Tupatilize Fursa ya Sha’aban

بسم الله الرحمن الرحيم

Katika mwezi kama huu wa Shaaban Mtume SAAW alikuwa akikithirisha sana ibada. Alipoulizwa na Swahaba wake Usama bin Zaid (ra) juu ya sababu ya kufunga sana katika mwezi huu alijibu:

((ذاك شهر تغفل الناس فيه عنه، بين رجب ورمضان، وهو شهر ترفع فيه الأعمال إلى رب العالمين، وأحب أن يرفع عملي وأنا صائم))
“Shaaban ni mwezi ambao watu wameghafilika nao, upo kati ya Rajab na Ramadhan, nao ni mwezi ambao amali hupandishwa kwa Mola wa Ulimwengu, na mimi napenda amali zangu zipandishwe na hali ya kuwa nimefunga.
(An-nasai)

Vile vile Mtume saw amesema: “Ibada wakati wa matatizo (fitnah) ni kama Hijra…” (Muslim)

Hadithi kama hizi zinatuonyesha umuhimu wa Waislamu kujifunga katika kutenda amali njema wakati wote bila ya kughafilika katika kipindi au muda fulani.
Uislam ni mfumo kamili wa maisha ya mwanaadamu na kwa kipindi chote cha maisha yetu tunatakiwa tuishi chini kwa mujibu wa mfumo huo.

Hata hivyo, kwa kuwa mwanaadamu hutokea kukabiliana na mazingira tofauti katika mzunguko wa maisha yake ambayo huweza kumpelekea kughafilika na baadhi ya mambo. Katika hali kama hiyo ndipo Mtume SAAW anatuzindua na kutuhimiza kutopunguza kasi ya kutenda matendo mema katika hali ambazo aghlabu ya watu hufadhaika, kuchanganyikiwa au kusahau yaliyo muhimu zaidi katika Uislamu wetu.

Masoud Msellem
18/03/2022

Maoni hayajaruhusiwa.