‘Ngono kwa Ufaulu wa Kimasomo’ Fedheha kwa Nidhamu ya Elimu ya Kibepari
Habari:
Mnamo tarehe 9 Oktoba Mahkama ya Kisutu ya Hakimu Mkaazi jijini Dar es Salaam iliendelea kusikiliza kesi ya Samson Mahimbo, mhadhiri msaidizi katika Chuo cha Usafrishaji cha Taifa (NIT) jijini Dar es Salaam anayetuhumiwa kudai huduma ya ngono kwa mwanafunzi wa kike ili kumpatia alama bora za ufaulu katika mtihani wake wa marudio.
Maoni :
Mtuhumiwa huyu alikamatwa mwaka jana na Taasisi ya Kuzuiya na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kuwekewa mtego, na awali shauri lake kuanza kusikilizwa rasmi mwezi wa Agosti 2018.
Mahakama ilielezwa kwamba mhadhiri Mahimbo alikamatwa mwezi wa Januari 2017 katika nyumba ya wageni akijiandaa kufanya tendo la ngono na mwanafunzi wa mwaka wa pili aliyefeli mtihani wake mkubwa katika somo la masuala ya utawala wa usafiri, kitendo hicho cha ngono ikiwa kwa lengo la kumpatia alama bora za ufaulu. Jambo hilo likiwa kinyume na sheria za kupambana na rushwa Tanzania.
Suala la utoaji wa alama bora za ufaulu kwa ngono ni jambo maarufu sio Tanzania tu bali limeenea kimataifa hususan katika taasisi za elimu za juu, kwa walimu kuwatishia na kuwalazimisha wanafunzi wa kike kwa mkabala wa kuwapatia alama bora za ufaulu, au wakati mwengine wanafunzi hujipeleka wenyewe wakiona ndio njia ya mkato kimasomo.
Mwaka jana, mhadhiri wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chuo kikongwe na mashuhuri Tanzania alipaza sauti yake kwa kunadi kuenea kwa kiwango cha juu cha utamaduni wa utoaji wa alama za ufaulu kwa ngono. Aidha, ugunduzi wa karibuni wa kituo cha BBC kutokana na uchunguzi wa kisiri wa mwaka mzima zimeweka wazi uwepo wa wa suala kama hilo (ngono kwa ufaulu) katika Chuo Kikuu cha Lagos, Nigeria, pia ugunduzi huo ulifedhehi kuenea na kukita mizizi suala la unyanyasaji wa kijinsia. Ugunduzi huo mpaka sasa umepelekea mhadhiri wa kiume kusimamishwa kazi.
https://www.bbc.com/news/world-africa-49971067
Ni jambo la kuhuzunisha sana namna mfumo wa kielimu wa kibepari unavyoleta kiwango kikubwa cha ufisidifu, badala ya elimu hiyo kuwa ndio fungamano thabiti baina na mja na Muumba wake. Pia badala ya elimu hiyo kuwa chanzo cha kutanua na kuendeleza fikra safi na kuzalisha stadi kwa ajili ya ustawi wa binadamu, elimu imegeuka kuwa uwanja wa fujo na aibu unaozalisha nakama mbalimbali.
Fikra ya usekula imeichafua elimu kwa namna nyingi, kama vile kuifanya elimu ndio chanzo cha rizki, kitu kinachowasukuma baadhi ya wanafunzi kuwa katika hali ya kutapatapa na kutenda lolote lile ili kupata alama bora za ufaulu. Wakati huo huo elimu hii huwapa walimu kuwa na kiburi cha hali ya juu kwa kuwa hujihesabu wanamiliki mikononi mwao funguo za rizki kwa ajili ya wanafunzi wote. Amma kuhusiana na wanafunzi wa kike kujipeleka wenyewe kwa ajili ya ngono, au wanafunzi wa kiume wanaotoa rushwa ili kupata alama bora za ufaulu , jambo hilo huashiria moja katika ya mawili: kiwango cha elimu walichokipata wanafunzi hao kutoka sekondari ni dhaifu, au maarifa waliyoyapata hayaendi sambamba na kiwango cha chuo Kikuu. Yote mawili yanafedhehi kushindwa kwa nidhamu ya elimu ya kibepari.
Chini ya fikra za kibepari za ‘uhuru’ taasisi za kielimu zimegeuka kuwa mahala pa aibu na utovu wa maadili. Basi vipi tutarajie taasisi hizi kutoa kizazi safi kitakachoweza kuitumikia vyema jamii zetu?
Ili nidhamu ya kielimu iwe safi, yenye muelekeo thabiti na yenye kuzaa matunda, inahitaji kujengwa juu mfumo thabiti na safi wa Uislamu, chini ya dola yake ya Khilafah Rashidah elimu italindwa na kila aina ya uchafu na takataka.
Imeandikwa na Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.