Nasaha Tukufu Kwa Mahujaji na Waislamu Wote
Siku chache zijazo baadhi ya Waislamu kutoka Mashariki na Magharibi ya ulimwengu wataanza ibada tukufu ya Hijja ndani ya mji mtukufu wa Makka. Ibada ambayo ni faradhi kwa kila Muislamu mwenye uwezo.
Kwa wanaobahatika kutekeleza ibada hii hupata fursa adhimu ya kuizuru na kufanya ibada katika nyumba tukufu ya mwanzo iliyoteuliwa na Allah Taala:
اِنَّ اَوَّلَ بَیۡتٍ وُّضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِیۡ بِبَکَّۃَ مُبٰرَكًا وَّہُدًی لِّلْعٰلَمِیۡنَ ﴿ۚ۹۶﴾
“Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka (Makka), iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote” (TMQ 3:96)
Ibada ya Hijja inatufunza kujizatiti vilivyo na majukumu ya Uislamu, kujitolea muhanga, kujifunga vilivyo na kipimo chetu cha halali na haramu katika chumo na matendo yetu, kupambana na kila taratibu ya kishetwani nk.
Aidha, ibada hii hutukumbusha uwajibu mkubwa wa kuishi chini ya bendera moja ya dola ya Kiislamu ya Khilafah na pia uwajibu wa kulinda na kutetea mshikamano wa kweli kwa Umma wetu, kwa Waislamu wa pembe moja ya dunia kujali na kushughulikia kwa kupambana kuondoa mashaka na misiba inayowasibu Waislamu sehemu mbali mbali duniani. Kama dhulma inayotendwa na mtawala kafir Bashar Assad kwa ndugu zetu wa Syria pia yanayojiri ya uonevu ndani ya Yemen, Somalia, Afghanistan, Iraq, Burma, China nk. Kwa kuwa kimaumbile Umma huu ni Umma mmoja usiogawanyika milele.
Katika zama tukufu za makhalifa, Umma wa Kiislamu ndani ya hijja ulipewa khutuba zenye risala za ukombozi na kuoneshwa suluhisho la matatizo kwa mujibu wa Quran na Sunna tofauti na hali ya leo ambapo serikali ya Saudia kuwahi kuwalingania mahujaji fikra za kizalendo, dini mseto na kuwaonesha Waislamu suluhisho kinyume na Uislamu kama kutoka Umoja wa Mataifa (UN) nk.
Umma wetu leo umetiwa uzito, ugumu na vikwazo visivyokubalika katika utekelezaji wa hijja. Urasimu wa ruhusa ati ‘viza’, huduma duni, na udhaifu katika mchakato mzima wa utekelezaji wake. Baya zaidi uchache wa masiku wanayoruhusiwa Waislamu kubakia ndani ya mji mtukufu, na yakimalizika masiku hayo machache hufukuzwa kwa idhilali kana kwamba wageni au wakimbizi wasio na haki na mji mtukufu ambao ni kwa ajili ya Waislamu wote wa mbali na wa karibu na kwa wakati wote.
Kama haitoshi Ufalme wa nchi hiyo kwa jeuri hutawanya matangazo ya kifedhuli, dharau na vitisho kwa watakaozidisha hata siku chache! Hii ni kwa sababu hijja leo haisimamiwi rasmi na dola ya Kiislamu ya Khilafah kama ilivyokuwa zama za nuru za makhalifa. Na badala yake husimamiwa kwa mapungufu makubwa na utawala dhalimu wa kitwaghuti na kuhudumiwa na vijumuiya binafsi ambavyo baadhi yao hata havina sifa, uwezo wala uaminifu, zaidi ya kujitajrisha.
Hali hii ni changamoto kwetu Waislamu sote ya kufanya kazi ya kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah ili isimamie ibada hii ipasavyo pamoja na ibada nyengine zote.
Tunamuomba Allah Taala Awawezeshe mahujaji wetu kutekeleza ibada hii na kufikia daraja ya kutakabaliwa/hajj-mabroor, pia Tunamuomba Yeye kuwawezesha Waislamu wengine kupata fursa adhimu ya kutekeleza ibada hii kabla ya kuondoka duniani.
Amiin
Maoni hayajaruhusiwa.