Nane Nane: Siku ya Msiba kwa Kilimo

Tarehe nane Agosti kila mwaka Tanzania huwa ni ‘Siku ya Wakulima’ inayoambatana na maonesho makubwa ya kilimo maarufu ‘nane nane’.
Maadhimisho hayo yaliasisiwa tangu mwaka 1977 kama sabasaba kisha kubadilishwa na kuwa nane nane. Maonesho haya yameendelea kufanyika kila mwaka yakivuruga fedha nyingi .

Kilimo kinaajiri 67% ya Watanzania, kinachangia 30% ya pato la taifa karibia theluthi ya pato la zima, kinatoa 100% ya chakula cha nchi na kinatoa 65% ya malighafi za viwanda vya Tanzania (FYDP2 na Hali ya Uchumi 2017). Hivyo kilimo ni suala nyeti kwa watu na maendeleo.

Pamoja na umuhimu wake huo serikali ya Tanzania kama zilivyo serikali nyingine za kibepari hawajali wanakipa nafasi ndogo mno. Bajeti iliyoombwa na Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2015/2016 ilikuwa ni bilioni 353, mwaka 2016/2017 ilikuwa bilioni 275.06 na mwaka 2017/2018 ilikuwa bilioni 267.8 na mwaka 2018/2019 iliomba bilioni 170.27 sawa na 0.52% ya bajeti nzima. Ilipaswa kilimo kupewa kipaumbele na kutengewa pesa za kutosha badala pesa hizo kidogo mno.

Hali hii ya kupuuzwa kilimo imepelekea kushuka kwa kasi hali ya ukuaji wa sekta hii nyeti, ambapo mwaka 2014 ukuaji ulikuwa 3.4%, mwaka 2015 ilikuwa 2.3%, mwaka 2016 ilikuwa 2.1% na mwaka 2017 ilikuwa 1.3%. Hii inaonesha hali ya mdororo mkubwa wa sekta hii muhimu huku serikali ikisema eti inataka nchi kuwa ya viwanda.

Hatua hii ya serikali kwa kilimo inathibitisha kuwa haina mpango na wananchi kwa kupuuza sekta inayotegemewa na wananchi wengi zaidi na badala yake kuwekeza katika sekta zinazofaidisha wachache.

Fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo kwa mwaka 2016/2017 ilikuwa ni bilioni 101.5 na zilizotolewa zilikuwa bilioni 2.25 sawa na 2.2%, mwaka 2017/2018 zilitengwa bilioni 150.2 lakini zilizotolewa bilioni 16.5 sawa na 11% Vipi kilimo kitakuwa sekta yenye kuleta tija?

Kiuhalisia kilimo katika hali kama hiyo hakiwezi kukua na kuleta tija kubwa kwa kuondoa njaa na mabalaa mengine kutokana na sera mbovu na usimamizi mbaya.

Uislamu chini ya dola ya Khilafah Rashidah utakuza kilimo na kuthamini wakulima kwa sera na usimamizi thabiti. Dola itawawezesha wakulima kwa mikopo isiyo na riba, itaondoa kodi zilizojazana sasa hivi za kumnyonya mkulima. Pia itaimarisha miundombinu ya usafiri, kuvifanya vyanzo vya maji kuwa milki ya Ummah ili kusahilisha mifumo ya umwagiliaji. Bila ya kutaja kuwaachia wakulima huria kuuza mazao yao kwa bei zao na wanapotaka, kwa sharti tu jambo hilo halitogongana na sera za nje za dola.

07 Agosti 2018
Said Bitomwa

Maoni hayajaruhusiwa.