Ramadhani: Kipambanuzi Cha Kimfumo

ﺑﺴﻢ ﷲ ﺍﻟﺮﺣﻤﻦ ﺍﻟﺮﺣﻴﻢ

Alhamdulillah tupo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni masiku adhimu kwa binadamu wote na haswa Waislamu. Ni mwezi ambao hudhihirisha utu wa mtu kiasili. Kiasili binadamu ni kiumbe mwana jamii (social creature) ambaye huishi na kutekeleza maisha yake kwa kutegemeana na viumbe wengine, akiwemo binadamu mwenzake. Kutegemeana huku kwapasa kufahamike vyema kwa binadamu ambaye ndie kiumbe pekee mwenye akili na utashi ili kuratibu mahusiano yao wenyewe na pia mahusiano yao na viumbe wengine. Kuipuuza au kuidogosha asili hii ni chanzo msingi cha matatizo yote duniani ikiwemo yanayochangia uwepo wa mabadiliko ya tabia nchi (climate change) ambayo hujiri kwa kukosekana kwa ufahamu sahihi juu ya mahusiano haya.

Ili kuyafahamu mahusiano haya ndipo mfumo wa Kiislamu ukamjenga mwanaadamu katika akili inayohisi na kuguswa na hali za wengine. Ibada ya Swaumu ya Ramadhani ni nyenzo msingi kwa mafunzo haya, hususan mahusiano mema baina ya wanaadamu.
Kufunga swaumu ya Ramadhani ni kujizuia kufanya mambo ya halali kwa muda maalumu. Kiasili mambo yaliyo haramu, ni haramu muda wote, sio kwa Ramadhani tu. Hivyo, katika mfungo huu Waislamu pamoja na kuwa na uwezo na mambo hayo ya halali, huacha vyakula na vinywaji vyao katika mchana, hujitenga katika jimai na wenza wao kwa mchana na huzidisha matendo mema kwa kutaraji malipo ya thawabu yasioshikika kama kitu cha kimada (intangible benefits). Pia hujipinda kwa toba baada ya kuyatathmini maisha yao na kukiri makosa yao.

Mtu kushinda na njaa kwa khiari japokuwa ana uwezo wa kula na kunywa anachotaka na anapotaka, ni ukumbusho kutoka kwa Allah SW kwa wanaadamu juu ya neema walizonazo ambazo baadhi ya wenzao hawana, ikiwemo chakula. Walionacho huoneshwa uchungu wa njaa na kiu ili wazihisi dhiki na tabu za kushinda na njaa huku wakikodolea macho majokofu (friji) yao yaliosheheni vyakula na vinywaji. Ni kama masikini wanavyoumia huku wakikodolea macho na kuumia pua kwa vyakula vinono vya matajiri, au bidhaa madukani na majumbani. Hivyo basi, kufunga huku ijengeke kwa wafungaji nishati ya kuwasukuma kuwasaidia wengine kwa kile walichojaaliwa na Allah SW. Kujitolea huku ni kwa kutafuta kuridhiwa na Allah SW na sio kwa kupata manufaa mbadala ya kushikika (material benefits).

Kwa masikitiko leo jamii inaishi chini ya mfumo wa kirasilimali/ kibepari ambao huongozwa na siasa ya kidemokrasia (kumtenga Mungu Muumba na maisha ya viumbe). Msingi mkuu wa ubepari ni kujenga kila fikra juu ya faida za kimaada, ambayo hupelekea watu kuwa wabinafsi, kutojali nafasi ya Mungu Muumba (Qadhaa) katika kufanikiwa na kufeli katika juhudi za mtu.

Huchukuliwa kuwa kila aliyefanikiwa ni kutokana na akili yake, na aliyeshindwa ni uzembe na kutojituma kwake.
Ubepari umejenga thamani ya mtu ni kutokana na mali anayoimiliki, asiye kuwa na kitu/mali hana utu. Fikra hii ikasukuma watu kuchuma kwa kila njia hata iwe ya kudhuru wengine (kama ujambazi, rushwa, utapeli na riba) ili tu kujikusanyia mali. Katika maisha haya, mwenye nacho humsaidia asiye nacho pale tu atakapojihakikishia kukuza kipato chake kimali. Ima kwa kulipwa mali moja kwa moja au kupata nafuu ya kisera itakayomuongezea faida katika utafutaji wake.

Ni Uislamu pekee unaotaka mtu kujali shida za mwenzake bila kutaraji malipo kutoka kwake, akiamini mtoaji kwamba ni Muumba pekee ndie Aliyemruzuku hicho alichonacho. Muumba ambae Anaweza kukichukua, na akabakia mwanadamu katika hali kama ya asiyenacho kwa muda huo. Kwa hiyo, utakuta lau jamii itakua chini ya serikali ya Kiislamu (ambayo haipo duniani leo hii) hakutokuwa na watu wanaokula na kusaza kwa kiwango cha kukuta majaa yamejazwa vyakula vilivyowashinda. Wala hutakuta watu wenye dhiki ya kukosa mlo japo mmoja, kwani tatizo lao ni tatizo la wenzao walio na nafuu, hulitatua pamoja kama jamii.

Katika mwezi huu wa Ramadhani hudhihirika athari ya utulivu wa jamii. Kila mmoja anakiri kupungua kwa maasi katika jamii, ikiwemo wizi, ulevi, umalaya nk. Haya ni natija/ matokeo ya maisha ya mfumo wa Kiislamu. Mfumo ambao hauna serikali kwa sasa, lakini yanaleta athari na watu hubadilika kitabia kutokana na nishati ya kiimani na kwa msukumo wa kiutu na hisia za kibinadamu tu, sio kwa nguvu ya dola, polisi wala mahakama kama ilivyo katika jamii hizi za kibepari.

Tunaona wafungaji wa Ramadhani hujiepusha kuwakera wengine ili kuhakikisha kufaulu kwa ibada yao. Hujizuiya kutukana, kugombana, na hata wizi na ujambazi hupungua. Wakati mwingine hata wasiokuwa Waislamu, baadhi ya wenye ufahamu wa kiutu, hujiepusha na mambo ambayo ni kero katika jamii ili wasiwakwaze Waislamu wanaofunga.

Utulivu huu wa jamii kwa mwezi wa Ramadhani, uibue hisia thabiti na ujenge fikra za hitajio la usimamizi wa ujumla wa Uislamu katika maisha yetu baada ya kujiuliza, iwapo bila ya dola (Khilafah), jeshi wala mahakama jamii inabadilika hivi, jee ukiwepo usimamizi kwa sharia kamili za Allah SW na muongozo wa Mtume SAW, utulivu na ustawi wa jamii utakuwa mkubwa kwa kiasi gani ?

Jambo hili pia ni changamoto kwa wasiokuwa Waislamu kwa kuibua mjadala juu ya mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kidemokrasia, kwani pamoja na kuwa na dola, majeshi, mahkama na vyombo vyengine vya dola bado hali ya kukosekana amani na utulivu inazidi kuzorota kila uchao. Aidha, hali hii ilete msukumo kwa jamii nzima kuona umuhimu wa siku zote kuwa ‘masiku ya mwezi mtukufu wa Ramadhani’, kushikamana na maadili mema bila shuruti.
#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Na. Abu Nuthutaq

Inatoka jarida la khilafah 59.  https://hizb.or.tz/2019/05/14/khilafah-59/

Maoni hayajaruhusiwa.