Ukiritimba Wa Kisiasa Katika Vifaa Vya Ujenzi Zanzibar: Pigo Jengine Kwa Walalahoi

بسم الله الرحمن الرحيم

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Karibuni serikali ya Zanzibar imepiga marufuku usafirishaji na matumizi ya mawe katika shughuli za ujenzi
Katazo hilo lilitolewa na Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Hassan Shaibu Kaduara, akitilia mkazo kwamba uamuzi wa kuzuiya matumizi ya rasilmali ya mawe umefikiwa kutokana na uharibifu wa mazingira unaoendelea.
Waziri huyo alidai kuwa serikali imekua ikipokea malalamiko mengi kuhusu uharibifu wa mazingira kutoka kwa wananchi (bila ya waziri huyo kutaja wananchi gani na wa wapi) kutokana na uchimbaji wa rasilimali ya mawe, na kuwaagiza wananachi kutumia matofali badala ya mawe katika ujenzi wao wa misingi ya nyumba katika kipindi chote cha katazo hilo.
Agizo la serikali ya Zanzibar la kutumia matofali ya saruji badala ya mawe katika ujenzi wa misingi ya nyumba ni dharau kwa wananchi, kwa kuwa serikali inajua kwa yakini kwamba bei ya matofali imepaa sana kutokana na hatua yao (serikali) kama hiyo ya awali ya mwaka 2017 ya kuingiza siasa katika suala la uchimbaji wa mchanga. Hali iliyopelekea kupanda bei ya mchanga katika hali ya kutisha.
Uzoefu unaonesha wazi kwamba pale serikali inapoingiza mkono wa kisiasa moja kwa moja katika vifaa msingi vya ujenzi huibuka uhaba wa bandia, kupaa bei, kuleta taharuki katika sekta ya ujenzi na kusababisha mzigo usiobebeka katika ujenzi hususan kwa mwananchi wa kawaida.
Mkono wa sasa wa kisiasa katika matumizi na uchimbaji wa mawe hauna tofauti na mkono wa awali wa kisiasa katika suala la mchanga. Uingiliaji kati wa kisiasa katika yote haya mambo mawili (mchanga na mawe) unaashiria uwepo wa nia ovu ya serikali ili kuhodhi na ukusanyaji wa maslahi kunufaisha wanasiasa na wapambe wao kwa gharama ya maumivu ya bei ya juu kwa walalahoi.
Ndani ya mwaka 2017 (baada ya serikali kuingilia katika suala la mchanga) ilitamkwa na serikali kwamba Zanzibar ilikuwa imebakiwa na hekta 14 tu za mchanga ilhali sekta ya ujenzi Zanzibar hutumia zaidi ya hekta 10 za mchanga kwa mwaka.
Swala la kujiuliza hapa, jee tangu mwaka 2017 mpaka sasa hizo hekta 14 za mchanga bado zipo au zimekwisha? Kwa sababu watu bado wanaendelea na shughuli za ujenzi.
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba badala ya serikali ya Zanzibar kurahisisha mambo na kutengeneza mazingira ya kuhamasisha yatakayowawezesha raia kumiliki nyumba zao, badala yake serikali naligeuza suala la upatikanaji wa mchanga na mawe kuwa mitaji mikubwa ya kibiashara, wakidandia visingizio vya uwongo vya “ uhaba wa mchanga’ ‘uharibifu wa mazingira’, bila ya kusahau kisingizio kiovu zaidi cha ‘kulinda maeneo ya uwekezaji’,kisingizio ambacho serikali inaendelea kufanya dhulma ya wazi ya kupora maeneo na viwanja vya wananchi wanyonge wahitaji katika maeneo kama Bweleo na Fumba (wilaya ya Magharibi B’ mkoa wa Mjini Magharibi). Ardhi ambazo wananchi walizifufua na kuziendeleza kwa kiwango kikubwa cha gharama ya fedha, wakati na jasho.
Kufuatia jambo hili sisi 𝐇𝐢𝐳𝐛 𝐮𝐭 𝐓𝐚𝐡𝐫𝐢𝐫 𝐓𝐚𝐧𝐳𝐚𝐧𝐢𝐚 tungependa kueleza nukta tatu zifuatazo:
a. Kwa ikhlasi kabisa tunaionya serikali ya Zanzibar ijiepusha kuivurugavuruga zaidi sekta ya ujenzi na kumtia dhiki zaidi mwananchi wa kawaida hususan katika jitihada yake ya kumiliki makaazi yake. Kuingiza uzito na dhiki kwa raia na katika maisha yao ni jambo la dhulma na khiyana ambayo itaadhibiwa vikali na Allah Taala kesho akhera. Pia wenye kuitenda dhulma na khiyana hiyo watatiliwa uzito katika mambo yao hapa hapa duniani.
Imepokewa kutoka kwa Mama Aisha (ra) kwa kusema: akiwa nyumbani kwake amemsikia Mtume SAAW akiomba dua hii:
«اللَّهُمَّ مَنْ وَلِيَ مِنْ أَمْرِ أُمَّتِي شَيْئًا فَشَقَّ عَلَيْهِمْ فَاشْقُقْ عَلَيْهِ وَمَنْ وَلِيَ مِنْ أَمْرِ أُمَّتِي شَيْئًا فَرَفَقَ بِهِمْ فَارْفُقْ بِهِ»
“Ewe Mola wangu, yoyote anayetawalia mambo ya Umma wangu na akawa anawatia dhiki, basi nae mtie katika dhiki. Na yoyote anayetawalia mambo ya Umma wangu akawa mpole kwao, basi Nawe kuwa mpole kwake”. (Muslim)
b. Dhulma hizi zinaibuka kutokana na maumbile ya mfumo wa kibepari na serikali zake za kidemokrasia ulimwenguni kote. Mfumo huu hulaghai kwamba upo kutumikia watu, bali katika uhalisia wake upo kujikusanyia maslahi kwa migongo ya watu.
Hii ina maana kwamba ubepari umekosa uhalali wa kutawalia ubinadamu, kwa kuwa ni mfumo wa jambo moja tu, nalo ni kujikusanyia maslahi kwa gharama yoyote hata kama ni kuleta madhara kwa raia.
c. Ni dola ya Khilafah Rashidah pekee (inayopaswa kuanzia katika ulimwengu wa Kiislamu) ndio ina kila sifa katika kusimamia uadilifu, heshima na kuutumikia ubinadamu kwa uadilifu bila ya kuzingatia rangi za watu, dini zao au jamii wanazotokana nazo.

 

KUMB: 1446 / 04 Jumapili, 24th Rabi’ II 1446 H 27/10/2024 M

Maoni hayajaruhusiwa.