Tafakuri ya Siku ya Nyerere

Oktoba 14 huwa ni Siku ya Kumbukumbu ya Nyerere, raisi wa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mwaka huu itakuwa imefika miaka 20 tangu kutokea kifo chake. Mwalimu Nyerere kama walivyo wengi wanaoitwa wapigania uhuru amekuzwa sana, kupewa hadhi hadi wengine kukaribia kumfanya mtakatifu anayestahiki kuabudiwa kinyume na uhalisia wa mambo ulivyo.

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia nafasi ya wakoloni wa kale, yaani Uingereza na Ufaransa ilidhoofika kimataifa. Badala yake dola ya Marekani ilikuja juu kiushindani kuondosha athari ya madola mawili hayo kiulimwengu. Licha ya kuwa madola hayo yanabeba mfumo mmoja wa kibepari, lakini yanatofautiana katika upande wa maslahi ya kinchi.

Uingereza ikaja na mikakati kadhaa kuokoa na kuhami ubwana na athari yake katika makoloni yake, kama vile mbinu ya kumakinisha Jumuiya yake ya Madola, kuimarisha mtandao wake wa elimu katika mashule na vyuo na kupitia taasisi zake hizo za elimu kuzalisha vibaraka thabiti atakaowapa ‘uhuru bandia’ kutii wimbi la kimataifa lenye msukumo wa Marekani kwa lengo la kuendelea kuhifadhi athari yake.

Mabingwa wa kiengereza katika tasnia ya elimu ndani ya makoloni ya Uingereza kama Lord Crommer ndani ya Misri na Lord Macaulay ndani ya India waliweka bayana kwamba dhamira ya mfumo wa elimu ya kiengereza ni kuwabakisha wazawa wa makoloni yao kuwa wazawa katika rangi tu, lakini wabadilishwe kuwa waingereza katika vionjo, sera na mitazamo yao.

Chuo cha Makerere cha Uganda katika Afrika ya Mashariki ni kimoja katika mifano mingi ya mkakati huo. Aidha, Nyerere ni mmoja wapo katika wengi wa wahudumu wa Uingereza waliopitia maandalizi hayo kisha kupatiwa masomo zaidi na kunyooshwa zaidi nchini Uingereza. Ndio maana Uingereza ilikuja kwa haraka sana kumnusuru ‘kijana wao’ Nyerere mwanzoni mwa miaka ya sitini ilipozuka zahama ya jaribio la kumpindua.

Aidha, Nyerere kwa kushirikiana na Zubeiri Mtemvu ndio waliotumwa na Uingereza kwenda haraka Zanzibar kufanikisha muungano wa jumuiya za Afro na Shirazi kisha kuzaliwa chama cha kisiasa cha Afro Shirazi Party ambacho kilikuwa chombo cha Uingereza. Chini ya usimamizi wa Nyerere chama hicho kikapindua serikali ya Zanzibar, kisha kufanikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa agizo la Uingereza. Bila ya kusahau namna kilivyotumika chama hicho kupandikiza na kukuza chuki na husuma baina ya Waislamu wa Zanzibar na raia jumla.

Kwa upande wa Tanganyika, Nyerere atakumbukwa sana namna kwa alivyowafanya Waislamu kuwa raia wa daraja duni, alivuruga umoja wao, kusambaratisha taasisi zao na kuwatupilia mbali licha ya mapokezi waliyompa, takrima yao kubwa kwake, kumuhudumia na kumshika mkono katika mapambano ya uhuru.

Nyerere akaibakisha nchi katika himaya ya Uingereza kwa jina la uhuru bandia, huku akiwapa waingereza kila fursa katika kuzoa rasilmali za nchi , ilhali raia wa kawaida hususan Waislamu na pia wasiokuwa Waislamu wakihangaika kwa dhiki na mashaka.

Uingereza ilipoona haiwezi tena kuhimili mikikimikiki na mabavu ya Marekani katika uroho wake wa kuitaka Tanzania ilimuamuru ‘mtu’ wake Nyerere aondoke kwa heshima asije akadhalilika, nae akijifanya kung’atuka. Na mara baada ya mng’atuko huo Tanzania ikatoka katika himaya ya Uingereza na kuingia rasmi katika himaya ya Marekani hadi leo hii.

Maoni hayajaruhusiwa.