Tuyatumie Vyema Masiku Kumi ya Mwanzo za Dhul Hijja

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Tumo katika masiku kumi matukufu ya mwanzo za mwezi wa Dhul Hija. Mwezi ambao ni miongoni mwa miezi mitukufu kabisa. Anasema Allah SW kuwa:
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنْفُسَكُمْ 36
“Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo minne mitukufu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo” (At-Tawba 9:36)
Siku kumi za mwanzo za mwezi wa Dhul Hija, yaani kumi la mwanzo lina fadhila nyingi sana. Kando na kuwa, siku hizo zimo ndani ya mwezi mtukufu wa Dhul-Hijja, kisha zikaongezwa utukufu na kheri kubwa kwa kuteuliwa kwa cheo ziada na Muumba Allah Taala.
Allah Taala kaziapia siku hizo kutokana na taadhima na umuhimu wake, kwa kusema katika Qur-aan:
((وَالْفَجْرِ وَلَيَالٍ عَشْرٍ))
‘Naapa kwa Alfajiri. Na kwa masiku kumi’ [Al-Fajr: 1-2]
Wanachuoni wafasiri wa Qur-aan wamekubaliana kwamba zilokusudiwa hapo ni siku kumi za Dhul-Hijjah.
Pia masiku hayo yameitwa kuwa ni siku za manufaa na kumdhukuru Allah SWT:
لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ
“Ili (watu) washuhudie manufaa yao na kulitaja Jina la Allah katika siku zinazojulikana” [Al-Hajj: 28]
Ibn ‘Abbaas (ra.) kasema: “Hizo ni siku kumi za Dhul-Hijjah.” Na akasema: “manufaa (hapo ni) ya dunia hii na ya Akhirah.” Manufaa ya Akhirah yanajumuisha kupata radhi za Allah Taala. Na Manufaa ya dunia ni vitu vya dunia yanajumuisha wanyama wa kuchinjwa na biashara.
[Tafsiyr Ibn Kathiyr]
Na akatusisitiza Mtume SAW kuhusu fadhila za masiku hayo, kwa kutokana na Ibn Abbas (ra.) kasema, “Kasema Mtume Sallallahu Alayhi Wassallam:
مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ)) يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ قَاُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟ قَالَ: ((وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْ)) البخاري
“Hakuna siku ambazo vitendo vyema vinapendwa (zaidi) na Mwenyezi Mungu, kama siku hizi kumi (za mwanzo za Dhul Hijja). Masahaba wakamuuliza Mtume Sallallahu Alayhi Wassallam:
“Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hata (zaidi ya) Jihad kwa ajili ya Mwenyezi Mungu?” Mtume SAAW akajibu akasema: “(Ndio) hata Jihad kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa mtu aliyetoka yeye na mali yake, na wala asirudi yeye na wala mali yake (yaani akafia huko)”.
[Al-Bukhaariy]
Wakati tukiwa katika masiku haya matukufu lazima tuelewe kwa kina juu ya hali mbaya ya Umma wetu ambapo leo damu tukufu ya Ummah wetu imekuwa kitu duni, inamwagwa hata na waliodhaifu kabisa, matukufu yetu kama Quran, Mtume SAAW , misikiti mitukufu yanadalilishwa, rasilmali zetu zinaporwa na maadui makafiri wakoloni, huku wazazi na watoto wetu wakifa kwa njaa na kukabiliwa na kila aina ya majanga na misiba, licha ya rasilmali nyingi katika nchi za Waislamu ambazo kwa bahati mbaya zinaporwa na mabepari kwa msaada wa mikono ya vibaraka waovu.
Aidha, kwa kupitia propaganda chafu dhidi ya Uislamu yaani vita vya ugaidi, wakoloni wamehalalisha mateso, mauaji na dhulma kwa Waislamu duniani. Wakiyafanya hayo kwa kulazimisha nchi changa zijumuike nao.
Maelfu ya Waislamu wameuawa, kuteswa, wako vizuizini kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi. Wakoloni na mawakala wao wanaotawala biladi za Kiislamu kwa niaba yao wamewaweka mahabusu Waislamu wengi kwa kuwabambikia kesi za uwongo za ugaidi. Kwa vile kesi nyingi za ugaidi huwa ni jambo lisilo na uhalisia, basi hukosa ushahidi, na hivyo ndugu zetu huendelea kusota katika mahabusu kwa miaka kwa kisingizio cha kutokamilika ushahidi kama inavyojidhihirisha pia hapa Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.
Hivyo, katika masiku haya kumi matukufu ambayo huwa tunajifunga kutenda amali mbalimbali njema kama kumdhukuru mno Allah (Subhaanah wa Ta’alaa) kwa kukumbuka neema, kufunga ikiwemo Arafa, kutoa swadaka, kusoma Quran, kuleta istighfar, kaumrisha mema na kukataza mabaya nk.
Pia tusisahau kuomba dua zaidi na kufanya jitihada kuikomboa hali mbaya ya Umma wetu mtukufu ambayo ni ya kusikitisha na kuhuzunisha kwa kuwa bado umezingirwa na dhulma kubwa isiyoelezeka.
Hivyo, ni wajibu kwa Ummah huu mtukufu kufanya kazi kivitendo usiku na mchana kuleta suluhisho la kudumu la uovu na dhuluma zinazotusibu kwa kupatikana utawala wa Kiislamu wa kiulimwengu (Khilifah) kwa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu kisha kuenea kila mahala mashariki na magharibi.
Utawala huo ndio utakaotetea kikweli na kulinda damu, heshima, hadhi ya Uislamu, Waislamu, na wanadamu wote kiujumla, kwani haukuwa huu Uislamu ila ni rahma kwa ulimwengu na walimwengu wote.
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 138
29 Dhu al-Qi’dah 1443 Hijria / 28 Juni 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
#WahyiChimbukoLaThaqafahYetu
#KataaUislamMamboleo

Maoni hayajaruhusiwa.