Simamisheni Khilafah Isimamie Hijja

Usumbufu katika mchakato wa safari ya Hijja umekuwa kitu cha kawaida kiasi kwamba baadhi ya Waislamu hudiriki hata kudai na kuhalalisha kwamba hali hiyo ni ya kimaumbile yaani huko kupata taabu ni sehemu ya uwezo unaotakiwa na sharia ili kuweza kuhimili mashaka katika safari hiyo.

Katika maeneo yetu ya Afrika Mashariki limekuwa kama jambo la mchezo wa kuigiza kwa kila mwaka kwa mahujaji kupata taabu na kila aina ya usumbufu na kuwaathiri zaidi miongoni mwa wazee na wanawake. Usumbufu hupatikana  amma  wakati wa kuelekea Makka  au wakati wa kurejea kwa kuchelewa kurudikwa wakati uliopangwa.

Hali kama hiyo ya usumbufu ilidhihirika wazi wazi mwaka jana wakati kundi kubwa la mahujaji wa Tanzania waliokuwa chini ya wakala wa ‘Tanzania Hajj Trust’ walipokwama katika kiwanja cha kimataifa cha Dar es Salaam kwa siku kadhaa na baadae kurundikwa na kusombwa na ndege duni katika dakika za majeruhi. Kadhalika yamejiri hayo mwaka huu kwa kusota mahujaji karibu 20 hapo hapo Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam kwa siku kadhaa, wakisubiri hatima ya mawasiliano kutoka kwa wakala wao Jumuiya ya ‘Al-Taibah’ na Shirika la ndege la Yemenia. Kwa hakika ni msiba mkubwa! Kana kwamba mahujaji hawa wamekwenda kuomba msaada wa ‘lift’ katika safari hiyo!. Usumbufu wote kama huu unawakuta mahujaji licha ya kuwepo kwa utitiri wa Jumuiya mbalimbali zinazosimamia safari za kuwapeleka watu katika ibada hiyo.

Amma kwa upande wa nchi nyingine kwa mfano nchi ya Tajikistan serikali inaweka vikwazo kuzuia watu kwenda katika ibada hiyo, pia usumbufu mkubwa na wazi zaidi ni ule unaotokana na dola dhaifu ya kifalme ya Saudia namna ilivyoweka shehena ya vikwazo na urasimu usiokuwa wa lazima kwa kuanzia mahujaji ndani ya Saudia ambao hawatakiwi kuhiji baada ya hija yao ya mwanzo ila baada ya kukamilika  miaka mitano, (‘hii kali hata Mtume SAAW hakuiona ?) kuweka gharama za unyang’anyi na dhulma ya kile wanachodai ati ‘viza ya Hijja’, ubaguzi wa kuwafanya wasiokuwa raia wa Saudia kama wageniwa daraja la pili  kwa kuwang’ang’aniza vitambulisho maalum vya kibaguzi kana kwamba ni vibarua/manamba katika shamba la mkoloni. Huku Serikali hiyo kibaraka wa Marekani ikijitia upofu na uziwi wa nyoyo kama kwamba hawaijui au kuisikia kauli tukufu ya Azza wa Jallah alipotangaza kwamba msikiti huo ni sawa kwa waislamu wote.

وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاءً الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِي

…‘Na msikiti mtukufu [Makka] ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote

sawa sawa ,kwa wakao humo na wageni’.(TMQ 22:25)

Na mengi mengineyo katika usumbufu unaotendwa na Serikali ya Saudia ikiwemo kulitumia vibaya jukwaa la Hijja kama njia ya kukuza fikra potofu  na kuchawanya maelfu kama si malaki ya majasusi wao kuwachunguza mahujaji si kwa lengo la kuwalinda kamwe! bali kulinda utawala wao dhalimu na kuwazuia waislamu wasipate fursa ya mawasiliano na ndugu zao wa kiislamu wa sehemu nyengine.

Hali hii ya usumbufu na masuala ya usimamizi wa hijja kwenda shaghalabaghala ni matokeo ya kutokuwa na msimamizi rasmi anayeisimamia ibada hii .Katika sharia ya Kiislamu jukumu hilo ni la Kiongozi rasmi wa kiislamu (khalifah). Katika kitabu cha ‘Taarikhu-ul Umamil –Islamiyah’ mwandishi anaeleza bayana kwamba: ‘katika kazi kubwa za Khalifah ni kusimamia Hijja’.

Hayo alianza kutuonesha wazi wazi kivitendo SAAW katika uhai wake akiwa kama kiongozi kwa kusimamia yeye mwenyewe ibada hii kama alivyofanya katika Hijja ya kuaga katika mwaka wa kumi hijria au kuchagua mwakilishi kwa niaba yake kama alivyomchagua Abubakar r.a kuongoza Hijja katika mwaka wa tisa wa Hjria, sambamba nae akampa Ali r.a jukumu maalumu la kwenda kutoa tangazo maalumu kutoka Surat Tawba kwa mahujaji wote.

Pia Makhalifah mbalimbali baada ya kuondoka SAAW walishika na kuandama mwenendo huo kiasi kwamba katika kila Hijja hakukosekana Khalifah au mwakilishi wake. Jukumu la kuisimamia Hijja lilibebwa kwa umakini wa hali ya juu wakati wote na makhalifa walikuwa mstari wa mbele. Kwanza, katika utendaji na usimamizi wa ibada yenyewe  na  pili katika  kutengeneza mazingira mwanana na mepesi ya  kuwawezesha mahujaji kuikamilisha ibada hii bila ya usumbufu kama uliopo leo.

Katika upande wa usimamizi wa ibada yenyewe makhalifa walikuwa wakihudhuria wenyewe au kwa kutuma wawakilishi wao, kwa sababu pia katika ibada hiyo ilikuwa ni pahala muwafaka zaidi kwa Khalifah kukutana na mawali / magavana wa sehemu mbali mbali na kupokea ripoti zao za usimamizi, lakini pia kupokea malalamiko ya raia kutoka sehemu za majimbo ya dola kuhusiana na viongozi wanaowasimamia kwa niaba yake. Mshairi mmoja akimsifu mmoja kati ya makhalifa wa Abbasiyah alisema:

“Atakaetaka kukutana na wewe ni katika miji miwili ya mbali. Amma katika Hijja au mipakani mwa dola (kwa jihadi)”

Na kwa upande wa pili pia Makhalifa walichukua hatua kabambe na thabiti  katika kutengeneza na kuandaa mazingira mwanana na sahali ili kuwawezesha mahujaji kufika katika ibada hiyo salama usalimini ,haraka na  kwa wepesi bila ya usumbufu wowote. Mfano mzuri kabisa wa ukweli huo tunaweza kuona namna Khilafah ya mwisho (Khilafah Uthmania)licha ya  kuwa katika karne ya ishirini ilikuwa imedorora na kudhoofika kiasi cha makafiri kuipa lakabu ya ‘Mahatuti wa Ulaya’ (‘Sickman of Europe’)  kwa kuandamwa na makafiri na kukabiliwa na upinzani kutoka kwa vibaraka wao wa  kiarabu na waturuki, kadhalika sehemu kubwa  ya ardhi yake ilikwishaporwa na madola ya  Uingereza na Ufaransa lakini bado Khilafah haikutelekeza dhamana yake ya kusimamia ibada ya Hijja na  ilibeba mabegani jukumu la kusimamia kiudhati ibada hiyo   na  kuwasahilishia waislamu mazingira ya kuweza kuifanikisha ibada ya Hijja kiurahisi. Katika kulifikia hilo Khilafah Uthmania chini ya uongozi wa Khalifah Abdul-HamidII ilijenga reli iliyokuwa ikijuulikanwa kwa jina la‘Reli ya Hijaz’. Mradi huo ulianza katika miaka 1900 na kufunguliwa rasmi katika Septemba mosi mwaka wa 1908.

Reli hii iliunganisha Makao makuu ya Khilafah Istambul Uturuki na kupitia katika majimbo mbali mbali ya dola ikiwemo miji mikubwa ya kiislamu ya   Damascus Syria hadi ndani ya Madina katika nchi ya Hijaz.

Kwa kujengwa ‘Reli ya Hijaz’ iliwezekana kuondosha usumbufu wa safari ya mahujaji wa kusafiri karibu miezi miwili kutoka Damascus hadi Madina katika hali ya hewa tete na kuifanya sasa kuwa safari ya siku chache tu,na ya gharama ndogo kutoka  Paundi 40 za awali hadi kufikia Paundi 3.5 kwa tiketi ya treni. Kufikia mwaka 1912 Treni hiyo ilifanikiwa kusafirisha karibu mahujaji 30,000 kwa mwaka, na kufikia mwaka 1914 iliweza kusafirisha idadi ya  juu ya mahujaji 300,000 kwa mwaka.

‘Reli ya Hijazi’ ilikuja kuhujumiwa na harakati za kujitenga kwa waarabu

(Arab Nationalism) chini ya Sharif Hussein kwa mashirikiano na jasusi Lawrence wa kiengereza [Lawrence of Arabia]

Kwa kuangushwa Khilafah katika mwaka 1924 na kukatwa mipaka katika nchi za kiislamu chini ya mkataba wa Sykes-Picot,’Reli ya Hijaz’ imebakia kuwa katika kurasa za kihistoria na usumbufu katika safari na usimamizi wa Hijja ni hadithi zisizokwisha kila siku.

Katika hali kama hii ni jukumu letu kama umma mtukufu kurejesha tena Khilafah Rashidah ili iweze kusimamia tena ibada hii kwa udhati wake na kuondosha kila aina ya vikwazo na usumbufu. Na hapo tutaona ladha ya maneno ya Mtume SAAW iliyonukuliwa katika Sahih Bukhari na Muslim aliposema:

Kwa hakika Imam (Khalifah/kiongozi) ni mchungaji naye ndiye msimamizi juu ya raia wote”

Jee Umma mtukufu wa Kiislamu Imamu wetu leo yuko wapi?

Maoni hayajaruhusiwa.