Risala ya Mtume (Saaw) Imeletwa Kushinda Mifumo Yote
Katika mwezi huu wa Rabi ul-awwal (Mfungo Sita), mwezi aliozaliwa kiongozi wetu na mkombozi wa wanadamu aliyetumwa kuwatoa wanadamu kutoka katika viza vya kila aina na kuwaleta katika nuru ya Uislamu, ni vyema kuangazia malengo mapana ya mfumo aliokuja nao wa risala ya Uislamu.
Allah (SWT) Anasema:
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَى وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ (التوبة: 33).
“Yeye ndiye aliyempeleka Mjumbe wake (Muhammad saaw)) kwa uongofu na dini (mfumo wa Kiislamu) wa haki ili ushinde mifumo mingine yote, hata kama washirikina watachukia” (TMQ At-Tawba: 33)
Katika aya hii Allah Taala anatuonyesha lengo la ujumbe wa Muhammad (saaw) kuwa ni kuutawalisha mfumo wa Kiislamu kuwa juu ya mifumo mingine, kwa kuwa huu ndio mfumo wa haki na sahihi.
Mfumo huu wa Kiislamu ndio pekee unaotokana na wahyi kutoka kwa Allah Taala ambae ni Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo, ambapo mifumo miengine kama Ukomunisti ambao hivi sasa haupo tena katika nafasi ya utawala, na Ubeperi ambao ndio wenye kutawala ulimwengu kwa sasa, ni mifumo isiyotoka kwa Allah Taala bali ni zao la akili ya mwanaadamu.
Akili kwa kuwa ni kiumbe, ni dhaifu na yenye mipaka isiyoweza hata kutambua kile kitakachotokea baada ya sekunde moja, seuze kuweza kubuni mfumo wa maisha utakaosimamia mambo ya walimwengu na ulimwengu.
Kutokana na ukweli wa mfumo huu wa Kiislamu ndipo imeshuhudiwa kuwa uliweza kupata mafanikio makubwa katika nyanja zote za kimaisha ikiwemo utawala, siasa, uchumi, sheria, jamii nk. chini ya utawala wa dola yake ya Kiislamu
Katika kipindi hicho dola iliweza kujumuisha jamii za watu wa mataifa mbalimbali wenye lugha, tamaduni, mila na desturi tofauti na kuwafanya kitu kimoja, walio na udugu na upendo chini ya bendera ya Laa ilaaha illa llaah Muhammada-Rrasulullah.
Dola iliweza kusimamia na kuboresha ustawi wa hali za kimaisha kwa raia wake kwa kusimamia rasilmali zake kwa manufaa ya raia wake. Kwani hili ndio katika jukumu msingi la dola ya Kiislamu. Pia iliweza kusimamia haki na sheria kwa usawa na uadilifu baina ya watu wote, bila kutofautisha baina ya watawala na watawaliwa, matajiri na masikini au wenye hadhi na wasio na hadhi katika jamii.
Dola iliweza kulinda heshima na utu kwa wote, wakiwa wanawake, wanaume, watoto, Waislamu na wasiokuwa Waislamu bali na hata wanyama.
Hali hiyo ni kinyume na iliyopo sasa katika biladi zetu zilizo chini ya mfumo dhalimu wa kibepari. Leo kunashuhudiwa ubaguzi, chuki, uhasama, baina ya wana jamii, uporaji wa rasilmali unaofanywa na mabepari wachache, wakoloni na vibaraka wao, huku idadi kubwa ya raia wakiachwa katika dimbwi la unyonge na umasikini wa kupindukia.
Chini ya mfumo huu wa kibepari, watawala, matajiri na wenye hadhi huwa wako juu ya sheria na ndio wenye haki, bali heshima na utu wa mwanadamu kwa mnyonge hauthaminiwi.
Ni jambo la kutarajiwa kuwa wakoloni hawa na vibaraka wao ambao ndio wanufaikaji wakubwa chini ya mfumo huu wa kibepari uliopo, hawatakuwa radhi kuona mfumo wao unaondoka na kusimamishwa mfumo wa haki na sahihi wa Kiislamu. Ndipo Allah Taala akaashiria hayo katika aya kuwa mfumo wa Kiiislamu utashinda ‘hata kama washirikina watachukia’.
Wapingaji na maadui hawa wa mfumo wataendeleza njama na uadui wao kwa kutumia mbinu mbalimbali, ambapo hilo kwetu tukiwa Ummah wa Kiislamu mmoja na Ummah bora ni changamoto katika kutekeleza wajibu wetu wa kuurejesha nafasi yake mfumo wetu.
Tutayafanya haya ya kupambana kifikra na kisiasa bila ya nguvu, mabavu wala silaha kama alivyolingania Mtume wetu SAAW dhidi ya wapinga mfumo – Maquraish hadi akaweza kuusimamisha na kuutawalisha.
Kupitia njia/ manhaj aliyopewa na Mola wake Mtume Muhammad saaw akaweza kuutabiqisha/kuutekeleza Uislamu na kuchukuwa nafasi yake ya kuwa juu na kuishinda mifumo miengine.
Tutaweza kuyafanya haya kwa kufuata manhaj ya Mtume wetu SAAW huku tukiwa na yaqini ya ushindi iliyoambatana na imani thabiti nafsini mwetu, bila ya kujali udhaifu au nguvu za maadui wetu.
وَلاَ تَهِنُوا وَلاَ تَحْزَنُوا وَأَنْتُمْ الأَعْلَوْنَ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ (آل عمران: 139
“Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini” (TMQ Al-Imran: 139)
#MuhammadNuruYetuKigezoChetu
Habib Abdullah
Risala ya Wiki No. 62
24 Rabi’ al-awwal 1441 Hijri 21/11/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.