Mandela Amekufa na Ndoto Zake !

Nelson Mandela alifariki dunia tarehe 05 Disemba 2013. Mtu aliyekuwa raisi mweusi wa mwanzo ndani ya Afrika Kusini baada ya mapambano makali dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi. Kifo cha Mandela aliyefariki akiwa na umri wa miaka 95 kilipelekea kumiminika rambirambi kutoka mashariki na magharibi zikitoka kwa watu mbalimbali kama viongozi wa jamii, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasiasa zikiwemo rambirambi za madola makubwa ya kibepari, kama zile za aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon akimsifu Nelson Mandela kwamba ni ‘shujaa’, ilhali dola yao ya Uingereza ndio iliyotaka Mandela anyongwe kwa ugaidi katika miaka ya 80’, na yeye David Cameron wakati ule alikuwa miongoni mwa walioendesha kampeni hiyo.

Maisha ya Mandela yamegusa hisia za wengi na amekuzwa mno hususan baada ya kile kinachoitwa kukomesha ubaguzi wa rangi, kuwa raisi wa mwanzo mweusi Afrika Kusini, na kutunukiwa nishani ya Nobeli ya Amani.

Hakuna anayepinga kwamba Mandela alijaribu kujitoa muhanga kupigania ili kukomesha ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Lakini mapambano hayo yalikuwa mapambano duni. Alipigania kuondoa tatizo bila ya kupambana na msingi wa tatizo. Na msingi wa tatizo ni mfumo wa kibepari. Ndio maana watu weusi wale wale aliwaongoza dhidi ya ubaguzi wa rangi wasibaguliwe, tahamaki wamekuwa wakiwabagua waafrika wenzao na kuwafanyia ukatili mkubwa usio na mfano, waafirika ambao baadhi ya nchi zao zilijitolea kwa hali na mali kusaidia mapambano yao.

Matukio ya kibaguzi yalidhihiri wazi wazi tangu zama za uhai wa Mandela, ndani ya mwaka 1994 na 1995 vijana walivunja nyumba za wageni mjini Johannesburg, wakiwataka polisi kuwarejesha raia wahamiaji makwao, mwaka 2008, 2015 matukio ya uvamizi yalijiri tena, na yamekuwa yakiendelea mpaka karibuni katika hali ya aibu na fedheha kubwa kwa nchi inayodaiwa ina kiwango cha hali ya juu cha demokrasia.

Nelson Mandela amekuja kuyaokoa mataifa ya magharibi, mfumo wao wa kibepari na makampuni yao ndani ya Afrika ya Kusini kwa kukubali muwafaka ambao umewabakisha mabepari kuendelea kuwa mabwana, kwa kuinua kijikundi kidogo miongoni mwa watu weusi kwa gharama ya walio wengi ambao wako katika hali duni kama awali au zaidi. Mandela kama walivyo wengi miongoni mwa vibaraka wenzake alitumia njia ya kupambana na tatizo kwa mfumo ule ule ambao ni tatizo. Yaani kunawa tope, kwa kutumia tope, jambo ambalo ni kuupa nguvu mfumo wa kibepari.
http://greenhouse.economics.utah.edu/…/2000-Mar…/016164.html

Nelson Mandela amekufa na kuzikwa, ndoto yake ya kuifanya Afrika ya Kusini bila ya ubaguzi na mahala bora imebwatika kama zilivyobwatika ndoto za vibaraka wengine wa Afrika, baadhi yao wakilingania muungano wa Afrika, ujamaa wa kiafrika nk. Afrika ya Kusini ya leo imejaa kila aina ya majanga kuanzia uhalifu, ubaguzi, ukabila, ukosefu wa ajira, umasikini wa kutupwa nk.

Tiba ya Afrika ya Kusini na ulimwengu jumla ni kuondoa kimsingi (radically) mfumo batil wa kibepari na nidhamu zake za kisiasa, kijamii, kiuchumi nk. kwa kutandika mbadala wa mfumo wa haki na uadilifu, yaani mfumo wa Kiislamu ulioko kando na kila aina ya dhulma na ukandamizaji.
#UislamuNdioUfumbuziSahihi

Risala ya Wiki No. 65
07 Rabi’ al-thani 1441 Hijri 04/12/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.