Ramadhani Ibada ya Ukombozi

ﺑﺴﻢ ﷲ ﺍﻟﺮﺣﻤﻦ ﺍﻟﺮﺣﻴﻢ

Lengo la Ramadhani ni kuwa tuwe wachamungu. Hii inamaanisha kuwa Waislamu tutakapo itikia wito wa funga ya Ramadhani kwa ukomo wa uelewa wetu katika taratibu za funga na katika utekelezaji wake, bila shaka kwa kiwango fulani tunapata uchajimungu.

Katika kukimbilia fadhila nyingi za mwezi huu, Muislamu hujikurubisha zaidi kwa Allah Ta’ala ili alipwe yalioahidiwa na kupata radhi zake Ta’ala. Mtume saaw amesema:
“Mwezi wenye baraka umekujieni. Allah amefanya funga katika mwezi huo ni wajibu juu yenu. Katika mwezi huo, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa, na mashetani hufungwa (hutiwa minyororo). Kuna usiku (ndani ya mwezi huu) ambao ni bora kuliko miezi elfu. Yeyote anayenyimwa kheri zake basi amenyimwa kikweli.“(Ahmad, an-Nisai, na al-Baihaqi).

Amesema vile vile SAAW: “Funga ni ngao ambayo mja hujikinga kutokana na moto.” (Ahmad).

Kwa fadhila na malipo makubwa kama haya Muislamu huwa tayari kutoa muhanga muda wake, juhudi yake na mali yake kwa lengo la kujitakasa zaidi na kwa kutaraji malipo makubwa zaidi ambayo hayapatikani katika miezi mengine. Muumini hupata furaha na kuihisi kuwa hio ndio furaha ya kweli, na sio ile tu ya kushibisha mahitaji yake ya kibaoljia na matamanio yake ya kijinsia ambayo hujizuwia nayo katika mchana wa Ramadhani, huku akiwa radhi na katika kuitikia mwito wa Mola wake.

Ndani ya mwezi huu Muumini hukuza nafsiya yake na kujengeka sehemu yake ya kiroho kwa kufanya ibada mbalimbali kwa ajili ya Allah Ta’ala aliyeumba, na kujikurubisha kwake kwa kufanya yaliyo mema, na kudumu kujenga kila matendo yake juu ya msingi wa imani kwa Allah (swt), huku akiahidiwa na Mola wake Ta’ala:

التَّائِبُونَ الْعَابِدُونَ الْحَامِدُونَ السَّائِحُونَ الرَّاكِعُونَ السَّاجِدُونَ الآمِرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَالنَّاهُونَ عَنْ الْمُنكَرِ وَالْحَافِظُونَ لِحُدُودِ اللَّهِ وَبَشِّرْ الْمُؤْمِنِينَ (التوبة: 112
(Hao walio ahidiwa bishara njema na kufuzu ni hawa): Wanaotubia, wanaofanya ibada (kwa juhudi kubwa), wanaomshukuru (Allah), wanaofunga, wanaorukuu na kusujudu, wanaoamrisha mema na kukataza mabaya, na wanaohifadhi mipaka ya Allah. Basi wape bishara njema Waumini. (TMQ 9:112)

Muumini huyu huzidisha twaa yake kwa Allah SW katika mwezi huu katika kuitilia nguvu nafsiya yake na kumpelekea kusonga mbele kuelekea kwenye ubora na utukufu. Atajenga uwezo wa kuyatawala maisha yake kwa mujibu wa vipimo vya ‘halali’ na ‘haramu’, kuitafuta kheri kutokana na bidii yake, kufungamana na ibada ya swala na ibada nyengine ikiwemo kuwa shujaa katika kubeba da’wah kwa bidii kubwa. Yote hayo ni kwa ajili ya kupata darja ya pepo ya wafungaji kama alivyosema Mtume SAAW :

Yule aliye miongoni mwa wenye kufunga ataitwa katika mlango wa funga, mlango wa Raiyan …” (Bukhari).

Swaumu katika mwezi huu humjenga Muumini kuwa mwenye subra, mkarimu, mnyenyekevu, mwenye huruma, mwenye moyo uliyostawi uchaji Mungu, na huku viungo vyake vikikimbilia wema badala ya maovu yanayomkasirisha Muumba wake. Akiwa mwenye moyo laini, ulio mtulivu na tamaa ya rehma za Mola wake, hukimbilia yale yenye kumridhisha Allah pekee na kuwacha maovu yenye kumkasirisha Allah SW. Huwa pamoja na Allah SW usiku na mchana akifunga mchana wake na kuswali usiku wake, kuwa tayari kumuitikia Mola wake katika hali zote.

Muumini huyu hatomalizia tu kujitakasa nafsi kwa ibada khaswa kama swala, swadaka nk. Bali husonga mbele zaidi peke kwa kuwa mletaji wa ukombozi wa kikweli katika ulimwengu huu uliojaa dhulma, ufisadi na kila aina ya uovu. Kwa kupitia ibada hii ya funga na muitikio wake wa kikweli kwa Allah SW katika matendo yake kumemfanya moyo wake na nafsi yake kuwa tayari kwa mwito wa ukombozi unaotokana pia na Mola wake Mtukufu, Mwenye nguvu na Aliye Mkuu, na Ambae kupitia kwake ndiko kwenye ushindi. Ndipo ikashuhudiwa katika historia ya Uislamu ndani ya mwezi huu kupatikana ushindi muhimu huku Waislamu wakiwa katika ibada ya swaum. Miongoni mwao ni Vita vya Badri, Fathu Makkah, Fathi ya Andalusia (Spain na Ureno) ushindi wa Salahuddin dhidi ya Makruseda, ushindi katika Vita vya Ain Jaluut nk.

Habib Abdullah

Kutoka Jarida la Khilafah no. 59 Ramadhani 1440 Hijri/ Mei 2019
https://hizb.or.tz/2019/05/14/khilafah-59/

Maoni hayajaruhusiwa.