Mtume (Saaw) Katuonesha: Misikiti Kituo cha Harakati za Kimwamko

Alhamdulillah tupo katika mwezi wa Rab ul-awwal (Mfungo Sita), mwezi ambao alizaliwa Rasulullah SAW. Mtume, Mwalimu, Kiongozi na Mlezi wa Ummah huu.
Ni kawaida iliyozoeleka katika dunia kwa Waislamu kuyaadhimisha masiku ya mwezi huu ikiwa ni kumkumbuka Mtume wetu SAW na kuonesha upendo kwake. Wapo ambao hukusanyika katika mitaa, vijiji na hata vitongoji wakisoma na kughani nashiid zenye sifa mbalimbali za Mtume SAW, wengine hufanya makongamano na mihadhara, bali pia khutba za ijumaa husheheni maelezo ya ukumbusho unaonasibiiana na hili. Mradi kila mmoja ana namna yake ya kuyaenzi haya masiku.

Ni muhimu kukumbushana kwamba dini yetu ya Uislamu ni mfumo kamili na sahihi wa maisha yetu wanaadam. Umeundwa na aqidah, sharia/nidhamu, hisia zinazotuunganisha sote pamoja tunaomuamini Mungu Muumba na Mtume SAAW. Na aqidah ikawa ndiyo msingi na chimbuko la kila jambo la Muislamu, iwe kiimani, kiuchumi, kijamii, kisiasa nk.

Mtume SAW Ameletwa kwetu kwa ajili ya kuelezea kwa maneno na kivitendo na kuisimamia aqidah ya Uislamu katika maisha yote. Na aliiishi kwa aqidah hii ili nasi tuishi vivyo hivyo, kama alivyowahi kutamka: ‘swalini kama muunavyo niona mimi nikiswali’. Yaani tuishi katika kufuata taratibu za kila jambo kama alivyokuwa akifanya yeye SAAW. Ndipo Allah SW Akatwambia katika Qur’an kwa wale wanaotaka kufaulu katika maisha haya (na bila shaka sote ni wahitaji wa hilo) kwamba tuna kiigizo chema kutoka kwa Mtume wa Mwenye Mungu…

Alipopewa utume, Mtume SAW Makka ilikuwa zaidi ya ilivyo jamii yetu zama hizi kwa uovu, uchafu na kila baya. Mpaka anafariki aliacha jamii iliyokuwa namba moja kwa ustaarabu na heshima duniani kuliko zote.

Uislamu ulikuwa ni mfumo mkuu duniani na wenye nguvu ya kuathiri (influence) mifumo na jamii nyingine. Alijua Mtume SAAW haiwezekani kuibadili jamii kufikia muamko wa kimaendeleo jumla na mahsusi bila kuwa pamoja, bila kufanya kazi kama kundi ili kuwaamsha waliolala na kuwafumbua macho waliosinzia.

Hivyo, akatumia mbinu za kuwakusanya watu baada ya ulinganizi wa mmoja mmoja ilikuwa na watu wenye fikra na ufahamu unaofanana. Kwa kuwa utatuzi wa masuala ya jamii ni jambo la kisiasa alihitaji SAW kupata nguvu ya kidola, nayo ni kwa kupewa na wale unaotaka kuwaongoza.
Madina ikawa sehemu muafaka. Aliutumia msikiti kwanza, kwa kazi yake ya asili ya kuswali swala tano na nyingine, lakini fursa ya msikiti iliboreshwa kuwa nyenzo ya harakati za ukombozi wa kifikra na kimfumo.

Waliokutana misikitini walijadili ukubwa na nafasi ya Uislamu na namna ya kuifikia hadhi aliyoikadiria Allah SW kwa dini hii. Mtume SAW Aliongoza swala kisha akaongoza mapambano ya kivitendo katika viwanja vya vita lakini mikakati ikiwa katika misikiti ambapo walipatikana Waislamu kwa wingi na umoja wao. Watu walikuwa wanahamasika kwenda misikitini maana zaidi ya ujira wa swala walipata mwamko wa dini yao uliowafanya waithamini, kuipenda na kuilinda katika hali zote.
Misikiti ilikuwa madrasa, kukifundishwa Uislamu kijumla kama mfumo wa maisha ukikusanya ibada kwa upana wake, yaani utii kwa maamrisho yote na makatazo yote ya Allah SW. Ikawa pia ni vituo vya kukusanywa na kusaidiwa wenye shida na waliopatwa na changamoto katika mapambano dhidi ya mfumo pinzani yaani ukafiri nk.

Leo misikiti ni mingi sana na kiidadi Waislamu ni wengi sana, lakini ‘sio’ tena misikiti ile ya Mtume SAW.
Misikiti michache leo ndio hubeba jukumu hilo ipasavyo la kukumbusha Waislamu nafasi na hadhi yao kwa Ummah, kuhadharishwa juu ya uadui, na kuelekeza nguvu na juhudi zao katika kupambana nao. Misikiti mingi leo hakutajwi tena sifa za Mtume SAW za kuleta muamko na mabadiliko chanya katika Ummah, bali ni kuulaza Ummah na kuuondoa katika mstari sahihi.

Kwa masikitiko leo baadhi ya misikiti ni sehemu ya fitna ya Ummah. Ndipo kunapo ibuliwa sintofahamu za kutengenezwa baina ya Waislamu, na kundi moja kuungana na viongozi wa mfumo pinzani kulidhibiti kundi la pilli. Ndipo serikali zinapowakamatia na kuwadhalilisha masheikh wengi na Waislamu jumla lakini kwa msaada wa Waislamu wenzao.
Masiku haya ya mazazi ya Mtume SAW yaturejeshe katika da’awah yake, tuifahamu na kuiishi ili tufanikiwe kama waliotangulia.

Tutumie fursa, majukwaa na mimbari vyema kuunganisha Ummah na kuwapa Waislamu muamko na sio kuulaza na kuuvuruga Ummah ambako ni kuwasaidia maadui wa Uislamu.
#MuhammadNuruYetuKigezoChetu

Abu Nuthutaq Hamza
Risala ya Wiki No. 61
23 Rabi’ al-awwal 1441 Hijri 20/11/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.