Ubepari Unavyoutaabisha Ulimwengu wa Tatu Katika Uchumi

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Moja kati ya ya nguzo iliyojengwa nidhamu ya uchumi wa kibepari ni nadharia ya uhaba wa rasilmali (scarcity of resources), yaani uchache wa bidhaa na huduma, nayo ni kuwa haiwezekani kushibisha mahitaji na huduma zinazohitajika.

Dhana hii imetokana na ufahamu wa kimakosa ambao mfumo wa kirasilimali/ kibepari umejengwa juu yake nao ni kutenganisha dini na maisha (secularism), msingi unaomwekea mipaka Mola juu ya viumbe vyake alivyoviumba.

Pia wao wanazingatia kuwa haja za binadamu ni haja nyingi zisizoweza kudhibitika na wakafanya njia ya kupata bidhaa na huduma hizi ni pesa pekee yake. Pia hawakutenganisha baina ya uzalishaji na ugavi, licha ya kuwa mawili hayo kuna tofauti kubwa baina yake.

Zaidi ya hayo wanafikra katika nidhamu ya uchumi wa kirasilimali huona kuwa thamani (bei) ya kitu ndio njia pekee ya kuwawezesha watu kupata huduma kama vile chakula na bidhaa nyingine za msingi kwa maisha yao ya kila siku.

Hivyo, ndani ya ubepari njia pekee ya kupata bidhaa na huduma kama chakula nk. ni uwezo wa kumilki pesa kiasi kwamba wapo tayari kumwaga chakula ila kisiingie kwenye mzunguko wa watu kwa kukipata bure na kuathiri bei ya bidhaa kama inavyofanya Marekani na Canada, hapo ndiyo utafahamu maana ya kauli ya mwanauchumi maarufu wa kibepari, Adam Smith aliposema : ‘Hakuna mlo wa bure’

Amma kuhusu suala la uchache wa bidhaa na huduma, dhana hii haikuzingatia uhalisia wa mambo kwa kushindwa kutenganisha baina ya haja za msingi za binadamu (basic needs) na haja zisizo za msingi.

Katika maisha anayoishi binadamu haja zake ni aina mbili pekee, nazo ni haja za msingi kama vile chakula, maji, makaazi na mavazi. Mahitajio haya ya msingi pindi mwanadamu anapoyakosa hawezi kubakia kwani kila mwanadamu anahitaji chakula, maji, mavazi na makazi kwa ajili ya kuendesha mahitaji yake ya kila siku, lakini je maji yawe ya baridi au ya moto hili linaingia kwenye haja za anasa ambazo mwanadamu hata kama akiishi bila maji ya baridi au kula chakula kizuri chenye gharama kubwa bado anaweza kuendelea kuishi bila shida yoyote.

Pia wanafikra katika mfumo wa kibepari hawakutofautisha kati ya uzalishaji wa bidhaa na huduma, bali wao wamefanya uzalishaji na ugavi ni kitu kimoja licha ya kuwa kila kipengele kinajitegemea. Kwa mfano, kuzidisha uzalishaji wa bidhaa na huduma na kuzifanya kupatikana kwa wingi katika soko imma kwa kutumia zana za kisasa za uzalishaji kama vile mbegu bora, mbolea inayofaa kwa ardhi husika au machine za kisasa zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa nyingi kwa haraka, kama vile mashine za uzalishaji wa nguo, mashine za kuvuna na kuhifadhi chakula na mazao na yanayohusiana na yote haya huingia katika fani ya elimu ya uchumi ambayo fani hii ni ya kiulimwengu huchukuliwa kutoka kokote sawasawa imetoka kwa Muislamu au kwa asiye kuwa Muislamu.

Amma ugavi wa bidhaa na huduma (distribution) kwa kila mmoja ndani ya jamii hili hutatuliwa kwa nidhamu ya kiuchumi (economic system) nazo ni fikra na hukumu zinazohusiana na kufahamu waqiah (reality) na jinsi ya kutatua tatizo kwa kulisoma na kulifahamu na kulitatua. Hivyo, ni lazima nidhamu hii itokane na mwelekeo maalum wa Umma kwani hufangamanishwa na itikadi ya Umma.

Mchanganyo huu baina ya elimu ya uchumi na nidhamu ya uchumi katika mfumo wa kibepari ndio huzalisha matatizo kila kukicha na kuufanya ulimwengu kupita kwenye matatizo ya mara kwa mara, kwani wao huona kwamba kuzidisha uzalishaji na kuongezeka bidhaa katika soko ndio njia pekee ya kutatua tatizo la uchumi kwa kuzingatia kuwa muhimu ni kushibisha haja za watu jumla na sio mtu mmoja mmoja.

Nadharia hii mbovu ndio iliyopelekea baadhi ya wanafikra katika nidhamu ya kirasilimali kukiri uozo huo, Profesa Benard Shaw aliwahi kusema:
“Nidhamu hii ya uchumi ya kibepari…. ina pupa katika uzalishaji na nidhamu mbaya kwenye ugavi”

Kutokana na nadharia hiyo ya kimakosa imepelekea kuwepo kwa pupa kubwa katika uzalishaji wa bidhaa na huduma katika ulimwengu na mfumo mbovu wa ugavi.
Nadharia hii ndio imepelekea kundi la watu wachache kumiliki rasilimali nyingi na kuwaacha watu wengi wakiwa hawawezi kunufaika na rasilimali, licha ya kuwepo rasilimali za kutosha hasa katika bara la Afrika, lakini bado watu wake hufa na njaa kila siku na watoto wadogo kukabiliwa na tatizo la utapia mlo kwa kukosa chakula kutokana na sera mbovu za ardhi.

katika repoti iliyotolewa na Mo Ibrahim Foundation ya mwaka 2018 inaonesha kuwa zaidi ya aslimia 79 ya ardhi safi ya kilimo ndani ya bara la Afrika haijalimwa ambayo ni sawa na asilimia 60 ya ardhi yote duniani huku hekari zaidi ya milioni 60 za ardhi walipewa au zilinunuliwa na watu kutoka nje mwaka 2009. Na asilimia 80 ya wakulima wadogo wakimiliki chini ya hekari 2 ya ardhi kwa wastani. Pia theluthi mbili za nchi za Afrika zinaagiza chakula kutoka nje.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 925 wanakabiliwa na njaa duniani kote, idadi ambayo ni sawa na wakaazi wote wa Afrika, huku watu zaidi ya 240 wapo Kusini mwa jangwa la Sahara. Aidha, watoto zaidi ya milioni 5 hufa duniani kote kwa kukosa lishe, na mtu mmoja kati ya watu saba hufa kwa njaa duniani, wengi wao ni kutoka bara la Afrika.

Ripoti ilionesha zaidi kuwa nchi zilizoathirika zaidi ni Burundi, Chad, DRC, Eritrea Madagasca na Malawi (African Agriculture- Mo Ibrahim Foundation).

Kutokana na hali hiyo nchi za Afrika zimeshauriwa kuthibiti ongezeko la watu ili kuendana na malengo ya millennium .Huo ndio ubepari uligeuza dunia kuwa sehemu mbaya ya kuishi binadamu licha ya rasilimali za kutosha zilizipo duniani.

Amma katika upande wa mfumo wa Kiislamu sera zake za uchumi ni tofauti na mfumo wa kibepari, zimetokana na msingi wa uwepo wa Muumba, Mola ambaye kabla ya kuumba ulimwengu huu alikadiria rasilimali (zitakazowatosha wanadamu watakaoishi katika mgongo wa ardhi.

وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ مِنْ فَوْقِهَا وَبَارَكَ فِيهَا وَقَدَّرَ فِيهَا أَقْوَاتَهَا فِي أَرْبَعَةِ أَيَّامٍ سَوَاءً لِلسَّائِلِينَ (فصلت: 10).

“Na akajaalia juu yake milima na ikaibariki na akakadiria ndani yake (ardhi) chakula chake, sawa sawa kwa wenye kuuliza.”

Hivyo kabla ya kuwepo duniani, Mola tayari ameshakadiria riziki kwa wanadamu wote kiasi kwamba ameweka riziki kwa kila kiumbe katika mgongo wa ardhi.

Hivyo, nidhamu ya kiuchumi wa Kiislamu daima inalenga kudhamini kushibisha mahitajio ya msingi ya mwanadamu mmoja mmoja na pia kumwezesha kushibisha haja zake za ziada/ anasa kwa kadri awezavyo. Kwa msingi nidhamu ya uchumi ya Kiislamu haipimi kwa kuangalia uchumi kijumla jumla kwa kuangalia nchi bali hupimwa kwa kuangalia mtu mmoja mmoja kwa kumdhaminia kupata mahitajio yake ya msingi kama vile chakula, mavazi na makazi mazuri na kumwezesha kupata mahitajio yake ya ziada.

Pia Uislamu umeweka sera nzuri za kumiliki kama vile mali za Umma, mali za serikali na mali za mtu binafsi. Kwa upande mwengine pia kuna sera ya ardhi kwa kumfanya kila mtu aweze kunufaika nayo, imeruhusu mtu kumiliki ardhi maiti na ikawa yake kama alivyosisitiza Mtume saw, kuwa mwenye kuhuisha ardhi basi ni ya kwake.

Pia Uislamu ukakataza kukodisha ardhi kwa ajili ya ukulima, akafundisha Mtume SAAW kwamba yeyote mwenye kumiliki ardhi basi ailime au ampatie ndugu yake, hivyo, imekatazwa mtu kumiliki ardhi pasina kuindeleza kama ilivyokuwa leo.

Pia Uislamu umeweka uwajibu wa kila mwanamume mwenye uweza kufanya kazi kwa ajili ya kukidhi mahitahi yake na ya familia yake. Mtume SAAW Siku moja alipeana mkono na sahaba mkumbwa Saad bin Muuadh akaona mikono yake imekuwa migumu, Mtume SAAW akamuuliza kwanini iko hivyo, Saad akajibu ninachimba sehemu ngumu kwa ajili ya kupata rizk ya kulisha familia yangu.

Mtume SAAW akaibusu mikono yake, kisha akasema vitanga viwili anavyovipenda Mola mtukufu.

Pia imepokewa kutoka kwa Umar ra. kuwa alipita kwa watu wakisoma akawaona wameketi wakiinamisha vichwa vyao akauliza wakina nani hawa, akaambiwa hawa ni watu wenye kumtegemea Mola wao. Akasema hapana, hawa ni wavivu wanakula mali za watu pasina jasho, je nikujulisheni watu wenye kumtegemea Mwenyezimungu ? wakasema ndio, Umar akasema ni Yule ambaye analima ardhi kisha anapanda mbegu kisha anamtegemea Mola wake mtukufu.

Pia Uislamu ukafaradhisha matumizi ya familia juu ya baba mzazi kwa watoto na mama.

وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ لاَ تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلاَّ وُسْعَهَا (البقرة: 233

“Na ni ni juu ya baba (watoto) chakula cha mama na watoto na nguo zao kwa sheria wala nafsi hailazimishwi isipokuwa kwa kadri inavyoweza”

Uislamu pia umefaradhisha juu ya dola ( baitul mal) kutoa matumizi ikiwa kuna watu ambao hawana uwezo au wa kuwasimamia.

Uislamu umehimiza kila mmmoja kuchuma kwa njia ya kisheria na kunufaika na rasilimali ambazo wamezichuma ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanafikiwa katika nchi kwa kuhakikisha kila mtu mmoja mmoja kushibisha haja zake za msingi na kumwezesha kushibisha haja zake za ziada (anasa)

Pia swala la kushibisha mahitajio ya msingi Uislamu umelifanya na jukumu la kusimamiwa na dola, yaani Khalifah kupitia (baitul mal) kwa ajili ya raia wote wasio na uwezo, wawe Waislamu au wasiokuwa Waislamu (dhimiyy). Katika Hadithi aliyoipokea Bukhary, Mtume SAAW kasema:

“kiongozi juu ya watu ni mchunga na ataulizwa juu ya kile alichokichunga”na pia akasema yeyote atakayepewa dhamana na Mwenyezimungu ya kusimamia katika mambo ya Waislamu akawa ni kikwazo (kizuizi) cha kutatua shida za watu wahitaji wao na mafukara wao basi Mwenyezi Mungu atamwekea pazia katika shida zake na haja zake na uhitaji wake.

Ust. Issa Nassib

#UislamuNdioUfumbuziSahihi

Risala ya Wiki No. 70
28 Jumada al-thani 1441 Hijri / 22 Februari 2020 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.