Tuirejesheni Nuru ya Mtume (Saaw) Kuukomboa Ulimwengu

Muhammad SAAW ni Mtume wa Allah swt aliyetumwa kwa ulimwengu mzima ili kuufikisha / kubalighisha ujumbe wa Uislamu  kwa kupanga mahusiano baina ya mtu na Muumba wake, mtu na nafsi yake, na mtu na mtu (maingiliano ya kiuchumi, kijamii, kisiasa nk.  Mfumo aliokuja nao ni kwa lengo la kuutawalia ulimwengu.
Uzawa wa Mtume Muhamad saw ni bishara ya mabadiliko na mageuzi msingi na nuru ya kimfumo. Nuru hiyo haikuangaza Bara Arabu pekee bali ilikuwa ni mabadilko yaliyoanzia tu Bara arabu na kuenea ulimwengu mzima.

Kabla ya kuja kwake Mtume Muhammad saw palikuwapo na Mitume As wengi waliomtangulia, nao walifanya kazi kama aliyoifanya Mtume wetu saaw licha ya kuwa kazi yao ya kufikisha ujumbe wa Allah sw ilikuwa imefungika na sehemu maalumu na jamii ya watu maalumu. Ila Mtume wetu saw alitumwa kwa watu wote.

Amesema Allah Taala :

إِنْ هُوَ إِلاَّ ذِكْرٌ لِلْعَالَمِينَ (التكوير: 27).

‘Haikuwa hii Quran isipokuwa ni ukumbusho/zinduo kwa ulimwengu wote.

Hii inatupa picha ya pekee na ya aina yake kwamba ujumbe aliopewa Mtume wetu SAAW licha ya kuwa baada ya kuondoka Mitume hao As na muda wao kumalizika, wafuasi wao walinajisi na kuharibu miongozo waliyokuja nayo mitume wao na kuipotosha dini waliyoamrishwa kuifuata na Mitume wao As. Kwa hivyo, mpaka Mtume saw anapewa wahyi hapakuwepo na itikadi/ dini au mfumo sahihi wenye kumkomboa mwanadamu licha ya kuwa baadhi ya dini kama ukristo na uyahudi wakijinasibisha na mwongozo ambao tayari ulikuwa umeharibiwa. Hivyo, nao walihitaji mwongozo sahihi ambao utawaondolea shaka na mazonge ambayo tayari walikuwa nayo katika dini zao, nao si mwingine bali ni mwongozo wa Mtume Muhammad saw.

Amesema Allah Taala :

لَمْ يَكُنِ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ مُنفَكِّينَ حَتَّى تَأْتِيَهُمُ الْبَيِّنَةُ (البينة: 1)

‘Hawakuwaacha kuendelea kwenye shaka makafiri wa ahlu al kitaab ( wakristo na mayahudi) mpaka wafikiwe na ubainifu

رَسُولٌ مِنَ اللَّهِ يَتْلُوا صُحُفًا مُطَهَّرَةً (البينة: 2

Mtume kutoka kwa Allah akiwasomea swahifa tukufu’

Hivyo, wale waliokuwa na kitabu kabla ya kuja kwake Mtume SAAW nao pia walikuwa na shauku ya kupata mwongozo utakaondoa sintofahamu nyingi baina yao kama ilivyokuja katika mamia ya aya ndani ya Quran tukufu licha ya kuwa kwa upande wa Ahlu kitab wao walikuwa tayari wana  ufahamu fulani  juu ya ujio wa utume wa Muhammad saw

Amesema Allah sw :

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِنْدَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ يَأْمُرُهُمْ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنْ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمْ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمْ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالأَغْلاَلَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ أُوْلَئِكَ هُمْ الْمُفْلِحُونَ (الأعراف: 157

‘Wale ambao wanamfuata Mtume nabii (Muhammad)asiyejua kusoma wala kuandika, Mtume ambaye wanamwona ameandikwa kwao kwenye taurati na injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya na kuwaondolea mizigo yao na minyororo yao (sheria ngumu na mila za kikafiri kama utawa nk) basi wale waliomwamini yeye na kumheshimu na kumsaidia na kuifuata nuru iliyoteremshwa pamoja na yeye hao ndio wenye kufaulu.’

Huo ni kwa upande wa Ahlu kitab (mayahudi na wakristo). Amma kwa upande wa jamii ambayo ni mushrikina wao hawakuwa na mwongozo wowote kutoka kwa Muumba, hivyo walikuwa wakiishi maisha duni zaidi ya wanyama.

Walikuwa wakiabudu masanamu kiasi kwamba ndani ya kaaba kulikuwa na zaidi ya masanamu 360, hii inamaana kila sanamu lilikuwa na kazi yake kwa takriban mwaka mzima katika maisha yao ya kila siku, hata kama mtu akitaka kusafiri basi kulikuwa kuna mungu maalumu wa safari.

Kwa upande wa nidhamu ya kiuchumi, masikini akinyonywa na akipokonywa hata chake kidogo alichonacho, watu wachache ndio waliokuwa wakimiliki mali na wala hawakuwa wakiitoa kwa masikini kama sadaka na zakka.

Wanawake pia walikuwa ni watu duni, hawakuruhusiwa kurithi, wakizuiwa kumilki mali hata kama ni mali ya mume wake aliyekufa na kumzalia watoto, kama ilivyokuja katika sababu za kuteremka aya za mirathi. Pia hawakuwa na nafasi yoyote ya haki wala maoni ndani ya utawala wa Makka. Zaidi walikuwa wanawake wakiamiliwa kama viumbe dhalili kiasi kwamba kuzaliwa mtoto wa kike ilikuwa kama mkosi, nuksi na balaa kwa jamii, kiasi kwamba walikuwa wako tayari hata kuwazika mabinti zao wakiwa hai.

Amesema Allah Taala:

وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُمْ بِالأُنثَى ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ (النحل: 58)

‘Na anapopewa habari mmoja wao kupata mtoto wa kike huukunja uso wake hali ya kuwa amechukia kwa kujaa sikitiko.’

يَتَوَارَى مِنْ الْقَوْمِ مِنْ سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ أَيُمْسِكُهُ عَلَى هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ أَلاَ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ (النحل: 59).

Akiona aibu kuonana na watu kwa sababu ya khabri mbaya (kupata mtoto wa kike) je abaki nae kwa fedheha au amzike ardhini ( akiwa hai), ni mabaya wanayoyahukumu.

Dhulma hizi kwa wanawake hazikuwa tu kwa jamii ya Makka, bali ni mila iliyokuwa imeenea maeneo kadhaa ulimwenguni, kama ilivyokuwa Misri  zama hizo, wakati inapotokea kupungua maji katika Mto Nile, ambapo kafara kubwa ilikuwa ni kumtupa ndani ya mto binti mzuri ili kuondoa mkosi. Aidha, mabinti walikuwa kama bidhaa wakilazimishwa kujiuza kwenye majumba ya uashareti.

Kwa upande wa siasa kwa maqureishi, maamuzi yalikuwa chini ya watu maalumu, watu duni kama vile wakina Walid bin Mughiyrah,  tena wakiwatungia watu sheria kwa kufuata matamanio ya watu wachache ndani ya Daarul Nadwa, ndio wenye maamuzi na mustakbali juu ya watu wa Makka.

Siasa yao ilikuwa imejengwa juu ya utabaka, ikiwa ni tabaka maalumu tu yaani mabwenyenye wa kiquraishi ndio tabaka lenye mamlaka na kuamua kila kitu, kiasi kwamba jamii nyingine kama watumwa na wengineo wakionekana kuwa watu duni waliotengwa.

Yote haya yaliendelea mpaka alipokuja Mtume Muhamad saw alipowalingania watu juu ya kumpwekesha Mungu mmoja akiwazuia kupunja katika vipimo, kuzika mabinti zao, akawaongoza ibada sahihi nk. Aidha, aliwaandaa maswahaba zake kuwa na nafsiya na akillya ya Kiislamu (shakhsiyya) kiasi kwamba aliwamakinisha ufahamu sahihi juu ya maisha ya dunia, nao kwamba ni lazima maisha haya ya dunia yaendeshwe kwa kufuata maamrisho ya Mola na kuacha makatazo yake, na pia maisha haya yana mahusiano na   maisha ya kabla yake, na siku ya mwisho tutahesabiwa kutokana na matendo ya duniani.

Ufahamu huo wa aina yake aliokuja nao Mtume SAAW kutoka kwa Mola wake ulikuwa na msukumo mkubwa katika kuleta mabadiliko na kuulingania Uislamu pasina kuogopa lawama ya mwenye kulaamu.

Imepokewa kuwa Jaafar bin Abi Twalib ra. aliposimama kidete kuutetea Uislamu na kuulingania mbele ya mfalme Najashi wa Habash baada ya propaganda kutoka watu wa Makka, alisema kumwambia mfalme

‘Tulikuwa sisi wakati wa ujahillya tukiabudu masanamu tukila mizoga tukifanya mambo machafu tukikata udugu tukiwafanyia ouvu jirani zetu, mwenye nguvu akimdhulumu mnyonge tulikuwa katika hali hiyo mpaka Allah SW alipomtuma Mtume miongoni mwetu tunaejua nasabu yake, ukweli wake na uaminifu wake, akatulingania kwa Mola tumpwekeshe na tuache yale tuliokuwa tukiyaabudu sisi na baba zetu, na akatuamrisha kusema ukweli, kutekeleza amana, kuunga udugu na wema kwa majirani na kujizuia kumwaga damu, na ametuzuiya kufanya mambo machafu na kusema uongo na kula mali ya yatima, na kumsingizia mwanamke msafi uzinzi na ametuamrisha kumwabudu Mola tusimshirikishe na chochote na ametuamrisha kuswali kutoa zakka na kufunga….

( Seerah Ibn Hisham,  juzuu ya pili  uk. 257)

Hiyo ndio ilikuwa hali ya wanadamu hasa ndani ya Makka kabla, baada kufikiwa na nuru kutoka kwa Mola wao nayo si mwingine ni Mtume Muhammad saw hali hii ilibadilishwa kwa mabadiliko ya kimfumo baada ya Mtume SAAW kuasisi dola ndani ya Madina, iliyokuwa ndio nukta kianzio ya mabadiliko katika ulimwengu uliokuwa umejaa giza, dhulma na utumwa. Dola hiyo ilisimamia utabikishaji wa mfumo wa Kiislamu na kuibeba risala yake ulimwengu mzima.

Kuanzia hapo nuru ya Mtume Muhaamd SAAW haikuenea tu Arabuni bali ilienea ulimwengu mzima na kubadilisha ulimwengu kithaqafa hata kimadania kupitia hadhara ya Kiislamu ambayo bila shaka kufaulu kwake kulikuwa kusiko na kifani, kiasi cha Uislamu kutawala dunia na kuwa mbele katika kila fani kwa makarne.

Ufanisi huo uliwafanya hata wale wenye chuki na Uislamu kushindwa kulificha hilo na kukiri wazi wazi. Anasema Benard Lewis:

“Uislamu uliwakilisha nguvu kubwa mno ya kijeshi ulimwenguni…. Ulikuwa na nguvu kubwa kiuchumi ulimwenguni, ulifikia kiwango cha juu cha ufanisi katika tareekh ya wanadamu, katika ubunifu na sayansi…”  (Lewis, 2002)

Yote hayo yanatupa picha ya hali iliyokuwa pale Mtume Muhammd SAAW na maswahaba zake na waliowafuata kwa wema alipouwacha ulimwengu katika hali nzuri isiyokuwa na kifani

Lakini pindi Waislamu waliporudi nyuma kifikra na kuacha kuubeba Uislamu kama alivyotufundisha Mtume Muhammad SAAW tulizorota kifikra na kufungua mlango kwa makafiri wakoloni kupenyeza fkra  chafu za utaifa, ukabila, uhuru, demokrasia nk, hapo Umma wa Kiislamu ulizorota na mwishowe kuanguka kwa dola ya mwisho ya Kiislamu kupitia kuzorota huko.

Na mara baada ya kuanguka serikali hiyo, ule muongozo wa Mtume SAAW ukaondoka katika nyanja za maisha ya Waislamu, na hatimae Umma wa Kiislamu umekuwa katika dhiki, maisha mabaya, kudhulumiwa, kuporwa ardhi zao, mali zao, rasilimali, kuvunjwa heshima ya Waislamu na Uislamu nk.

Leo hatuna budi kurudi kuufuata mwongozo aliotuachia Mtume SAAW kwa kupitia kurejesha tena serikali ya Kiislamu kwa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu kwa kupitia mvutano wa kifikra na kisiasa pasina kutumia nguvu wala mabavu ili  kuutoa ulimwengu katika giza totoro na kuurejesha tena katika nuru ya Mtume SAAW ili iwakomboe Waislamu na walimwengu kwa jumla.

Kama alivyotukumbusha Mtume SAAW alipotamka,

“Nimekuacheni katika njia nyeupe, usiku wake kama mchana wake, maadamu mtashikamana navyo hamtopotea, kitabu cha Allah Taala na Sunna za bwana Mtume SAAW.”

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Issa Nasibu

 

Maoni hayajaruhusiwa.