Chuki Dhidi ya Wageni Afrika Ya Kusini na Penginepo: Sababu Pekee ni Ubepari:
Habari:
Vyombo vya habari vimeripoti qadhia ya Raisi wa Afrika ya Kusini kukabiliwa na idhilali ya hadhira iliyoambatana na nyimbo za kejeli na kuzomewa katika hafla ya kiserikali ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Raisi wa Zimbwabwe, bwana Robert Mugabe, mjini Harare. Hadhira ilichukua hatua hiyo kutokana na vitendo vya karibuni vya raia wa Afrika ya Kusini kuwavamia wageni.
Maoni:
Suala la chuki dhidi ya wageni sio jambo la Afrika ya Kusini pekee. Bali limekita kila mahala chini ya mfumo huu wa kibepari, lipo katika madola ya Magharibi pamoja na Marekani, nchi zinazoitwa vigezo vyema vya demokrasia.
Machafuko ya kikatili ya karibuni dhidi ya wageni nchini Afrika ya Kusini yameshutumiwa kila mahala ndani ya Bara la Afrika, yakasukuma pia hali ya ulipizaji kisasi nje ya Afrika ya Kusini. Nigeria ilimwita nyumbani balozi wake, kuanza zoezi la kuhamisha raia wake na kususia Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Kilimwengu kuhusu Afrika uliopangwa kufanyika mjini Capetown nchini humo.
Itakumbukwa kwamba uvamizi unaotokamana na chuki dhidi ya wageni umekuwa ni jambo maarufu nchini Afrika ya Kusini kwa muda sasa. Mwaka 1994 na 1995 vijana waliokuwa na silaha walivunja nyumba za wageni mjini Johannesburg, wakiwataka polisi kuwarejesha raia hao makwao. Mwaka 2008 matukio ya uvamizi dhidi ya wageni yalijiri tena hapo hapo (Johannesburg) kiasi cha kuwafukuza na kuwatoa kwenye makaazi yao maelfu ya wahamiaji, kulitendeka wizi mkubwa wa mali, biashara na wa majumbani, na idadi ya waliofariki kufikia hadi 56. Pia mwaka 2015 matukio kama hayo yalitokea kufuatia kauli za uhamasishaji za Mfalme wa Wazulu Goodwill Zwelithini kaBhekuzulu alipowataka wahamiaji “wafunge virago vyao na kuondoka mara moja”. Ndani ya mwezi Aprili mwaka huo huo (2015) watu saba waliuwawa, na wageni wengine zaidi ya 2000 walitolewa kwenye makaazi yao.
Hali hii imezua chuki dhidi ya wageni wanaoingia Afrika ya Kusini. Waafrika ya Kusini wengi hudhani kwamba wahamiaji wanapora fursa zao na ndio dhamana wa umaskini wao, badala ya wao kukabiliana na chanzo halisi, ambacho ni sera thakili za uchumi wa kibepari.
Mfumo wa kibepari waliorithi kutoka kwa wakoloni wa Kiengereza umechochea hisia za kibaguzi za kiaswabia/utaifa hususan miongoni mwa vijana. Fikra za uchoyo wa Kiutaifa zimezuwa mauwaji ya wengi, uporaji kwa jina la kuhami rasilmali za nchi kutokana na kuvamiwa na wageni.
Nidhamu ya uchumi ya kibepari imeisukumiza Afrika ya Kusini katika shimo kubwa la kukosekana uwiano wa kiuchumi baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. (maskini na matajiri). Afrika ya Kusini imekuwa ni moja katika nchi ambayo imekosa kwa kiasi kikubwa uwiano na usawa huo wa kiuchumi baina ya raia wake. Wakati raia wao wengi wakimwaga lawama kwa wageni na kujijaza fikra za chuki dhidi ya wahamiaji, ukweli ni kuwa nchi hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi na kubwa zaidi kuliko uwepo wa wageni.
Kwa mfano, madai kuwa wageni wamekuwa shehena katika huduma zao za kijamii ikiwemo suala la mpango wa Afya wa kitaifa, taarifa za serikali zinaonesha kwamba nchini humo kuna wageni 2.1 katika idadi yao ya watu 51.7 milioni. Idadi hiyo ni kwa mujibu wa hesabu ya 2011 (kwa sasa inawezekana idadi hiyo imeshapaa mpaka milioni 55.7).
Afrika ya Kusini licha ya kuitwa kuwa miongoni mwa vinara bora wa demokrasia, nchi ya pili kuwa na uchumi wa juu barani Afrika, ikiwa na miundo mbinu bora, nidhamu mwanana iliyoboreshwa ya masuala ya kifedha na kuwepo uzalishaji wa hali ya juu wa maadini na viwandani, ukweli uliopo bado nchi hiyo inakabiliwa na msinyao mkubwa katika uchumi wake hususan robo ya mwanzo ya mwaka 2019, pia ikikabiliwa msambaratiko mkubwa wa kijamii.
Kuhusiana na ukosefu wa ajira, suala hilo limekita na kutapakaa nchini Afrika ya Kusini, kiasi cha Raisi Ramaphosa kuwahi kusema kuwa ni “mgogoro mkubwa na wa hatari” . Julai mwaka huu 2019 kiwango cha ukosefu wa ajira kitaifa kilikuwa ni 29% kikiwahusisha watu karibu milioni 6.7. Baadhi ya 56.4% ya vijana wa miaka 15- 24 hawana kazi, na kiwango cha 35.6% kwa wenye miaka 25-34 nao hawana kazi. Kadhalika 71% ya wasioajiriwa hutumia kipindi cha mwaka au zaidi wakiendelea katika kutafuta kazi.
https://qz.com/…/what-is-behind-south-africas-xenophobic-a…/
Sura pana katika jamii ya Afrika ya Kusini, ni kama zilivyo jamii nyengine chini ya ubepari kama hiyo, imeemewa na kuchanganyikiwa bila ya kuwa na suluhisho halisi kutatua matatizo yao ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, na badala yake hukimbilia kulaumu na kuwasingizia wageni wakiwa wao ndio mbuzi wa kafara, huku wanasiasa wakionekana kuyaunga mkono matukio ya chuki hizo kijanja, ikiwa ni mbinu yao ya wao kujikusuru (kukwepa lawama).
Uhalisia ni kuwa serikali imeshindwa kutatua matatizo yao yaliyoibuka kutokana na mfumo wa kibepari, na hivyo kuhamishia tatizo la umasikini kuwa linasababishwa na wageni na wahamiaji, kitu ambacho hatima yake ni huzua umwagaji damu na vurugu la ukatili kama zama za ubaguzi wa rangi au zaidi kamwe.
Zaidi ya hayo, vurumai hizi za chuki dhidi ya wageni Afrika ya Kusini zinafedhehi waziwazi fikra butu ya ‘Umajmui wa Afrika’, kauli mbiu tupu bila ya uhalisia, kama ilivyo fikra ya ‘Umajmui wa Waarabu’. Aidha, ni kielelezo cha fedheha ya wazi ya kushindwa dhana ya ukabila, fungamano duni na tete mno, kwa kuwa baadhi ya jamii za makabila zinazoishi Afrika ya Kusini kama Wazulu na Xhosa ndio jamii za makabila ya watu hao hao yanaoishi katika nchi za jirani kama Botswana, Lesotho, Zimbwabwe, Malawi, Msumbiji nk. lakini bado watu hao hawakusalimika walidhuriwa kwa ukatili na wimbi hili la chuki dhidi ya wageni, wakihesabiwa kuwa nao ni wageni
Ubepari shahir dhahir umeshindwa katika sekta ya kiuchumi na kijamii. Unazalisha umasikini na kutengeneza pengo baina ya wenye nacho na wanyonge, unazalisha husuma / uadui ukikosa fungamano thabiti na imara kuwafungamanisha watu pamoja. Tumaini pekee la kuuokoa ulimwengu kutokana na minyonyoro ya ubepari ni Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah Rashidah
Imeandikwa na Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.