Miaka Mia Moja ya Jeshi la Polisi Hakuna cha Kujivunia

Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza maadhimisho ya kutimia miaka mia moja tangu kuasisiwa kwake.
Ukubwa huu wa umri wa jeshi hili tangu kuundwa kwake si jambo la kujifakhiri kutokana na rekodi mbaya ya taasisi hii hususan katika miaka ya karibuni.

Licha ya Jeshi la Polisi kudai kwamba jukumu lake msingi ni kulinda na kuhifadhi usalama wa maisha ya watu, mali na heshima zao, ukweli uko tofauti, na hilo ni kaulimbiu isiyo na matendo. Jeshi hilo limewadhuru wengi katika raia jumla na jamii ya Waislamu ndio muhanga mkubwa zaidi

Tunashuhudia maumivu endelevu kila siku, kama wimbi kubwa la utekwaji, mauaji, mateso ya wahadhiri Kiislamu na wanaharakati, raia wa kawaida, wanasiasa, watu maarufu, wafanyabiashara, waandishi wa habari nk.

Pia kuna wimbi la watu kutoweka kwa mamia kwa kunyakuliwa na kutekwa katika Wilaya za Kibiti na Mkuranga ndani ya Mkoa wa Pwani na mpaka sasa wahanga hao hawajuulikani walipo. Bila ya kusahau kuonekana maiti zinazoelea katika Mto Ruvu na mwambao ya Bahari ya Hindi na uwepo wa mahandaki maalumu ya mateso chini Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi kwa ajili ya kutesea watuhumiwa wa Kiislamu (wa ugaidi) na watuhumiwa wengine. Jambo ambalo limeshapigiwa kelele mara nyingi.

Haya yote ni kielelezo cha wazi, sio tu cha udhaifu na kushindwa kwa vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi kulinda maisha ya watu, mali na heshima zao, bali ni dhihirisho la uwepo wa kiburi cha hali ya juu kwa taasisi hii inayoendeshwa kwa fedha za walipa kodi.

وَجُنُودُهُ فِي الأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ إِلَيْنَا لاَ يُرْجَعُونَ﴾ ﴿وَاسْتَكْبَرَ هُوَ

“Na alipanda kiburi yeye (Firaun) na majeshi yake katika nchi bila ya haki, na wakadhani kwamba hawatorejeshwa kwetu ” (Al-Qas’as : 39)

﴿وَأَتْبَعْنَاهُمْ فِي هَذِهِ الدُّنْيَا لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ هُمْ مِنَ الْمَقْبُوحِينَ﴾
“ Na tukawafuatishia laana katika dunia hii , na Siku ya Kiyama watakuwa miongoni mwa watu waovu kabisa” (Al-Qas’as : 42)

Jeshi la Polisi kama vilivyo vyombo vyengine vya dola kama jeshi na mashirika ya kijasusi ulimwenguni kote chini ya mfumo wa ubepari wa kisekula, yanafanya kazi kwa misingi ya ubaguzi, ukatili, ushenzi, mabavu na hali ya kukosa ubinadamu, bila hata ya kujali misingi ya maadili waliyojiwekea wenyewe ambayo hudai kushikamana nayo. Na hii ni kwa sababu yanafanya kazi chini ya nidhamu/ system inayotokamana na akili finyu ya kibinadamu isiyokuwa na haja ya thamani ya kiroho.

Kitu pekee cha kukabiliana na maumivu haya na kuzuiya kiburi cha vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi, ni kwa ulimwengu kuondoa mfumo wa kibepari kwa mbadala wa mfumo wa uadilifu na ufafanuzi wa Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah.

Masoud Msellem

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Kumb: 1440/07

Alkhamis 28 Dhul-Hijja 1440 Hijri

29 Agosti 2019

Maoni hayajaruhusiwa.