Kiwango cha Juu Zaidi Anachostahiki Kupewa Mtu Katika Zaka

بسم الله الرحمن الرحيم

 Swali:

Assalamu Alaikum shaikh, nina swali. Je, waweza kulijibu upatapo muda, tafadhali?

Ni kiwango kipi cha juu zaidi anachostahiki kupewa mtu katika Zaka? Kwa mfano, je mtu anaweza kupata pesa za kutosha za kujenga nyumba ikiwa hana nyumba? Au kuna kikomo chochote juu ya kiwango ambacho mtu anaweza kupokea? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

 Jibu:

Wa Alakum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh.

Swali lako ni kuhusu kiwango cha juu zaidi anachoweza kuchukua mtu anayestahiki zaka kutoka katika zaka.

Na jibu ni kwamba, halijaja andiko (nasw) la kisheria la moja kwa moja linalo bainisha kiwango cha juu ambacho anapewa mtu anayestahiki zaka. Lakini aya ya zaka (Sadaqah) ambayo Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ)

“Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima” [At-Tawba: 60].

Inawezekana kuvuliwa (kutokana na aya hii) kiwango cha juu zaidi anachoweza kupewa mtu anayestahiki zaka. Hilo ni kwa sababu, wanaostahiki zaka wametajwa kwenye aya kwa sifa zenye kujulisha sababu za wao kupewa zaka na hilo lina maana kuwa, wao kupewa zaka kumefungamanishwa na sababu ya kisheria (‘illa) ambayo inawafanya wao kustahiki kupewa zaka. (Kwa hiyo) maadamu watakuwa na hiyo sifa basi watapewa zaka, na wakikosa hiyo sifa basi hawatapewa.

Kwa mfano: Mafukara na Masikini: Wanastahiki zaka kwa sababu ya sifa ya ufukara na umaskini. Kwa hiyo, kiwango cha juu zaidi watakachopewa katika zaka ni kile kitakachowafanya wasihitajie tena zaka. Yaani, kitakacho watosheleza, mpaka wawe hawastahiki tena kupewa zaka. Yaani, kwa kupewa zaka watakuwa hawana tena sifa ya ufukara wala sifa ya umaskini, na haifai kupewa zaidi ya hivyo. Na hicho kiwango kimaumbile kinatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwengine, na kutoka hali moja hadi nyengine.

Na mfano:  Wakusanyaji zaka, watapewa zaka kwa sababu, wao hufanya kazi ya kukusanya zaka. Yaani, wanapewa kwa mkabala wa juhudi wanazotoa katika ukusanyaji zaka, na serikali itakadiria malipo yao kulingana na juhudi zao. Ikiwa serikali haitakadiria, basi watalipwa ujira unao nasibiana nao wala hawatozidishiwa, kwa sababu zaka sio msaada kwao, bali (wanapewa kwa) mkabala wa juhudi zao.

Na mfano: Wanaodaiwa (Al-Gharimun), wanapewa katika zaka kile kitakachotimiza kulipia madeni yao, wala hawatapewa zaidi. Kwa sababu, kilichofanya wastahiki zaka ni madeni, na hiyo sifa ikiondoka kwao hawatostahiki zaka.

Na hivyo hivyo kwa makundi yote ya wastahiki zaka, watapewa katika zaka kiasi ambacho kitaondoa sifa iliyofanya wastahiki kupewa zaka.

Na tulikwisha taja baadhi ya maana yaliyo bainishwa hapo juu kwenye kitabu cha “Mali ya Dola ya Khilafah” katika mlango wa: Matumizi ya Zaka, kama ifuatavyo:

1. Mafukara (Al-Fuqaraa): Nao ni wale ambao hawafikiwi na mali inayotosha kukidhi mahitaji yao ya msingi. ambayo ni: chakula, mavazi, na makaazi. Kwa hiyo, yeyote anayepata mapato kidogo zaidi yasiyoweza kukidhi mahitaji yake msingi, huyo atazingatiwa ni fukara, na zaka ni halali kwake, anaruhusiwa kuichukua. Na yafaa kupewa zaka kwa kiasi kitakacho ondoa mahitaji yake na ufukara wake.

Na hakika Mwenyezi Mungu amewaharamishia matajiri kuchukua zaka. Amepokea Ahmad, na wenye Sunan, kutoka kwa Abdullahi ibn Amri amesema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (swa):

 «لا تحل الصدقة لغنيّ، ولا لذي مِرَّةٍ سَوِيّ»

“Si halali zaka kwa tajiri wala mwenye nguvu sawa”.

Na “Dhuu Mirratin” ni mtu mwenye nguvu na uwezo, anaye chuma. Na endapo atakosa chumo atazingatiwa kuwa ni fukara. Na tajiri: ni yule aliyejikwasia kutoka kwa wengine, na akawa na pato linalozidi mahitaji yake. Na zimekuja hadithi zilizo bainisha nani tajiri. kutoka kwa Abdullah ibn Mas’ud amesema: amesema Mtume (saw):

«ما من أحد يسأل مسألة، وهو عنها غني، إلاّ جاءت يوم القيامة كدوحاً، أو خدوشاً، أو خموشاً في وجهه. قيل: يا رسول الله، وما غناه، أو ما يغنيه؟ قال: خمسون درهماً، أو حسابها من الذهب»

 “Hakuna yeyote atakaye ombaomba hali ya kuwa yeye ni tajiri, isipokuwa atakuja Siku ya Kiyama akiwa mwenye taabu, au mwenye mikwaruzo kwenye uso wake. Wakasema: Ewe Mtumbe wa Mwenyezi Mungu, ni nini utajiri wake? Na nini kinamfanya kuwa tajiri? Akasema: Ni dirham hamsini, au kiasi chake kwa dhahabu” (Imepokewa na maimamu watano).

Kwa hiyo, anayemiliki dirhamu hamsini za fedha – yaani: gramu 148.75 za fedha au kiwango sawa cha dhahabu – iliyozidi chakula chake, mavazi yake, makaazi yake, na mahitaji ya watu wake na watoto wake na mtumishi wake, hapo atazingatiwa kuwa ni tajiri, na haitofaa kwake kuchukua zaka.

2. Masikini (al-Masaakin): Nao ni wale wasio na chochote, kukosa kumewatuliza. Na wala hawaombi watu. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

“ليس المسكين الذي يطوف على الناس ترده اللقمة واللقمتان، والتمرة والتمرتان. ولكن المسكين الذي لا يجد غنى يغنيه، ولا يفطن به فيتصدق عليه، ولا يقوم فيسأل الناس”.

Maskini sio yule ambaye huwazungukia watu, akirudi kwa kupewa tonge moja ama mawili, na tende moja ama mbili. Lakini maskini ni yule asiye na kinachomtosheleza. Wala hatambuliki na kupewa sadaka, wala yeye hasimami na kuwaomba watu” (Imepokewa na Bukhari na Muslim).

Na maskini yuko chini ya fukara. Kwa neno lake Mwenyezi Mungu:

أو مسكسيناً ذا متربة

“Au masikini aliye vumbini” [Al-Balad: 16]

Yaani aliyeambata mchanga kwa sababu ya kukosa nguo, na kwa sababu ya njaa yake. Na maskini zaka ni halali kwake, na anafaa kuichukua. Na yafaa apewe katika zaka mpaka kiasi kitakacho muondelea umaskini wake, na kumfanya kuwa mwenye kujitosheleza na kushibisha mahitaji yake msingi.

3. Wanafanya Kazi ya Zaka (al-‘Amilina ‘Alyha): Nao ni wale wanao teuliwa ili kukusanya zaka kutoka kwa wanao paswa kutoa, au kuisambaza kwa wanao stahiki. Na watapewa katika zaka hata kama ni matajiri, mkabala wa ukusanyaji wao au kusambaza. Amepokea Abu Ubaid kutoka kwa Atwaa ibn Yasaar amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

“لا تحل الصدقة لغني إلاّ لخمسة: عامل عليها، أو رجل اشتراها بماله، أو رجل له جار فقير تصدّق عليه بصدقة فأهداها إليه، أو غازٍ، أو مغرمٍ”

“Zaka si halali kwa matajiri isipokuwa watu aina tano: mwenye kuikusanya, au mtu aliyeinunua kwa mali yake, au mtu ambaye ana jirani fakiri anaye mpa zaka kisha akamuongoza katika matumizi, au mpiganaji vita vya Jihad, au mwenye deni”

وعن بسر بن سعيد «أن ابن السعدي المالكي قال: استعملني عمر على الصدقة، فلما فرغت منها، وأديتها إليه، أمر لي بعمالة، فقلت: إنّما عملت لله. فقال: خذ ما أعطيت، فإني عملت على عهد رسول الله ، فعملني، قلت مثل قولك، فقال لي رسول الله : إذا أعطيت شيئاً من غير أن تَسألَ فَكُلْ وتَصَدَّق» متفق عليه.

Na kutoka kwa Busr ibn Said, kwamba ibn Saadi Almaaliki amesema: Umar aliniteua ili kukusanya zaka, na nilipomaliza na kumkabidhi, aliamrisha nipewe malipo. Nikamwambia: sikufanya ila kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Akasema: Chukua ulicho pewa. Kwa hakika mimi pia nilifanya kazi kama hiyo wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akanilipa, nikamwambia mithili ya maneno yako. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akaniambia: “Ukipewa kitu bila ya wewe kuomba basi kula (chukua) na utoe sadaka”. (Bukhari na Muslim).

Wenye Kuunganishwa Nyoyo Zao (Al-muallafatu qulubuhum): Nao ni kundi la viongozi, au wenye ushawishi, au mashujaa, ambao iman zao hazijakita mizizi na Khalifah au mawali wake wakaona wapewe kitu katika zaka ili kuziunganisha nyoyo zao, au kuzitia nguvu iman zao, au kwa ajili ya kuwatumia kwa maslahi ya Uislamu/Waislamu, au ili waweze kushawishi makundi yao. Hii ni sawa na ambavyo Mtume (saw) aliwapa, kama vile: Abu Sufyan, Uyaina ibn Hisn, Al-Aqra ibn Habis, Abbas ibn Mirdaas, na wengineo.

«أن رسول الله صلى الله عليه وسلم أتي بمال، أو سبي فقسمه، فأعطى رجالاً، وترك رجالاً، فبلغه أن الذين ترك عتبوا، فحمد الله، ثم أثنى عليه، ثمّ قال: أمَّا بعد، فوالله إني لأعطي الرجل، وأدع الرجل، والذي أدع أحب إليّ من الذي أعطي، ولكني أعطي أقواماً، لما أرى في قلوبهم من الجزع والهلع، وأَكِلُ أقواماً إلى ما جعل الله في قلوبهم من الغنى والخير»

Imepokewa kutoka kwa Amri ibn Taghlib, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliletewa mali – au mateka – akaigawa. Akawapa watu, na wengine hakuwapa. Akafikiwa (na habari) kwamba, ambao hawakupewa wanamlaumu! (Mtume (saw) Akamhimidi Mwenyezi Mungu kisha akamsifu, kisha akasema: “Ama baada ya hayo, naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi humpa mtu na kumuacha mwengine, wakati niliyemuacha ni mpendwa zaidi kwangu kuliko niliyempa. Lakini mimi huwapa watu kwa kile ninachokiona nyoyoni mwao kutokana na upapiaji na mbabaiko, na wengine nawategemeza kwa yaliyomo nyoyoni mwao kutokana na ukwasi na kheri” (Bukhari).

Na hawa wanao unganishwa nyoyo zao hawapewi katika zaka ila tu wakiwa ni Waislamu. Wakiwa ni makafiri hawatopewa katika zaka, kwa sababu, zaka haipewi kafiri. Kwa maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akimwambia Muadh alipomtuma Yemen:

(فأعلمهم أن الله افترض عليهم صدقة في أموالهم، تؤخذ من أغنيائهم، وترد على فقرائهم) رواه البخاري من طريق ابن عباس.

Basi, wajulisheni kwamba Mwenyezi Mungu amewafaradhishia zaka katika mali zao. Itachukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kurudishwa kwa mafukara wao.” (Bukhari).

Kama ambavyo pia hawatopewa ila ikiwa sababu ya kisheria (‘illah) iliyo sababisha wao kupewa bado ipo. Na ikikosekana hawatopewa, kama alivyo kataa Abu Bakr na Umar kuwapa, pale Uislamu ulipokuwa na nguvu na kusambaa.

Watumwa (ar-Riqaab): Nao ni walio utumwani. Watapewa katika zaka ili kuwakomboa ikiwa wana mkataba huo, ama kuwanunua kwa mali ya zaka na kuwaacha huru ikiwa hawana mkataba. Na leo hakuna watumwa.

Walio na Madeni (al-Ghaarimun): Nao ni waliojibebesha deni ili kusuluhisha mzozo, au kulipa pesa za ridhaa (Diyah), au kukidhi mahitaji yao binafsi. Ama ambao wamebeba madeni kwa ajili ya kupatanisha watu, au kulipa diyah, watapewa katika zaka wawe ni mafukara au matajiri. Na watapewa tu kiwango walichojibebesha bila ya ziada. Kutoka kwa Anas r.a kwamba Mtume (saw) amesema:

إن المسألة لا تحل إلاّ لثلاثة، لذي فقر مدقع، أو لذي غرم مفظع، أو لذي دم موجع .

“Hakika, kuomba si halali ila kwa watu watatu: mwenye ufukara kupindukia, au mwenye madeni yalomlemea, au mwenye damu inayomuumiza (Deni la Diyah)”.

وروى مسلم وأبو داود والنسائي عن قبيصة بن مخارق الهلالي قال: «تحملت حَمَالَةً، فأتيت رسول الله ، أساله فيها، فقال: أقم حتى تأتينا الصدقة، فنأمر لك بها، ثمّ قال: يا قبيصة، إن المسألة لا تحل إلا لأحد ثلاثة: رجل تحمل حمالة، فحلت له المسألة حتى يصيبها، ثمّ يمسك، ورجل أصابته جائحة اجتاحت ماله، فحلت له المسألة حتى يصيب قواماً من عيش، أو قال سداداً من عيش، ورجل أصابته فاقة حتى يقول ثلاثة من ذوي الحجا من قومه لقد أصابت فلاناً فاقة، فحلت له المسألة حتى يصيب قواماً من عيش، أو قال: سداداً من عيش، فما سواهن في المسألة يا قبيصة، فَسُحْتٌ يأكلها صاحبها سُحْتاً “.

Na amepokea Muslim, Abu Daud, na Nasai kutoka kwa Qubaiswa ibn Makhariq Alhilali amesema: Nilijibebesha deni, nikamwendea Mtume (saw) nikimwomba, akasema: “Subiri mpaka tufikiwe na zaka ili tuamrishe upewe”. Kisha akasema: “Ewe Qubaiswa, hakika kuomba si halali ila kwa mmoja kati ya watatu: mtu aliyebeba deni: ikawa halali kwake kuomba hadi apate, kisha ajizuilie. Na mtu alopatwa na mkasa ulioangamiza mali yake: ikawa halali kwake kuomba hadi apate kitakachosimamisha maisha yake. Na mtu alopatwa na shida, hadi waseme watatu miongoni mwa wenye akili katika watu wake: hakika fulani amepatwa na shida. Hivyo iwe halali kwake kuomba, hadi apate kitakachosimamisha maisha yake. Wasiokua hao katika kuomba Ewe Qubaiswa ni haramu tu wanayokula (Suhut).

Ama wale wanaobeba madeni ili kukidhi mahitaji yao binafsi: watapewa katika zaka ili walipe hayo madeni wakiwa ni mafukara, au sio mafukara ila wameshindwa kulipa madeni yao. Na ama wakiwa ni matajiri wanaoweza kulipa madeni yao, hawa hawatopewa zaka, kwa sababu zaka sio halali kwao.

Walio Katika Njia ya Mwenyezi Mungu (Fi Sabilillah): Yaani walio kwenye Jihad, na mahitaji yake, na ambayo Jihad haitimii bila kupatikana kwake: kama vile kuunda jeshi, kuwepo viwanda, kutengeza silaha. Na popote pakitajwa katika njia ya Mwenyezi Mungu” (fii sabilillahi) kwenye Qur’an basi haina maana nyengine ilaJihad tu. Kwa hiyo, itatolewa katika zaka kwa ajili ya Jihad na yanayolazimu. Wala haitokadiriwa kiwango maalumu, bali yafaa kutengewa zaka yote au baadhi yake kwa ajili ya Jihad, kulingana na Khalifah atakavyoona yenye maslahi kwa wanaostahiki zaka. Amepokea Abu Daud kutoka kwa Abu Said, amesema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

لا تحل الصدقة لغني إلا في سبيل الله…” وفي رواية له:”…أو لغاز في سبيل الله..”

“Si halali (kupewa) zaka tajiri ila akiwa katika Jihad katika njia ya Mwenyezi Mungu…” – Na katika mapokezi mengine – “au kwa mpiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu …”

Aliyekatikiwa na Safari (Ibn us-Sabiil): Naye ni asiye na mali ya kumfikisha mjini kwake . Atapewa katika zaka kiasi kitakachomfikisha mjini kwake, kiwe kichache au kingi.

Pia atapewa matumizi yatakayomtosha njiani hadi kufika mjini kwake. Atapewa katika zaka hata kama mjini kwake ni tajiri. Kwa kauli yake Mtume (S.W.A): “

“لا تحل الصدقة لغني إلا في سبيل الله، أو ابن السبيل أو..(رواه أبوداود).

Si halali (kupewa) zaka tajiri ila akiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, au msafiri …” (Abu Daud).

Na wasio kwenye makundi haya manane yaliyotajwa katika aya hawafai kupewa zaka. Haitotolewa katika zaka ili kujenga misikiti, au hospitali, au huduma za misaada au katika maslahi yoyote ya serikali au ya ummah. Kwa sababu zaka ni milki maalumu kwa makundi manane tu, na wala hawana mshirika mwengine yeyote katika zaka. Na Khalifah ndiye mwenye mamlaka ya kuisambaza zaka kwa haya makundi manane, kulingana na atakaloona litatimiza maslahi ya haya makundi manane, kama alivyo kuwa akifanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Makhalifah baada yake. Na yafaa kwa Khalifah kuigawa zaka kwa makundi haya manane. Vilevile, anaweza kutosheka kulipa baadhi ya kundi, kulingana na atakaloona lina maslahi na haya makundi. Na kama hayatapatikana haya makundi basi zaka itahifadhiwa katika hazina ya mali, katika diwani ya Sadaqah, ili iweze kusambazwa kwa makundi husika pale watakapoihitaji.

Amepokea Abu Ubaid kutoka kwa Ibnu Abbaas amesema kuhusu zaka:” Pindi utakapoigawa kwa kundi moja katika makundi manane hilo litakutosheleza”. Hivyo hivyo amesema Atwaa, na Hasan. Na amesema Malik:” Suala la kugawanya zaka kwa mtazamo wetu, ni kwamba suala hilo haliwi ila kwa ijtihad ya mtawala. Kwa hiyo, makundi yoyote ambayo yatahitaji na kuwa wengi, basi litatangulizwa hilo kundi kwa kiwango atakachoona mtawala”.

Mwisho wa nukuu kutoka katika Kitabu cha Mali katika Dola ya Khilafah (Al-Amwaal Fii Dawlat al- Khilafah.

Natumai hayo yanatosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwingi wa Hekima.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah.

17/8/1441 H 10/4/2020 M

 

Maoni hayajaruhusiwa.