Utawala Bora Upo Katika Khilafah Na Sio Demokrasia
بسم الله الرحمن الرحيم
Leo hii mabepari wakoloni pamoja na vibaraka wao duniani wanataka kuuaminisha ulimwengu kuwa hakuna mfumo wa kiutawala (political system) ambao unaweza kutumika kutawala ulimwenguni kwa haki tofauti na nidhamu yao ya kiutawala ya demokrasia.
Kimsingi, kabla ya ubepari kuanza kutekeleza demokrasia katika Ulaya Magharibi na hatimaye kuutawala ulimwengu kupitia ukoloni mwishoni mwa karne ya 19 na kulazimisha nidhamu hiyo, ulimwengu ulitawaliwa na Uislamu kupitia nidhamu (system) yake ya kiutawala ya Khilafah kwa zaidi ya karne kumi na tatu.
Mfumo wa utawala wa Kiislamu (Khilafah) wenye sura ya kiulimwengu ni mfumo thabiti wenye viwango (quality) vyote halisi vya utawala bora tofauti na mfumo wa utawala wa kibepari (demokrasia) ambao ni ndoto ya kilaghai isiyotekelezeka wala kuingia akilini.
Mfumo wa utawala wa Kiislamu umejengwa juu ya msingi imara ambao ni kitabu cha Mwenyezi Mungu (S.W.T) yaani Quran na ufafanuzi kutoka kwa Mtume Muhamad (S.A.W) yaani Sunnah. Huu ni msingi thabiti usiotetereka ambao sheria zote hutoholewa kutokana na msingi huu, hivyo ni bora kuliko demokrasia ambayo haina msingi wowote wa kiungu isipokuwa hutegemea mawazo ya kibinadamu pekee, na binadamu kimaumbile ni dhaifu hawezi kamwe kwa akili zake tu kutengeneza sheria bora za kumtawala binadamu mwenzake.
Katika Uislamu viongozi wala wanachi hawatungi sharia, bali wananchi huwa na mamlaka ya kumchagua kiongozi atakayewaongoza kupitia msingi tulioutaja, yaani Quran na Sunnah na pia wana uwezo wa kumuwajibisha.
Wananchi chini ya serikali ya Kiislamu ya Khilafah huwa na nguvu ya kumuwajibisha na kumtoa madarakani kiongozi ikibidi kupitia mahakama inayoshughulika kuzuiya dhulma za watawala dhidi ya wananchi ambayo huitwa “Mahkamatul Madhalim”.
Tofauti na demokrasia ambapo kikundi kidogo cha matajiri na makampuni yao ya kibepari ya kinyonyaji ndio huamua nani awe kiongozi, na wananchi hupotezewa muda kupiga kura ambazo hazina athari yoyote katika maamuzi. Amerika ni mfano mzuri katika hili, katika kampeni za uraisi za Barrack Obama mwaka 2012 ziligharimu dolari bilioni moja zilitolewa na matajiri na makampuni yao kama vile Microsoft nk.
Katika mfumo wa utawala wa Kiislamu watu wote wapo chini ya sharia, hakuna mtu aliye juu ya sharia hata kiongozi wa nchi (Khalifah). Amesema Mtume (S.A.W)
“Ummah zilizopita ziliangamizwa kwa sababu walikuwa akiiba mtukufu wao humlinda, na akiiba mtu dhaifu humuadhibu, Wallah! hata kama Fatima mtoto wa Mtume akiiba nitaukata mkono wake”
(Bukhari na Muslim).
Hii ni tofauti kabisa na demokrasia ambapo viongozi huiba bila kuwajibishwa wakati wananchi huendelea kuwa masikini wa kutupa wakitaabishwa na makodi ya kila aina.
Kwa mfano, kampuni kama Acacia ambayo ilikuwa ikidaiwa na serikali zaidi ya trilioni 400 Tsh nchini Tanzania ni kielelezo kizuri cha wizi huu lakini hakuna aliyeiwajibisha, jambo linalodhihirisha uhalisia kuwa matajiri ni tabaka lisiloguswa, na wanasiasa wa kidemokrasia kwa kupatiwa maslahi binafsi huwa tayari kuwalinda.
Katika utawala wa Kiislamu watu wa dini zote, rangi zote, jinsia zote, walemavu na wazima huwa na haki sawa. Amesema Mtume (S.A.W)
“Yeyote atakayemuua asiyekuwa Muislamu (Dhimmiy) bila hatia hataipata hata harufu ya pepo” (Tirmidhi).
Jambo hili ni maarufu katika tareekh, wasiokuwa Waislamu walioishi katka utawala wa Kiislamu (Khilafah) walikuwa wakilindwa na kuamiliwa kwa wema na insafu kiasi kwamba walikuwa wakisaidia Waislamu kupambana na maadui baada ya kuona uadilifu mkubwa wa Uislamu. Mfano mzuri ni ulinzi walioupata mayahudi katika Istanbul katika Khilafah ya Kiuthmani hususan kipindi cha Khalifah Suleyman Al- Qanun (Mtenda Haki).
Uadilifu huu haupatikani hata harufu yake katika tawala za leo hii za kidemokrasia ambapo Waislamu kuanzia katika biladi za Kiislamu na katika nchi za kikafiri wamekuwa wakiteswa, kudhalilishwa hadi kuuliwa bila sababu yeyote.
Aidha, Uislamu unakataza kumkamata mtu au kumzuiya bila ushahidi na marufuku serikali kuchunguza wananchi, na wananchi kuchunguzana wao kwa wao ( spying).. Anasema Allah Taala:
وَلاَ تَجَسَّسُوا
“Na wala msichunguzane” (TMQ 49:12).
Zaidi ya hayo, Uislamu unakataza kutesa watu kwa ajili ya kutafuta ushahidi au vinginevyo. Bali umekataza hata kutesa maiti seuze aliye hai. Mtume SAAW akahadharisha kuwa maiti anasikia maumivu kama aliye hai, hivyo tujiepushe kufanya matendo ya kumpa maumivu.
Hii ni tofauti kabisa na utawala wa kidemokrasia ambapo watu hutekwa, hushikiliwa, hufungwa, huzuiliwa, na hata kuuawa bila ya makosa wala ushahidi wowote. Mfano mzuri ni sheria chafu, ovu ya ugaidi iliyolazimishwa na wakoloni katika nchi changa ambapo imehalalishwa vifo na mateso vya mamilioni ya Waislamu kwa dhulma, chuki na bila ya ushahidi wowote.
Mfumo wa utawala wa Kiislamu ni wa haki, thabiti, wenye uadilifu, na sharia zake hazipitwi na muda wala kuathiriwa na mazingira’
Ni muda muwafaka umefika kwa ulimwengu kutafakari kuhusu utawala huu wa uadilifu ili kuondokana na dhiki, mateso na uonevu ulioletwa na mfumo mbovu wa kidemokrasia usiojali maslahi ya wananchi jumla, bali ni maslahi binafsi ya wanasiasa, familia zao na wapambe zao.
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 99
15 Jumada al-thani 1442 Hijri
28 Januari 2021 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.