‘Uhuru’ Kibwagizo cha Ukoloni Mpya
Ni jambo la kimaumbile mwanaadamu kupenda kuwa juu na wala sio chini ya wengine, ndio maana mataifa mengi yaliyokuwa chini ya wakoloni kwa nyakati tofauti yameonesha juhudi za ‘kujikomboa’. Bara la Afrika likiwa ni makoloni isipokuwa nchi ya Ethiopia pekee.
Uhuru ni hali ya nchi kujitawala (kujiamulia mambo yake) kiuchumi, kisiasa, kijamii na nyanja nyingine zote za maisha ikiwemo thaqafa (civilization) yake.
Historia inaonesha kwamba vuguvugu la kudai mabadiliko katika nchi tawaliwa sio zao la mawazo/fikra za wanasiasa wao (japo hutakiwa kuaminishwa ni za kwao) bali ni mapokeo na miongozo kutoka kwa mataifa tawala/ wakoloni baada ya kufahamu kwamba watawaliwa wamewachoka wazungu, na sio fikra za kimagharibi.
Ndiyo utakuta mabadiliko ya upatikanaji wa kinachoitwa uhuru yalitokea takriban katika kipindi sawa tena kwa mpangilio maalumu. Uhuru katika Afrika, kwa mfano, ilikuwa haswa miaka ya katikati ya 1950 na katikati ya 1960, ndiyo hata mwaka 1960 ukaitwa mwaka wa Afrika, kwakuwa nchi nyingi zilipata huo unaoitwa ‘Uhuru’. Ikitanguliwa na kukomesha biashara ya utumwa (ikilenga kupata soko baada ya uzalishaji katika nchi za wakoloni kuimarika), baadae ukafuata ‘mfumo mpya wa vyama vingi’, kisha sheria ya ‘mapambano dhidi ya ugaidi’, na kufuatia ‘mabadiliko ya katiba’ .
Wakoloni wakubwa duniani walikuwa ni nchi za Ulaya ambao waligawana kutawala ulimwengu kwa kuchora mipaka na ramani kama ilivyoshuhudiwa katika maazimio ya Mkutano wa Berlin, Ujerumani mwaka wa 1884-5, kisha wakaendelea kunyonya na kupora rasilimali vitu na watu katika nchi walizo kalia.
Baada ya Vita ya Pili ya Dunia, Ulaya iliathirika sana na vita kiasi cha kupoteza uwezo wao wa kushawishi mataifa mengine kisera na maamuzi. Udhaifu huu ulitoa mwanya kwa Marekani (lilikuwa koloni la Uingereza lililoibuka kuwa dola kubwa) kujipanga, kujikuza na kutaka kutanua athari na ushawishi wake kama mkoloni mpya duniani.
Marekani ilianzisha vuguvugu la fikra ya uhuru kwa mataifa koloniwa. Lililenga kuwaamsha raia wa nchi makoloni kuzinduka na kupinga ukoloni (uwepo wa Ulaya) katika ardhi zao. Ndio zikaibuka fikra ndani yake za Uzalendo wa Afrika, “Pan-Africanism” ikiwa na kaulimbiu ya Afrika kwa Waafrika. Ndipo waliposikika na kuonekana wanafikra (thinkers) wa vuguvugu hilo kama vile Marcus Garvey, Du Bois nk katika weusi waliokuwa Marekani kueneza athari hizi kwa waliokuwa Afrika.
Ulaya ikiongozwa na mataifa ya Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ilishitukia hatari inayoikabili ya kupoteza ushawishi katika makoloni yake, hususan Afrika. Kwa kuwa Uingereza ilikuwa hodari kisiasa zaidi ya Marekani (lilikuwa koloni la Uingereza) ilibaini kwamba lengo sio kubadili mfumo, bali ni kubadili watu (weusi badala ya weupe). Uingereza kwa haraka iliamua kutumia mbinu hii ya Marekani na kuiteka kuifanya yake na kisha kuiboresha. Ndipo walipoanzaUingereza walipoanza kuandaa watu katika raia wa nchi makoloni kuibeba agenda ya Uhuru huku wakiwaunga mkono kwa hali zote za kimaarifa, kiuchumi na kiulinzi.
Walianzisha vikundi/vyama vya uhuru kwa maeneo ambapo havikuwepo na kuingiza watu wao kule katika nchi ambazo vyama vilishakuwepo. Walichagua watu kupitia walimu wao ambao walikuwa wakifundisha katika shule walizo zimiliki. Walichaguliwa watu ambao kwa vigezo walivyopewa walimu, walikuwa wameiva kimfumo, na kuwa wanyenyekevu (loyal) kwao.
Ndivyo hata alivyosema Lord Maccaulay, mmoja wa waratibu wa elimu ya kikoloni alipoongelea ‘harakati’ za uhuru Misri alisema:
“Uingereza haitakuwa tayari kuikabidhi nchi yoyote uhuru mpaka pale itakapoona wapo raia ambao wamesoma katika mfumo wetu, kwa sababu yeyote aliyepitia katika mfumo huu ni tofauti na aliyesoma katika mfumo wa asili” (yaani Uislamu).Kwa kauli hiyo walijua fika tangu awali kwamba Uislamu ndio kitisho chao kimfumo.
Baada ya kuchaguliwa walioonekana kufaa kukabidhiwa nchi, walijengewa vigezo na umahiri kwa kupewa nafasi katika vyuo vikuu vya Uingereza na Marekani kikiwemo chuo kikuu cha Edinburg na Lincoln, walijengwa zaidi ki thaqafa kwa elimu maalum na miongozo ya kiutendaji. Wakarejea na kuingia au kuanzisha vyama baada ya kutangulizwa sera ya kwamba lazima kuwe na vyama/vikundi kwa ajili ya shughuli za kisiasa. Na ndio utakuta hata vyama vyao wengi vilikuwa na majina yanayoendana (NU-National Union; KANU,ZANU,TANU nk) kwa kuwa vilikuwa na chimbuko na muelekeo mmoja kutoka kwa bwana mmoja. Hatimaye wakakabidhiwa nchi baada ya maafikiano yaliyofanyika katika jumba la Lancaster House, London. Ndio hata katiba zao pia zina muelekeo huo huo wa Uingereza hadi hivi leo, kwa kuwa sio za kwao.
Katika Tanzania utakuta kila tarehe 9 Disemba huadhimishwa kama siku ya uhuru, ambapo uhuru hutajwa kupatikana mwaka 1961. Lakini cha kujiuliza huku tukijua maana ya uhuru; Je, baada ya Uhuru wa Disemba 1961 ni nani alikuwa mkuu wa nchi? kwanini?. Bila shaka kila mmoja anaweza kuwa na majibu yake lakini uhalisia ni kwamba mkuu wa nchi alikuwa Mtawala wa Uingereza (Malikia), na sababu ni kwamba walikuwa bado wanamchunguza Waziri mkuu (probation period) kuona uwezo wake na anavyotekeleza matakwa yao na kuhakikisha kuendelea kwa maslahi yao. Na baada ya kujiridhisha kwamba anafaa, ameelewa maelekezo, ndipo akawa Rais na uwaziri mkuu kumuachia Rashid Kawawa, na wala sio suala la ujamhuri. Hili linatiliwa nguvu pia na hoja kwamba, Tanzania iliendelea kuwa chini ya Uingereza hata baada ya ‘Uhuru’, ndiyo tukaona Uingereza ikiingilia kati jaribio la mapinduzi la mwaka 1963.
Leo Marekani imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuondoa athari na ushawishi wa madola ya Ulaya hususan Uingereza kupitia mlango wa vyama vingi kwa kuweka vibaraka wake, likiathiri mataifa mengi kwa sera zake, nchi za Afrika nazo zimejikuta katika mkondo huo huo wa kubadilika kuondokana na mabwana wa asili yaani Uingereza na Ufaransa na kuwa na bwana mwingine Marekani.
Hata Tanzania ililazimika kukubali vyama vingi ikiwa ni shinikizo na mbinu mpya ya Marekani kuondoa athari ya Uingereza, Rais Nyerere (alkiyekuwa upande wa Uingereza) akaamua ‘kung’atuka’ kwakuwa alitaka kulinda hadhi yake aliyojijengea. Vyama vingi ni mlango mwengine wa wakoloni kuingiza vibaraka wao katika mamlaka wanazozimendea.
Kawaida ya kimaumbile, hakuna aliye tayari kuacha kunufaika na machumo mema anayoyapata ila kwa kunyang’anywa, tena baada ya mivutano na hata mapigano makali kama ilivyokuwa Uhuru wa Marekani kutoka Uingereza. Ndiyo unaona Marekani inajiamulia kila jambo lake yenyewe hadi kutafuta na hatimaye kuwa dola kiongozi duniani kwa gharama ya kuyaondoa madola wenzake ya kibepari kama Uingereza nk.
Ulimwengu unahitaji uhuru wa kimfumo, wa madola kuweza kujiamulia mambo yao kwa misingi ya utu, na hili ni kwa kuishi katika mfumo wa Muumba wa Ulimwengu na vilivyomo. Tunahitaji mabadiliko ya fikra ya kiadiolojia na sio kubaki na kujivunia kibwagizo cha uhuru wa bandia.
#UislamuNiUfumbuziSahihi
Hamza S. Sheshe
Maoni hayajaruhusiwa.