Subira na Msimamo Wa Zaynab Mbele ya Yazid Mtawala Dhalimu
Ndani ya mwezi wa Muharram ndipo ilipotendwa dhulma kubwa ya kuuwawa kikatili mjukuu, kipenzi cha Mtume SAAW, Imam Hussein bin Ali Ra. akiwa pamoja na kundi la Waislamu waliojumuika naye. Ilitendwa dhulma hiyo kwa amri ya mtawala dhalim Yazid bin Muawiyah.
Kwa munasaba huu ni muhimu kuangazia walau kidogo maisha ya bibi Zaynab bint Ali Ra. Bibi mtukufu, shujaa, jasiri na mcha Mungu ambae alikuwa ndugu wa Imam Hussein Ra. Na isitoshe alikuwa bega kwa bega na kaka yake katika vita vya Karbala vilivyoleta masaibu ya dhulma na ukatili wa kuuwawa kaka yake. Bibi huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wetu SAAW kutokana na bintie Bi Fatma Ra. aliezaliwa katika mwaka wa 6 Hijria akiwa mdogo kwa miaka michache kwa Imamu Hussein Ra. Jina la ‘Zaynab’ alipewa na Mtume SAAW na alibashiriwa kukutwa na mashaka mengi katika maisha yake.
Naam kweli alikutwa na mashaka. Zaynab Ra. aliondokewa na babu yake Mtume SAAW, kisha akafariki mama yake akiwa na umri mdogo, kikafuatia kifo cha baba yake Imam Ali Ra. Aidha, alishuhudia kifo cha kaka yake Imam Hassan Ra. na alishiriki kikamilifu katika mapigano ya Karbala dhidi ya Yazid na kushuhudia kifo cha kaka yake kipenzi Imam Hussein Ra. pamoja na wanawe wawili Muhammad na Aun.
Wakati Imam Hussein alipopanga safari ya kwenda Hijjah kisha kuelekea Kuffah Iraq alijumuika nae bega kwa bega. Bi Zaynab alimuaga mumewe Abdullah (binamu yake) na kufuatana na wanawe wawili Aun na Muhammad katika safari hiyo. Mumewe alihisi uzito juu ya safari akamuhadharisha juu ya mashaka na taabu wanazoweza kukutana nazo.
Zaynab Ra. alijibu kumueleza mumewe: “Kwa miaka khamsini na tano hatujawahi kutengana mimi na kaka yangu (Hussein) , Sasa ni umri wa uzee, ni muda wa kufunga maisha yetu. Ikiwa nitamuacha pekee, basi vipi nitamkabili mama yangu ambae wakati wa kifo chake aliniusia kwa kusema:
‘ Ewe Zaynab , baada ya mimi, kuwa mama na dada wa Hussein ”Ni wajibu kuwa na wewe (mume wangu) , lakini nisipokwenda wakati huu nitashindwa kuhimili kutengana nae”
Zaynab akaruhusiwa na mumewe, akafanya ibada ya Hijja kisha wakafunga safari ya kuelekea Iraq.
Vita viliporipuka alikuwa mstari wa mbele katika mapigano ya Karbala na akashuhudia dhulma na mauwaji aliyofanyiwa kaka yake na Waislamu wengine wakiwemo wanawe wawili wa kiume waliouwawa katika mapigano. Zaynab na Waislamu wengine walichukuliwa mateka na kupelekwa mbele ya mahkama ya Yazid.
Mbele ya qasri yake, Yazid aliwasomea mateka mashairi ya zama za jahilia yaliojaa kejeli ya Uislamu na aya za Allah SW, pia kuwakejeli na kuwacheza shere Waislamu hao.
Bi Zaynab Ra. licha ya kuwa ni mateka mikononi mwa adui aliepoteza jamaa zake wengi wakiwemo kaka na watoto wake katika mapigano hakukhofu alisimama kidete na kumjibu Yazid kwa hotuba ndefu, miongoni mwa maneno yake alimueleza:
“Yazid Umeifikia kiwango hiki kwa sababu ya dhambi nyingi ulizokwisha tenda. Kwa mujibu wa quran, anaeshika njia ya dhambi na kudumu nazo akakanusha aya za Allah na kuzikejeli na mwisho ataingizwa katika adhabu kali”
Zaynab alifariki akiwa na umri karibu wa miaka sitini ndani ya mwaka wa 62 Hijria. Ametuachia mafunzo bora ya subra, ujasiri, mapenzi kwa ndugu, ucha Mungu, na kusimama kidete kuwawajibisha/kuwahisabu watawala madhalimu nk,
Maoni hayajaruhusiwa.