Nasaha Tukufu za Mtume (Saaw) Kuhusu Mwezi wa Ramadhani

ﺑﺴﻢ ﷲ ﺍﻟﺮﺣﻤﻦ ﺍﻟﺮﺣﻴﻢ

Imam Ali Ra. Amesema: Mtume SAAW alikhutubia katika ijumaa ya mwisho wa mwezi wa Shaaban, na katika khutba hiyo akaeleza haya yafuatayo:

“Enyi watu! Kwa hakika umekujilieni mwezi wa Allah kwa Baraka, Rehma na Maghfira.

Ni mwezi  ambao mbele ya Allah ni bora zaidi kuliko miezi yote, na siku zake ni  bora zaidi kuliko siku zote, na usiku wake ni bora zaidi kuliko usiku wote, na saa zake ni bora zaidi kuliko saa zote.

Ni mwezi mnaoalikwa kuwa wageni wa Allah, na mnakuwa ni watu wa kukirimiwa na Mwenyezi Mungu.

(Katika mwezi huu) pumzi zenu ni sawa na kuleta tasbihi, usingizi wenu ni ibada, amali zenu ni maqbul na dua zenu ndani ya mwezi huu hujibiwa.

Basi muombeni Mwenyezi Mungu Mola wenu kwa nia safi na kwa moyo uliotoharika Akupeni tawfiq ya kufunga na kusoma kitabu chake (ndani ya mwezi huu.)

Kwa hakika mtu muovu ni yule atakaekosa maghfira katika mwezi huu mtukufu.

(Kwa mwezi huu) kumbukeni kwa njaa yenu na kiu yenu, njaa na kiu ya Siku ya Kiama.

Na toeni swadaka kwa mafakiri wenu na masikini wenu, na waheshimuni wakumbwa wenu, na warehemuni wadogo wenu, na waangalieni jamaa zenu na chungeni ndimi zenu.

Yafumbeni macho yenu kwa yale yasiyoruhusiwa kutazama, na yazibeni masikio yenu kwa yasiyoruhusiwa kusikia.

Wahurumieni mayatima wa watu, ili mayatima wenu nao wahurumiwe pia.Tubuni kwa dhambi zenu. Nyanyueni mikono yenu kuomba dua wakati wa sala zenu, kwani wakati huo saa zake ni bora zaidi kuliko saa zote, ambazo Mwenyezi Mungu huwaangalia waja wake kwa Rehma.

Huwajibu wanaomuomba kwa siri, na Huwaitikia wanaomnadi, na Huwajibu dua zao wanapomuomba”.

Enyi watu!  Kwa hakika nafsi zenu zimewekwa rehani kwa mali zenu, basi zikomboeni kwa kuomba kwenu msamaha.

Na migongo yenu ni mizito (kwa dhambi) basi punguzeni kwa kurefusha kusujudu.

Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ambae kudhikiriwa Utukufu wake ameapa kwa Utukufu Wake kwamba, Hatawaadhibu wanaosali na wanaosujudu, na kwamba Hatawatishia moto, siku watakayosimamishwa watu mbele ya Mola wa ulimwengu.

Enyi watu! mwenye kumfuturisha Muumini aliefunga miongoni mwenu katika mwezi huu, thawabu zake ni kama kumwacha huru mtumwa mmoja, na kusamehewa katika dhambi zake zilizopita.

Pakasemwa Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Si kila mmoja wetu ana uwezo (wa kumfuturisha)? Mtume akajibu ogopeni moto hata kwa nusu ya kokwa ya tende, ogopeni moto hata kwa funda la maji.”

#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Maoni hayajaruhusiwa.