Ndoa Ya Profesa Kapuya ‘FarasI’ Wa Kushutumu Uislamu

Mitandao ya kijamii imesheheni vidio fupi (clip) ya sherehe ya ndoa ya Profesa Juma Athumani Kapuya (74) Mbunge wa zamani wa jimbo la Urambo, pia aliyewahi kushika nyadhifa kubwa mbalimbali katika serikali ikiwemo uwaziri katika elimu, ulinzi, kazi, michezo nk.

Mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii umewafanya baadhi kuambatanisha na dharau na kebehi kwa ndoa hiyo. Hoja yao ni kutokana na tofauti kubwa ya kiumri iliyopo baina ya Profesa na binti aliyemuowa Mwajuma Mwinko (25) ambapo tofauti baina yao ni umri wa miaka 49.

Mjadala wa ndoa hii umewateka hata baadhi ya wale wanaodai kuamini demokrasia na dhana ya ‘uhuru binafsi’, baadhi wanakosoa kijanja, lakini wengine wamekuwa kifuambele kwa ujasiri wakijisahaulisha na kuiweka kando dhana hiyo ya ‘uhuru binafsi’ wanayoiamini, hadi kuambatanisha pia na sura ya chuki ya kidini. Cha Ajabu ! ni kuwa Profesa Kapuya hakukosea kwa mujibu wa Uislamu, sheria za nchi, wala kwa mtazamo wa dhana ya ‘uhuru binafsi’ katika demokrasia, ambayo ni nguzo miongoni mwa nguzo za demokrasia.

Ndoa za tofauti kubwa ya kiumri ni jambo lipo na maarufu, kamwe halikuasisiwa na Profesa Kapuya, ni jambo maarufu katika jamii mbalimbali hususan za kiafrika, zikitekelezwa na wengi miongoni mwa hata wasiokuwa Waislamu pia. Mfano hai mzee na Mkurugenzi wa kampuni za IPP Reginald Mengi mnamo mwaka 2015 alimuoa aliyekuwa msanii Jacqueline Ntuyabaliwe. Pamoja na tofauti yao kiumri ambapo Mzee Mengi ana umri wa 75 na mkewe akiwa na miaka 41, hata hivyo Mzee Mengi alijinasibu kwamba ndoa yao na mkewe inasonga mbele raha mustarehe:

“Ananipenda sana (mke wangu), ananipikia, anafua nguo zangu kwa mikono yake na sio kwa mashine ya kufulia, ananiheshimu, na anajua nafasi yangu kama mwanamume na mume, na yeye anajua nafasi yake kama mwanamke na mke….” https://informationcradle.com/africa/reginald-mengi/

Ukosoaji na kebehi kufuatia ndoa ya Profesa Kapuya kamwe haukulengwa kwake binafsi, bali ni matokeo na athari ya kampeni ya kimataifa ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, kiasi cha kampeni hii kuwatia upofu hata wale wanaonekana kuwa ni mufakirina/wanafikra katika jamii, ambao baadhi wanaonekana hata kukhalifu/kupingana na fikra wanazoziamini, kama vile fikra ya ‘uhuru binafsi’. Matokeo yake wamedandia tukio hili kuchochea chuki zaidi na kuonesha kama inavyopigiwa debe na nchi za magharibi na wakala wao kwamba Uislamu ni dini ya ‘kishenzi’ na wafuasi wake wanafanya ‘ushenzi’.

Makala hii ipo zaidi kuweka sawa mambo kwa mujibu wa Uislamu, ukiwa mfumo kamili wa maisha uliokuja na masuluhisho katika kila sekta ya maisha ya mwanadamu, na kamwe haipo kujadili masuala ya kibinafsi.
Uislamu unamuangazia mwanadamu kwa namna ya kuwafikiana na maumbile yake. Haumkwazi katika mambo, wala haumpi fursa ya kuruka mipaka kuwakwaza wengine, bali unaweka mizania sawa iwe ni kwa nafsi yake au kwa jamii iliyomzunguuka.

Aidha, Uislamu unatambua mwanadamu kuwa ana mahitajio ya kibailogia yanayohitaji kushibishwa kama kuhitajia kwake maji, chakula, hewa nk. Pia Uislamu unatambua kuwa mwanadamu ana hisia za kimaumbile (instincts) zinazohitaji kushibishwa ikiwemo hisia ya kuendeleza kizazi. Hii ndio humsukukuma mwanamume na mwanamke kupendana na kuibua hisia ya kutaka kukidhi matamanio yao kijnsia.

Kwa kulitambua hilo, Uislamu kamwe haukumbana mwanadamu kama ulivyofanya ukiristo wa kumtia mwanadamu kitanzi kinachoitwa ‘utawa’ aishi bila ya kuoa au kuolewa, wala haukumuachia huria akidhi matamanio yake kama mnyama kama wanavyotuhubiria wanademokrasia kwa kudandia kisingizio cha ‘uhuru binafsi’. Kwa sababu kumuachia mwanadamu kukidhi matamanio yake bila ya nidhamu thabiti kutapelekea kvuruga muundombinu wa kijamii katika suala la urathi, uwalii, huduma za watoto na hata kupelekea kujenga chuki baina ya wanadamu nk.

Hivyo, Uislamu ukaona utatuzi pekee kwa hisia hiyo ya kuendeleza kizazi na kukidhi matamanio ya kijinsia ni ndoa, na ndoa yenyewe ukaruhusu zaidi ya mke mmoja, pia ukaruhusu talaka, na sio pingu ya maisha. Kwa kuwa kuna mazingira huwa suluhisho la kurekebisha hali baina ya wanandoa ni kuachana kabisa, baada ya kushindikana hatua mbali mbali za kuokoa ndoa husika.

Uislamu umeweka vipimo vingi vya kisheria na kwa ufafanuzi katika utekelezaji wa suala la ndoa, hayo yameelezwa kwa urefu katika fiqhi ya Kiislamu. Amma suala la mke au mume kumzidi umri mwenzake kamwe sio jambo kamwe linalozingatiwa kisheria, almuradi wanaoowana ni balegh. Labda hapa tuulize swali, jee ikiwa mwanamume mkubwa kiumri, au mwanamke mkubwa kiumri wametokea kupendana baina yao, jee wafanye nini ili kukidhi kiu yao ya mapenzi? Bila ya shaka kama sio ndoa watatumbukia katika shimo la zinaa!! Hili ni jambo la ajabu ya mwaka, ni vipi inashutumiwa ndoa na kutengeneza mazingira kwa ajili ya zinaa !!! Pamoja na ukweli kwamba ndoa ni jambo adhimu linalokubalilka na kuhimizwa na jamii na dini zote.

Uislamu umehimiza ndoa ili kuongeza kizazi, kukidhi matamanio na kujenga ustawi mwema baina ya wanadamu na ukaweka ufafanuzi wa kutosha ambao ni maarufu kwa Waislamu kushikamana nao katika utekelezaji wake. Amma kwa wasiokuwa Waislamu wanapohisi kuwa Waislamu wamekwenda kombo katika utekelezaji wa jambo lolote katika Uislamu, wanachopaswa kufanya amma ni kuwaachia Waislamu watende kwa mujibu wa dini yao, au kukaribisha mjadala wa kistaarabu juu ya misingi ya kiimani. Kama kujadili uwepo wa Mwenyezi Mungu, ukweli wa ujumbe wa Mtume SAAW, ukweli juu ya Quran nk.

Kwa kuwa Waislamu wanapotekeleza jambo lolote iwe ndoa au jengine huwa wanatekeleza kwa mujibu wa Quran na Sunna (Mtume), na kwa wasiokuwa Waislamu kwa kuwa wao hawayaamini yanayotokamana vyanzo hivyo, walipaswa kwanza wahoji uhalali wa vyanzo hivyo kwa hoja za kiakili

Tukio kama hili ni vyema kwa wasiokuwa Waislamu kulitumia katika kujadili misingi ya Uislamu kwa njia ya hoja za kiakili ili waweze kuona udhati wa Uislamu katika sura ya upana wake kiuadilifu kinyume na unavyoneshwa na maadui.

Risala ya Wiki No. 30

Jumada al-Thanni 1440 Hijri / Februari 2019 Miladi

14 Jumada al-Thanni 1440 Hijri | 19-02- 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.