Umaskini wa Leo Kwa Kiasi Kikubwa Unatokana na Misingi Miovu ya Nidhamu ya Kiuchumi ya Kibepari
بسم الله الرحمن الرحيم
Sehemu kubwa ya wanaadamu duniani hasa katika nchi zinazoitwa za ulimwengu wa tatu wanakabiliwa na hali duni ya maisha na umasikini mkubwa licha ya kuwepo kwa rasilimali nyingi katika nchi hizi na kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali.
Wakikabiliwa na uhaba au ukosefu wa chakula wa mara kwa mara, uhaba wa maji safi na salama, na makaazi duni, huku wengi wao wakiendelea kuishi kwa kutegemea kipato kidogo cha chini ya wastani wa dola 1.25 kwa siku katika kukidhi mahitaji yao.
Hali hii imeambatana na ukosefu mkubwa wa kazi, ambapo kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kiwango kimefikia watu milioni 470 duniani, na idadi ikiendelea kupanda.
Huku madeni yakiongezeka katika nchi hizi, pengo kati ya matajiri na masikini nalo linaongezeka kwa kasi. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Oxfam kutokea kwenye Mkutano wa Baraza la Uchumi Duniani, World Economic Forum (WEF) uliofanyika Davos, Switzerland hivi karibuni, ‘mabilionea 2,153 wa dunia wanamiliki utajiri wa zaidi ya watu bilioni 4.6 wanaofanya asilimia 60 ya watu wote duniani’.
Hali hii ya kiwango hiki cha umasikini huchangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo mbovu wa kibepari chini ya nidhamu yake ya uchumi ambayo hushughulikia na kuchunguza mambo yahusuyo mada tu (materialistic) na kujengwa juu ya misingi: uhaba wa kukadiria (relative scarcity), thamani ya bidhaa na nidhamu ya bei.
Wanauchumi wa kibepari humchukulia mwanaadamu kuwa ana mahitaji yanayoongezeka kila siku na ambayo huhitajia kutoshelezwa. Ndipo huona kuwa kuna tatizo la uhaba wa rasilimali za kuweza kutosheleza mahitaji hayo yasiokwisha lakini bila ya kutosheleza mahitaji ya kila mtu angalau kwa yale ya lazima. Wameyachukulia mahitaji ya kilazima na ya anasa kuwa yote yanalazimika kutoshelezwa, na hivyo kulifanya suala la uzalishaji wa bidhaa na huduma kuwa ni tatizo la uchumi na ndio suala la kukimbiliwa badala ya kushughulikia zaidi suala la usambazaji ili kuwapatia raia wote mahitaji yao ya kimsingi ambayo ni chakula, mavazi na malazi.
Hivyo suala la ukuzaji wa uchumi jumla wa nchi kwa kipimo cha GDP, ambacho ni kipimo batil kinachogawa tarakimu /nambari badala ya mahitaji kwa watu.
Hali hii ni kinyume na Uislamu ambapo hugawa mahitaji halisi na sio namabari kwa kila raia katika dola, kwa kuhakikishiwa kutoshelezewa mahitaji yake ya msingi kwa kutumia rasilimali zilizopo, kabla ya kutoshelezewa mahitaji ya ziada.
Vile vile mabepari huchukulia suala la ‘thamani’ ya kitu ni yenye kukadiriwa na si kitu halisi, yaani huifanya ni yenye kulinganishwa, na hivyo huwa sio thabiti na ni yenye kubadilika kila mara kulingana na soko lilivyo. Hivyo, hii huwa ni njia ya kupata fedha kutokana na hali ya soko na haitokani na thamani au manufaa yake. halisi. Kimsingi kwa mtazamo wao huo suala la thamani sio sahihi kutoka msingi wake, na ni lenye makosa kwa sababu dhana ya msingi wake ni ya uwongo.
Msingi mwengine wa nidhamu ya kiuchumi ya kibepari ni kile kinachoitwa ‘bei’ (price) ambayo ni uwiano wa kitu kinachobadilishwa na fedha ambapo bidhaa na huduma hutathminiwa kulingana na mahitaji ya watumiaji. Bei huchukuliwa na mabeperi kuwa ndio kipimo, kigezo, kichocheo na muongozaji wa shughuli zote za kiuchumi katika nchi. Mwanauchumi maarufu wa Uingereza wa karne ya 18, Adam Smith na ambae hujulikana kuwa ni ‘Baba’ wa uchumi na ‘Baba’ wa ubepari, ameitaja ‘bei’ katika nadharia yake kuwa ni ‘invisible hand’ akimaanisha ni nguvu isiyoonekana lakini ikiwa ndio inayoendesha, kusimamia na kuongoza uchumi katika njia bora zaidi bila kuingiliwa kati. Bei kwao ndio inayochochea uzalishaji, inayosimamia usambazaji na pia kuweka mizani baina ya uzalishaji na utumiaji.
Mtazamo huu wa mabepari kwa namna unavyoiangalia dhana ya bei ni kinyume na uhalisia na hauko sahihi. Ni mtazamo unaoikosesha jamii kuwa na tabia ya kusaidiana, na kufanya juhudi katika kukuza ustawi wa jamii husika na kuboresha hali za raia katika nchi. Masuala ya uadilifu, ukarimu, shukrani na mfano wake hupuuzwa, au hufanywa kwa namna ya kupata maslahi ya kushikika tu. Kwa kufuatwa dhana hii ya bei, humaanisha kuwa mwanaadamu asiyeweza kuchangia uzalishaji hastahiki kuishi kwa kuwa hastahiki kupata mali ya nchi ambayo ingemtosheleza kukidhi mahitaji yake.
Kwa upande mwengine, wale wenye uwezo mkubwa wa kuchuma na kumiliki huweza kuhodhi na kuwamiliki watumiaji kwa kulazimisha bei wanazotaka. Hivyo, fikra ya kuifanya bei ndio nidhamu pekee ya usambazaji mali, na kuwepo fikra ya uhuru wa kumiliki katika ubepari kumechangia sana kuifanya dunia kuwa ni mahala pa ‘samaki mkubwa kumla mdogo’ na kuwanyima wanaadamu haki yao ya kupata mahitaji ya msingi, na hivyo kuendelea kubaki katika dimbwi kubwa la umasikini.
Hali ya umasikini iliopo leo katika ulimwengu hasa katika nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika inaweza kuepukwa kama ilivyoepukwa wakati ambapo mfumo wa Kiislamu ukifanya kazi. Katika kipindi cha Khilafah ya Umar ibn Abdul Aziz (ra), imepokewa na Yahya bin Said aliyekuwa Wali (Gavana) wakati huo kuwa alisema: “Nilipelekwa na Umar bin Abdul Aziz kukusanya zaka Afrika. Baada ya kukusanya nikakusudia kuwapa watu masikini. Hata hivyo, sikupata yeyote. Umar bin Abdul Aziz amewafanya watu kuwa matajiri wakati huo. Mwishowe nikaamua kutumia mapato ya zaka kuwanunua na kuwaacha huru watumwa”
(Ibn Abd Hakam, Abdullah (1994) Al-Khalifat al-Adil Umar Ibn Abd Aziz.
Bila shaka nidhamu ya uchumi ya Kiislamu chini ya Khilafah ndio pekee inayoweza kutoa hakikisho la maisha bora kwa wanaadamu, wakaepukana na majanga na udhalilifu. Huu ni mfumo uliotoka na kuidhinishwa na Allah SWT, Muumba wetu na Mjuzi wa kila kilicho bora kwa viumbe wake.
Amesema Allah Taala:
أَلاَ يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ (الملك: 14
‘Basi asijue aliyeumba, nae ndie Mjuzi wa siri, Mwenye habari ?’
Habib Abdullah
Risala ya Wiki No. 70
12 Jumada al-thani 1441 Hijri / 06 Februari 2020 Miladi
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.