Ya Rabb Mpokee Mursi, Na Muangamize Al-Sisi

بسم الله الرحمن الرحيم

Baada ya mashaka, dhiki, mateso na idhilali ya kuwa mahabusu hatimae Dr. Muhammed Mursi ameungana na wenzake wengi waliodhulumiwa nchini Misri kwa kurudi kwa Mola wake. Inna llilahi wainna ilayhi rajiuun. Allah Sw Awamakinishe kwa subra familia yake, Amsamehe marehemu, Amjazie mapungufu yake na kumuingiza katika pepo ya Firdausi.

Na kwa kuwa Dr. Mursi alikuwa mikononi mwa dhulma mwa utawala dhalimu wa Al-Sisi, hapana shaka utawala huo kamwe hautosafika na damu ya kifo hicho.

Mwendelezo wa dhulma za vibaraka ukiwemo utawala wa Al-Sisi wa Misri hazitokuzwa, kupigiwa debe wala kupazwa sauti sana ulimwenguni, kwa kuwa vibaraka hao ni watumwa waaminifu wa nchi za magharibi wanaowafanyia kazi nzuri mabwana zao hususan Marekani kuzuiya wimbi la Uislamu kushika hatamu za kiutawala.

Utawala wa mabavu wa Misri kuzuiya Umma katika maziko ya Mursi, kuwanyima fursa hata baadhi ya wanafamilia kushiriki mazishi yao ya kiserekali na kutangaza hali ya vitisho kufuatia kifo hiki, si dalili ya nguvu ya utawala huo, bali ni kielelezo cha uwepo wa shaka kubwa katika kifo hicho, mabavu, kutoungwa kwake mkono na Umma. Jambo lenye sura ya wazi juu ya udhaifu wa utawala dhalimu wa Misri.

Kibaraka Al-Sisi kama walivyo vibaraka wengine katika ardhi za Waislamu anaendelea kujigubika nguo dhaifu kama nyumba ya buibui kwa kujidanganya na kujighilibu nafsi yake na utawala wake kwamba ana nguvu.

Tunasema mtawala wa Misri Al-Sisi anajidanganya wazi wazi akidhani kuwa ni mjanja, mwerevu, na mwenye utawala wenye nguvu, tena kwa bahati yumo katika nchi ile ile aliyopita Firaun (laana iwe juu yake) mwenzake aliyejidanganya kama yeye, kwamba mjanja, mwerevu na mwenye maguvu. Tahamaki pale Allah SW alipomtia mkononi hakuwa na pa kukimbilia wala wa kumnusuru, akamdhibiti sawasawa bila yakumponyoka, akaangamizwa na kumwagiwa laana ya milele kwa dhulma na uovu wake.

وَأُتْبِعُوا فِي هَذِهِ لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ بِئْسَ الرِّفْدُ الْمَرْفُودُ (هود: 99).

“Nao wamefuatishiwa (Firaun na wafuasi wake) laana hapa duniani na Siku ya Kiyama. Ni mabaya yaliyoje watakayopewa” (Hud: 99)

Tunamwambia na kumtanabahisha Raisi Al-Sisi wa Misri yaleyale aliyohadharishwa Firaun mwenzake kutoka kwa (kijana katika zama za Fir aun) rajul muumin :

يَاقَوْمِ لَكُمُ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ظَاهِرِينَ فِي الأَرْضِ فَمَنْ يَنصُرُنَا مِنْ بَأْسِ اللَّهِ إِنْ جَاءَنَا ِ (غافر: 29

“Enyi watu wangu ! leo mna utawala mmeshinda katika nchi, basi ni nani atakayenisaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia?”
(Al-Ghaafir : 29)

Tunawafariji tena familia ya marehemu, na Waislamu wa Misri kwa mitihani hii inayotusibu, lakini pia licha ya kurefuka kiza totoro cha dhulma na ukandamizaji tunawapa bishara njema watu wa Misri na Umma wote wa Kiislamu ulimwenguni kote kwa kauli tukufu ya Allah Taala aliposema:

وَنُرِيدُ أَنْ نَمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ (القصص: 5).

“Na tunataka kuwafanyia ihsani waliokandamizwa katika nchi, na kuwafanya wao wawe viongozi, na kuwafanya wao wawe warithi (Al-Qas’as’: 5)

Risala ya Wiki No. 44

15 Shawwal 1440 Hijri /18 Juni 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.