Taarifa ya Famili Tatu kwa Wanahabari Kuhusiana na Ndugu Zetu Walioko Mahabusu kwa karibu Miaka Mitatu Sasa
بسم الله الرحمن الرحيم
Magomeni Makuti Dar es Salaam – 09 Julai 2020 M – 18 Dhu al-Qi’dah 1441 H
Ndugu Wanahabari,
Asalaam alaykum, na Habari za mchana:
Jina langu naitwa Tiba Moshi Athumani Kakoso, awali ya yote kwa niaba ya wawakilishi wa familia tatu mbele yenu niwashukuruni kwa kutenga muda wenu wenye thamani kujumuika nasi leo hii katika mkutano wetu huu pamoja nanyi, tukitaraji mtasaidia na kutimiza wajibu wenu kwa kupaza sauti zenu juu kwa kilio chetu.
Ndugu wanahabari,
Mbele yenu, sisi ni wawakilishi wa familia tatu: Familia ya kwangu mimi ya Moshi Athumani Kakoso, familia ya mzee wetu Salum Omar Bumbo, na familia ya Suleiman Mkaliaganda ya Mtwara.
Ndugu wanahabari,
Tumewaita hapa kuelezea kilio, masikitiko na sononeko letu kutokana na masaibu ya ndugu na wanafamilia wetu ambao ni Omar Salum Bumbo (51) Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso (41) na Waziri Suleiman Mkaliaganda (33), wote hao wamekuwa mahabusu katika gereza la Lilungu la Mtwara kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa.
Ndugu wanahabari,
Masaibu ya ndugu na wanafamilia wetu hao yalianzia kama ifuatavyo:
Kwa kuanzia, mnamo tarehe 27/10/2017 mwanafamilia wetu Omar Salum Bumbo mkaazi wa Tandika Relini, Dar es Salaam, fundi mjenzi / mwashi alinyakuliwa na kutekwa na wanaoaminika kuwa ni maafisa wa usalama, baada ya mmoja wa maafisa hao kijanja kumpigia simu kwamba angetaka kumpatia Omar Salum Bumbo kazi ya ujenzi, kisha alipofika eneo aliloahidiwa kukutana nae maeneo ya Tabata alitekwa na wanaoaminika kuwa maafisa usalama, kumsweka garini, kutoweka nae kusikojuulikana, sambamba na kumtisha dereva wa bodaboda aliyemfikisha Omar Bumbo eneo hilo, kuondoka mara moja.
Ndugu wanahabari,
Siku tatu baada ya tukio la kutekwa Omar Salum Bumbo (30/10/2017) nae Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso ambae ni mwalimu wa dini ya Kiislamu na mfanyabiashara alitiwa nguvuni nyumbani kwake (hapa) Magomeni Makuti, Dar es Salaam mbele ya familia yake na watu waliojitambulisha kuwa maafisa wa usalama. Baada ya shinikizo la Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso kwa watu hao waliomtia nguvuni, kwamba kuna ulazima wa suala lake kuarifiwa mwenyekiti wake wa mtaa, wakapita karibu na Afisi ya Mwenyekiti wa serikali ya mtaa, ambapo maafisa hao waliomtia nguvuni waliahidi mbele ya mwenyekiti huyo wa mtaa kwamba taarifa zote za Ust. Ramadhan Moshi Kakoso zingepatikana katika kituo cha Polisi cha karibu.
Ndugu wanahabari,
Kwa masikitiko makubwa kwa wote wawili hao, (Omar Salum Bumbo na Ust. Ramadhan Moshi Kakoso) zilipita wiki kadhaa bila ya kupatikana taarifa za mahala walipo na kujua mashtaka yao, licha ya jitihada kubwa ya familia, ndugu na marafiki kufuatilia kwa karibu katika vituo mbalimbali vya Polisi. Jambo lililoashiria kutokuwepo kwa nia njema kutoka vyombo vya dola dhidi yao. Kwa kipindi chote kwa wawili hao, si tu kulikosekana taarifa zao, bali pia walinyimwa haki zao msingi, kama haki ya uwakilishi wa kisheria, kuwasiliana na familia zao nk.
Ndugu wanahabari,
Hatimae wawili hao (Ust. Ramadhan Moshi na Omar Salum Bumbo) wakapelekwa Mtwara na kuunganishwa na mtuhumiwa mwengine wa tatu ambae ni Waziri Suleiman Mkaliaganda, mwalimu wa sekondari hapo Mtwara mjini, aliyekamatwa mapema zaidi huko tangu tarehe 21/10/2017 karibu na nyumbani kwake mtaa wa Kiyangu hapo hapo Mtwara mjini. Wote watatu kwa pamoja wakafunguliwa kesi za makosa ya ugaidi, na mnamo tarehe 5/12/2017 kimya kimya wote wakaanza kupelekwa Mahkama ya Wilaya ya Mtwara kwa ajili ya kutajwa kesi yao.
Ndugu wanahabari,
Kwa kipindi chote cha zaidi ya miaka miwili na nusu sasa ndugu zetu hao wakiwa mahabusu, licha ya kuwa mbali na familia zao, ndugu, marafiki na kusita kwa shughuli zao za uzalishaji na za kijamii, pia wamerundikwa katika mahabusu zenye mazingira duni kibinadamu, yakikosa usalama wa kiafya na huduma stahiki kwa jumla. Kubwa, baya na la kusikitisha zaidi, kesi yao imekuwa ikitajwatajwa tu kila wiki mbili na kurudishwa mahabusu bila ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, kwa maelekezo kuwa ushahidi haujakamilika.
Kama suala ni upelelezi kutokamilika kwa karibu miaka mitatu sasa, ilikuwa na haja gani ya kuwakamata ndugu zetu hao na kuwaweka mahabusu na mateso? Kwanini imekuwa watuhumiwa wa tuhuma hizo za ugaidi tu, ndio kesi zao hazisikilizwi kinyume na ilivyo kwa makosa mengine makubwa zaidi ikiwemo mauaji?
Ndugu wanahabari,
Kwa kumalizia, sisi wana familia na ndugu wa watuhumiwa hao watatu tuliowataja tunachukua fursa hii kupitia vyombo vyenu kupaza sauti zetu kuitaka serikali ambayo imejipambanua kuwa ni serikali ya kusimamia haki na ya kutetea wanyonge itoe msukumo kwa vyombo vya kusimamia haki ili ndugu, na wanafamilia wetu hao na mahabusu wengine mfano wao ambao wanaendelea kukata miaka mahabusu watekelezewe kwa haraka utaratibu wa kisheria ambao ni haki yao, ili kesi zao zisikilizwe, na kama ushahidi haujakamilika wapatiwe dhamana, na kama ushahidi haupo waachiliwe huru mara moja, kuliko kubakia katika hali ya sasa ambayo inatoa sura ya wazi ya uonevu.
‘Uadilifu na haki huzaa furaha na utangamano, dhulma na uonevu huzaa chuki na uadui’
Ahsanteni sana, tunawashukuru tena kwa kutusikiliza.
Wawakilishi wa familia:
- Tiba Moshi Kakoso
…………………………….
- Salum Omar Bumbo
………………………………
- Faizuna Juma Issa
……………………………….
#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction
Maoni hayajaruhusiwa.