Si Mageuzi ya Sheria za Uchaguzi wala ya Katiba Yatakayoikomboa Tanzania
بسم الله الرحمن الرحيم
Habari:
Wakati Tanzania ikitarajia kuwa na Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, kumeibuka wimbi la mgawanyiko wa kisiasa na mitazamo tofauti kuelekea uchaguzi huo miongoni mwa wanasiasa na vyama vya kisiasa ambalo limezua mjadala mkubwa wa kisiasa.
Maoni:
Mazingira ya sasa ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu nchini Tanzania yameleta mitazamo mitatu mikuu ya kisiasa ambayo inaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na makundi mbalimbali ya watu kote nchini.
Kundi la kwanza ni wale wanaosisitiza haja ya haraka ya mageuzi ya sheria za uchaguzi, kundi linaloongozwa na chama kikuu cha upinzani-Chadema chini ya kaulimbiu yao, “Bila ya Marekebisho Hakuna Uchaguzi.” Msimamo huu una mtazamo kwamba bila kuwepo kwa mageuzi, uchaguzi hautakua huru na wa haki, na unapaswa kususiwa.
Kundi jingine ni wale wanaotaka marekebisho ya katiba, msimamo unaopigiwa debe na chama cha pili cha upinzani – ACT Wazalendo. Msimamo huu unasisitiza haja ya marekebisho ya katiba, lakini chama hiki kiko tofauti na Chadema, hakina mpango wa kususia uchaguzi.
Kundi la tatu ni wale wanaounga mkono hali halisi iliyopo (serikali). Hawaoni umuhimu wa mabadiliko katika masuala ya uchaguzi wala katiba. Wanaunga mkono katiba ya sasa, kanuni za uchaguzi na taratibu kama zilivyo. Kundi hili liko chini ya ushawishi wa serikali iliyopo madarakani na chama tawala – CCM.
Makundi yote matatu ya wanasiasa, vyama vya kisiasa na wafuasi wao wanapaswa kujua kwamba kamwe misimamo yao hiyo haina chochote kwa manufaa ya nchi na watu kama wanavyodai wote.
Ama wale wanaounga mkono mageuzi ya kanuni za uchaguzi, wanapaswa kukumbuka kwamba kumekua na mageuzi mengi ya uchaguzi hapo awali, kama vile ya 2010, 2019 na mageuzi ya karibuni zaidi ya 2023 ya Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi 2023. Lakini hakuna hata moja lililoleta tija.
Kwa wale wanaounga mkono mageuzi ya katiba wakioongozwa na chama cha pili cha upinzani cha ACT-Wazalendo, kampeni ambayo ilizinduliwa pia mwaka 2024, pia tunapenda kuwakumbusha kwamba, Tanzania tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1961 imepitia mageuzi na marekebisho mengi ya katiba. Mathalan, mwaka 1961, 1962, 1964, 1965, na 1977. Zanzibar kwa upande mwengine pia ilikuwa na mageuzi mnamo 1963, 1979 na 1984. Tangu wakati huo kumekua na mfululizo wa marekebisho mengi ya katiba katika sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hakuna kilichofanikiwa.
Kwa wale wanaounga mkono utawala uliopo, wafuasi wa chama tawala CCM na serikali iliyopo madarakani wanaoridhia kanuni zilizopo za uchaguzi na katiba za sasa, nao pia hawako kwenye upande salama, kwani udhaifu wa kanuni na katiba za sasa unaonekana wazi wazi na kila mtu.
Makundi yote matatu yameshindwa kuelewa chanzo kikuu cha tatizo ambacho si kanuni za uchaguzi, katiba au upinzani (kwa wanaounga mkono serikali). Chanzo kikuu ni mfumo wa ubepari ambapo kanuni na sheria zote za sasa nchini Tanzania na mataifa yanayoendelea ni za kigeni na za kikoloni.
Kupitia kanuni na sheria hizi za kibepari, ukoloni mamboleo unamakinishwa nchini Tanzania na nchi zinazoendelea na kuyawezesha mataifa ya kibepari kuyanyonya mataifa haya.
Hivyo basi, mabadiliko yenye tija ya kuikomboa Tanzania na kwengineko yanapaswa kuelekezwa katika kuondoa mfumo muovu wa ubepari kwa kuubadilisha kwa Uislamu chini ya utawala wake wa kilimwengu (Khilafah).
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.