Ulazima Wa Kuletwa Mitume AS.
بسم الله الرحمن الرحيم
Kipenzi chetu Mtume SAAW alizaliwa katika mwezi huu wa Rabi ul-awwal Mwaka wa Ndovu. Yeye ni Mtume wa mwisho katika silsila ya Mitume wengi As. walioletwa na Allah Ta’ala kuwaongoza wanadamu. Silsila hii ni ndefu na Mitume As. walitumwa katika zama, sehemu na kwa kaumu mbalimbali. Hapana shaka kwamba sheria za Mitume As. hawa zilitofautiana, lakini msingi mkuu wa Tawheed ulikuwa sawa kwa Mitume wote.
Haja au hitajio na ulazima wa kutumwa Mitume As. kwa wanaadamu ni suala la msingi lisilo na mjadala, ili Mitume As. waje kuwaongoza wanaadamu kuendesha maisha yao kwa nidhamu isiyogongana na maumbile yao.
Maumbile ya mwanaadamu yameumbwa yakiambatana na hisia (ghariza) maalumu za ndani za kimaumbile, ikiwemo hisia ya mwanaadamu kutaka kumuabudu/kumnyenyekea Muumba wake, hisia ya kuendeleza maisha, na hisia ya kuendeleza kizazi.
Hisia hizi tatu za kimaumbile zikiambatana na mahitajio ya kibaolojia ya mwanaadamu kuhitajia chakula, maji, hewa nk. ndio mambo makuu yanayofinyanga maisha yote ya wanaadamu wote katika zama zote.
Na hulazimu mwanaadamu awe na utaratibu/ nidhamu na sheria maalumu kumuongoza katika kuyashibisha mambo hayo. Na lau taratibu/nidhamu hizi hazikutokamana kutoka kwa Muumba wa binaadamu huibuka kikundi cha wajanja wachache kuwatungia na kuwatenza nguvu wenzao kuzifuata taratibu zao walizozibuni , au wanaadamu hao wafanye mawafikiano baina yao, au pengine pasiwe na utaratibu wowote kamwe, na kila mwanaadamu atende atakavyo.
Allah Ta’ala kwa Rehma zake na kwa kuwa Yeye ndie Muumba wa mwanaadamu na ulimwengu, katika suala la kutunga taratibu/nidhamu na sheria hizi za kuendesha maisha na kumuongozea mwanaadamu kamwe hakumwaachia mwanaadamu kumtungia mwanaadamu mwengine, wala hakuwaachia wanaadamu walifanye kuwa ni suala la kufanya mawafikiano baina yao, na pia hakuwaachia wanaadamu hawa waishi kama wanyama bila ya utaratibu maalum.
Hii ni kwa sababu kutokana na maumbile ya wanaadamu, kamwe hawatoawafikiana juu ya nidhamu husika na hatimae kutazuka husuma/ugomvi baina yao, zaidi ya hayo utambuzi wa mwanadamu kwa maumbile yake na mazingira yaliyomzunguuka ni finyu kuweza kuunda taratibu/ nidhamu na sheria zitakazokidhi na kumpa utulivu mwanaadamu. Na lau tuseme wanaadamu waachiwe watende watakavyo katika dunia bila ya nidhamu ya maisha, dunia itakuwa kama mbuga ya wanyama au zaidi.
Kwa msingi huu, ndio maana Allah Ta’ala akatuma Mitume As. katika kila zama ili wawe ni daraja la mawasiliano baina yake na wao, kwa Mtume husika kupokea muongozo kutoka kwa Muumba kuja kuwaongoza wanaadamu kwa kuwapa nidhamu za kuendeshea maisha yao, iwe katika ibada, uchumi, siasa, jamii nk.
Mitume As. wote ni kama familia moja, na wakati mwengine Mtume mmoja hubashiri kuja kwa Mtume mwengine baada yake. Zaidi ya hayo Mitume As. hutumwa na miujiza mbali mbali kuwa dalili za utume wao kwa kaumu zao.
Mtume wetu Muhammad SAAW nae ametumwa na miujuiza mbali mbali kama Mitume wengine, na muujiza wake mkubwa wa milele kwa utume wake ni kitabu kitukufu cha Quran. Kitabu chenye kujithibitisha ukweli wake kiakili na kiwahyi kwamba kinatoka kwa Allah Ta’ala, kwa kuwa ni kitabu kilichoteremshwa kwa lugha ya kiarabu, lakini waarabu wenyewe wameshindwa kutoa mithili yake. Na kushindwa kwa waarabu kutoa mithili yake, ni dalili pia ya kutoweza Mtume SAAW kutoa kitabu kama hicho, kwa kuwa na yeye pia ni miongoni mwa waarabu.
Kwa hivyo, hii pekee ni hoja ya kukinaisha akili kuwa Quran Tukufu haikutungwa na waarabu, wala Mtume SAAW, bali ni Wahyi kutoka kwa Allah Ta’ala.
Aidha, na kwa kuwa aliyebalighisha kwetu wahyi huu wa Quran ni Muhammad SAAW, hii pia nayo ni dalili tosha yenye kukinaisha akili kwamba Muhammad SAAW ni Mtume. Kwa kuwa, habalighishi wahyi kutoka kwa Allah Ta’ala, ila mtu huyo huwa ni Mtume na si mwengineo.
Utume wa Mtume SAAW ndio wa mwisho na hakuna Mtume mwengine baada yake, na risala yake ni risala ya kilimwengu na kwa watu wote. Yeye alibeba jukumu lake kikamilifu kwa muhanga na kujitolea upeo wa kujitolea kuwaongoza na kuwasimamia wanaadamu katika upande wa ibada, masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi nk. Kwa kuwa Yeye SAAW licha ya Utume wake, pia alikuwa mtawala na kiongozi wa dola ya Kiislamu. Baada ya kufariki kwake, hapana shaka yoyote mlango wa utume umekwishafungwa, lakini jukumu la kusimamia Umma kwa muongozo aliotuachia kupitia Quran na Sunnah zake liliendelezwa.
Na Waislamu zama zote kutokana na ufahamu thabiti waliokuwa nao walikuwa wakichagua Makhalifa kubeba jukumu hilo kwa niaba yao, kwa kuwa walifahamu kwamba makhalifa pekee ndio wenye haki ya kisheria kusimamia utawala, sheria na nidhamu ya Kiislamu katika kila kipengee cha maisha.
Kwa bahati mbaya, maadui wa Uislamu kwa kutumia vibaraka wa kiarabu na kiuturuki walifanikiwa kuiangusha dola ya mwisho ya Kiislamu ya (Khilafah Uthmania) ndani ya mwaka wa 1924, na tangu wakati huo Umma wa Kiislamu umesambaratishwa katika kila kipengee, na cha hatari zaidi ni kufanyiwa uvamizi katika thaqafa yake kwa kuundiwa ufahamu ulio kinyume na Uislamu wao ili kupotoa na kuharibu haiba ya Uislamu na Waislamu.
Leo wakati tukiyakumbuka mazazi/uzawa wa Mtume wetu Mtukufu SAAW, ni wajibu pia tutambue kwa dhati kwamba tunakabiliwa na vita vya hatari mno vya kuharibiwa thaqafa / mafunzo ya Uislamu wetu kwa kupandikiziwa fikra mbali mbali chafu kama kuharibiwa haiba ya Mtume SAAW, kupakwa matope vazi la hijabu, fikra ya dini mseto, kuoneshwa Uislamu dini ya kikatili nk.
Katika hali kama hiyo ni wajibu kujifunga kwa kuijua thaqafa yetu vilivyo na kuilinda kwa gharama yoyote.
Risala ya Wiki No. 115
23 Rabi ul awwal 1443 Hijri / 30 Oktoba 2021 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.