Miradi Mikubwa ya Dunia ya Tatu: Wanufaikaji Halisi ni Makampuni ya Kibepari

Habari:

Vyombo vya habari Tanzania vimeripoti kuhusu ombi la Rais Magufuli la kuharakisha ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga. Ombi hilo alilitoa wakati akimkaribisha Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, ambapo aliwataka mawaziri kutoka Uganda na Tanzania kuusimamia vyema mradi huo unaogharimu mabilioni ya dola za kimarekani unaotarajiwa kumalizika mwaka kesho.

Maoni:

Rais Magufuli alihimiza kwamba ujenzi wa mradi huo uongeze kasi kwa kuwa ni muhimu kwa wananchi wa nchi zote mbili. Mradi huo wa bomba la kusafirishia mafuta ghafi kutoka Uganda hadi kaskazini mashariki ya Tanzania ulianza mwaka 2016 na kutarajiwa kumaliza kwa miaka mitatu kwa bajeti ya dola za kimarekani bilioni 4. unadhamiriwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka visima vya mafuta vya Uganda kuja bandari ya Tanga, Tanzania katika Bahari ya Hindi.

Inakadiriwa kuwa Uganda ina akiba ya mapipa bilioni 6.5 ya mafuta, miongoni mwake kiasi cha mapipa bilioni 2.2 yatachimbwa. Pamoja na mafuta hayo kutumika kwa katika eneo, lakini mengi yatasafirishwa kwa bomba hilo kwenda nje ya nchi kwa kutumia bomba lililopo katika mwambao wa Bahari ya Hindi.

Pamoja na mradi huu kuonekana kuwa ni muhimu na una faida nyingi kwa raia wa nchi hizi mbili, uhalisia ni kwamba kuna kidogo kitakachovunwa, kwa kuwa makampuni ya kimataifa ya kibepari yana gawio kubwa sana (shares). Kwani kampuni ya Total ya Ufaransa ina 35%, kampuni ya China National Offshore Oil Corporation ina 35%, Tullow Oil ya Uingereza ina 10%, ilhali Uganda mwenye mali ni 15% na Tanzania ina 05% tu.

Ingawaje serikali za (nchi changa) daima zimekuwa zikiwajaza raia wake ahadi na matarajio mengi mazuri kwamba miradi hii ni chachu katika kusukuma maendeleo na ustawi wa raia, kama vile kupatikana huduma bora za kijamii kama afya, elimu na ajira, lakini kwa hakika hazileti matunda yanayotarajiwa.

Serikali huonekana kufurahia miradi kama hii kwani hujiongezea makusanyo ya kodi za aina mbalimbali, kama vile kodi za mishahara (payee), kodi za uwekezaji na ushuru wa forodha ambapo mapato hayo hunufaisha wachache kama tabaka la wanasisa wakubwa na watumishi wenye vyeo vikubwa kwa kulipana mishahara minono, marupurupu, motisha na vifuta jasho vyengine ilhali watumishi wa Umma wanaendelea kudhikika kwa mishahara ya ‘kijungu mwiko’ (isiyowatosha )

Japo serikali za nchi changa zinaonekana huwekeza katika huduma za kijamii kama hospitali na mashule, lakini kiuhalisia huduma hizi zinakuwa duni na chini ya kiwango zikikosa vifaa muhimu, ambazo humalizia kutumiwa na wanyonge na wenye vipato vya chini, ilhali wanasiasa na matajiri kamwe hawatumii shule wala hospitali za Umma.

Wafaidika wakuu wa miradi kama hii ni wawekezaji (mabepari) ambao huingia mikataba na serikali mikataba ya misingi ya dhulma na isiyozingatia usawa. Kazi nyingi za hatari na duni hufanywa na wazawa ambao ni wanyonge na hudhulumiwa sana na wawekezaji, na pale unapoibuka mgogoro wa mahala pa kazi, mara nyingi serikali huwa upande wa wawekezaji. Mfano hai ni nchi tajiri kwa madini ya Afrika ya Kusini ambayo raia wake wanaishi katika umasikini wa kutupwa, wachimba migodi wa nchi hiyo wakisimama kudai haki zao, wawekezaji na serikali hushirikiana kwa pamoja kuwaua, kama ilivyotokea tarehe 17 Agosti 2012 walipouliwa wachimba migodi waliogoma wa mgodi wa Lonmin, kwa kupigwa risasi na polisi, ambapo 34 waliuwawa na 78 kujeruhiwa.

Kwa kawaida miradi hii katika maeneo inapoanzishwa mara nyingi mali za wananchi kama ardhi, viwanja, mazao, mashamba hata nyumba zao hufilisiwa. Na ikiwa serikali au wawekezaji wanaamua kuzilipia fidia mali hizo, mara nyingi hufidia malipo machache yasiyolingana na thamani ya mali hizo.

Bila ya kusahau janga la kimazingira, ambapo miradi hiyo huzua nakama kubwa katika upande wa kilimo pamoja na afya za wananchi. Dunia bado inakumbuka qadhia ya mauaji ya dhulma ndani tarehe 10 Novemba 1996 aliyofanyiwa mwandishi na mzalishaii vipindi vya TV wa Nigeria Ken Saro-Wiwa na wenzake wanane kwa kuupinga uharibifu wa kimazingira uliotendwa na kampuni ya kidachi ya Royal Dutch Shell iliyoiharibu ardhi na afya za wakazi wa Ukanda wa Niger Delta nchini Nigeria.

Uslamu unaruhusu watu binafsi, kampuni au serikali kuwekeza kwa miradi mbali mbali mikubwa kama ujenzi, viwanda na usafiri lakini inakataza miradi hiyo kuwa na ajenda ya kimfumo ya unyonyaji na ukoloni.

Amma kuhusu miradi inayohusisha mali za Umma kama madini, nishati ya mafuta nk. hiyo inakatazwa moja kwa moja kumiliki, kama Mtume SAAW alivyosema:

«المسلمون شركاء في ثلاثة في الماء والكلإ والنار»

“Waislamu ni washirika katika mambo matatu, maji, moto na malisho ”.

Mbali na hayo pia Khalifah ana wajibu wa kutoa huduma zote za kijamii na mahitaji msingi kwa raia wote (wasiojimudu), wawe Waislamu au sio Waislamu. Huduma hizo sio kwa ajili ya kupata faida, bali ni kutokana kuwa ni jukumu juu yake.

Imeandikwa na Ali Amour

Mjumbe wa Afisi ya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.