Thamani Ya Wakati Katika Matendo
بسم الله الرحمن الرحيم
Wakati au muda umechukua mjadala mkubwa sana miongoni mwa jamii kiujumla na wasomi katika kutafuta uhalisia wake na thamani yake ukizingatiwa mwanzo wake na mwisho wake.
Kauli ya baadhi ya wasomi wa kisekula kuwa muda ni kitu kipo kidaima hakina mwanzo wala mwisho wake, na wengine wakasema una mwanzo wake na mwanzo wake ni pale ulipotokea mlipuko mkubwa (big bang).
Tukifuatilia uhalisia wa muda kwa kuzingatia mwanzo wake na mwisho wake ni kuwa hupimwa kiakili, kwani muda ni wenye kuhisika tu na hudhihirika kupitia mwanzo wa tukio na mwisho wake.
Kupitia vitendo ndiyo hudhihirika uhalisia wa muda kuwa ni mwanzo, na mwisho wa vitendo husika, mfano usiku ni wenye kuingia kwa mwanzo wake, na mchana vivyo hivyo, ni matukio kama haya ndiyo yanaonesha kuanza kwa muda husika na kuisha kwake.
Kwa kuzingatia hayo, tunaona kwamba kila dhihiriko (tukio) la muda lina chanzo chake, na chanzo cha matukio haya ni Mwenyezi Mungu, Mola, Muumbaji wa kila kitu, Allah (SWT). Ndiyo akasema katika kitabu chake Al Quraan, Al Kareem kuwa:
وَجَعَلْنا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِتَبْتَغُوا فَضْلاً مِنْ رَبِّكُمْ وَلِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ وَكُلَّ شَيْءٍ فَصَّلْنَاهُ تَفْصِيلاً (الإسراء: 12).
“Na tumeujaalia usiku na mchana kuwa ishara mbili, tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu, na mpate kujua idadi ya miaka na hesabu”(Q 17:12)
Thamani na hadhi ya muda fulani inawezwa kutajwa na Allah Taala mwenyewe kwa elimu yake kuwa muda fulani una hadhi na utukufu fulani. Amma kwa upande mwengine wa kibinadamu tunaupima muda kama mfano wa boksi tupu ambalo hutumika kuhifadhia vitu, hivyo thamani ya boksi hili huwa ni kutokamana na thamani ya vitu ilivyobeba.
Ni wazi kuwa muda huwa na thamani kutokana na vitendo na matukio yayofanywa au kujiri katika muda husika. Kwa mfano, muda wa mwezi wa Ramadhani ni wenye thamani na hadhi kubwa ni kutokana na kushushwa Qurani tukufu katika mwezi huo, usiku iliyoshuka Quran hiyo ukawa ndiyo bora kuliko masiku mengine.
Anasema Allah Taala kuwa:
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ (القدر: 1).
“Hakika sisi tumeiteremha Qurani katika Laylatul Qadri (usiku wa cheo)”(Q 97 :1)
Hivyo, haipatikani thamani ya muda iwe ni kwa faida au kwa hasara isipokuwa itakuwa ni yenye kufungwa na tukio lenye kufanyika katika muda huo. Tukio au kitendo ndani ya muda huo ndicho chenye kupandisha au kushusha thamani ya muda wetu.
Allah (SWT) kwa uzito wa jambo hili la kupatilizia muda wetu kwa matendo mema akatuambia katika kitabu chake kitukufu Al Quran Al Kareem kuwa:
وَالْعَصْرِ
إِنَّ الإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ
“Naapa kwa zama (muda): hakika binadamu yupo katika hasara, ila wale walioamini na wakatenda matendo mema (Q103;1-3)
Tukio la Mtume (SAW) na masahaba ra. kuhajiri kutoka Makka kwenda Madina, na hatimaye kuasisi serikali ya kwanza ya Kiislamu lilikuwa tukio hili ndiyo nukta msingi kwa masahaba ra. kuanzisha kalenda ya Kiislamu. Hii ni kutokana na thamani kubwa ya tukio hili ukilinganisha na matukio mengine kama ufunguzi wa Makka, Israi na Miiraj nk.
Hii ni katika thamani yenye kuonekana kiwazi kwa macho yetu, na kimsingi kuna mambo makubwa mengi yanayoweza kupatikana au kufanyika katika vitendo vya binadamu katika muda husika na hivyo kuupa muda huo thamani kubwa au kuupunguzia muda huo thamani.
Kwa kuzingatia hayo, thamani ya muda haipatikani ila kwa vitendo au matukio yaliyofanyika ndani ya muda ule. Kama ambavyo Ummah wa Kiislamu kipindi cha Mtume SAAW waliishi katika dhiki chini ya mfumo wa kikafiri lakini hatimaye walifanya kazi na kuishi chini ya mfumo wa Kiislamu wakitawaliwa na serikali ya Kiislamu ya kwanza (Al Nubuwah) na hivyo wakawa wameupa thamani muda wao kidogo walioishi katika maisha ya hapa duniani, hivyo hivyo na Ummah wa Kiislamu katika zama hizi ni lazima kufanya kazi kurejesha maisha ya Kiislamu kupitia kurejeshwa kwa serikali ya kiulimwengu ya Kiislamu (Khilafah) ili hatimaye maisha yawe na thamani na maana na tuweze kupata radhi za Allah Taala :
وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُم فِي الأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَى لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُمْ مِنْ بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا َ
“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale Walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kuwa atawafanya Makhalifah katika ardhi kama alivyowafanya kabla yao na kwa yakini atawasimamishia dini yao aliyowapendelea, atawabadilishia amani baada ya khofu yao” (Quran 24:55)
Ahmad Ally
Risala ya Wiki No. 93
11 Rabi’ al-thani 1442 Hijri / 27 Novemba 2020 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.