake kwa wanaume, na pia Awafariji wale wanaodhulumiwa katika majela, vitisho, na mateso kwa sababu ya ulinganizi wa Kiislamu.

Aidha, tunawapa pole ndugu zetu wote ndani ya ardhi za Palestina, Syria, Burma, Somalia, Afrika ya Kati, Iraq, Libya, Yemen, Afghanistan nk. kutokana na madhila ya kukosekana utawala wa Khilafah, iliyosababisha uvamizi na mateso ya makafiri hususani Marekani na Washirika wake kupitia hila za watawala madhalimu wa nchi za Waislamu wasiojali chochote zaidi ya matumbo yao na viti vyao vya utawala.

Amiin

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

11 Muharram 1440 Hijri | 21-09- 2018 Miladi

Risala ya Wiki No. 16

Maoni hayajaruhusiwa.