Mgongano Wa Kanisa Na Wanasayansi Zama Za Giza Huko Ulaya Ndio Zao La Itikadi Ya Kutenganishwa Dini Na Serikali Zama Hizi
Hali ya kutisha iliyoondoa mahusiano yote kati ya Dini na maisha huko Ulaya, hatimaye kutenganisha itikadi ya Dini na serikali ilichochewa na mapadri wa kanisa wakishirikiana na watawala wa dola ya Kirumi. Hali hiyo ilianzia pale Kanisa lilipohodhi peke yake haki ya kuielewa na kuifafanua Biblia kwa kumkataza mtu yeyote nje ya makada wao kujaribu kuielewa na kuifahamu Biblia. Halafu kukafuatia kuingiza katika mafundisho ya Dini hiyo imani za kibubusa(dogmas) ambazo zilikuwa hazieleweki, hazikubaliki na wala haziaminiki.
Kanisa likazifanya imani hizo zisizoeleweka “mafumbo ya Mungu” au “ibada”. Mfano dhahiri ni imani ya kibubusa juu ya Ekaristi (Chakula cha jioni cha Bwana) imani ambayo ilipingwa na Martin Luther, John Calvin na Ulrich Swingli na kuanzisha madhehebu ya Waprotestanti.
Kanisa likashinikiza dai hili kwa wafuasi wake na likakataza mijadala yahoja kwa tishio la kutengwa.
Zaidi ya imani hizi potofu zilizoingizwa katika Dini hiyo zilizoandamana na kuwakataza watu kuzithibitisha katika Biblia (ambayo walizuiliwa kuifafanua), Kanisa likajiingiza katika kutoa ufafanuzi wa nadharia juu ya uhai na ulimwengu. Likaziunga mkono nadharia fulani fulani za kijiografia, kihistoria na kifizikia zilizokuwa maarufu wakati huo, nadharia ambazo zilijaa makosa na udhanifu mwingi na Kanisa likadai kuwa nadharia hizo hazihojiki, hazisahihishiki, hazipingiki na hazibadilishiki.
Mfano dhahiri ni kwa upande wa jiografia na sayansi ya maumbile ambapo walizipa habari hizi hadhi ya “utukufu wa kidini” na wakazifanya kuwa ni sehemu ya Dini na hivyo kila mtu lazima aamini na akikatae kilicho kinyume na habari hizo. Wakaandika vitabu juu yake na wakauita udhanifu huo wa jiografia ‘Jiografia ya Kikristo’ na wakaishikilia kwa jino na ukucha na kila asiyeamini udhanifu huo akaitwa mpagani”.
Mapandikizi ya Imani hizi yalianzisha mapambano yasiyofaa kati ya sayansi, na ‘Dini’, na hatimaye ‘Dini’ ilishindwa vibaya sana kwa sababu Ilikuwa ni Dini ambayo kweli na urongo na haki na batili vimechanganywa na hivyo watetezi wake wasingeweza kupata chochote isipokuwa kushindwa ambako hawakuweza tena kurudisha hadhi yao.
Yote hayo yalitokea katika kipindi ambacho hoja zilikuwa zikiibuka huko Ulaya na wanasayansi walikuwa wakianza kuvivunja vizingiti vya ‘Dini’, na kuikosoa jiografia ya Kikristo waziwazi pamoja na vitabu vyake vingine wakatangaza kutoamini kwao fikra hizo kuwa ni takatifu na wakaonesha ugunduzi wao kupitia majaribio yao. Hili likaamsha ghadhabu ya Kanisa na viongozi wao huko Ulaya wakawahesabu wanasayansi hao kuwa ni wapotofu na makafiri. Hivyo wakaimwaga damu yao na wakawanyang’anya mali zao kwa madai kuwa wanautetea Ukristo, na zikaanzishwa Mahakama za Uchunguzi ili kuwaadhibu wale ambao kwa maneno ya papa ‘wale makafiri na waasi waliotawanyika katika miji, nyumba, misitu, mapango na mashamba’.
Mahakama za Uchunguzi hazikupoteza muda na zikafanya kazi kwa mori na zikajitahidi zilivyoweza kumteketeza kila adui katika ulimwengu wa Kikristo. Wakaanzisha taasisi za wapelelezi katika nchi zote, wakichunguza kila mtu kwa msisitizo ambao ulimfanya mwanatheolojia mmoja wa Kikristo aseme, “hakuna mtu awezaye kuwa Mkristo na kufa katika hali ya kawaida”.
Inahisiwa kuwa walioangamizwa na mahakama hizi walifika elfu mia tatu, na kati ya hao elfu thelathini na mbili walichomwa moto wakiwa hai. Miongoni mwao alikuwepo mwanafizikia mashuhuri Bruno ambaye fikra zake juu ya uwingi wa ulimwengu zilighadhibisha kanisa kiasi ambacho walimwua bila kumwaga tone la damu. Hii ilikuwa na maana ya kumchoma moto akiwa hai! Alikuwepo pia mwanasayansi maarufu Galileo aliyeamini kuwa dunia inalizunguka jua na imani yake ilimgharimu uhai wake.
Mambo yalipofikia hatua hii, wasomi na wagunduzi walishindwa kuvumilia na wakatangaza uasi wao dhidi ya Kanisa, mapadri na dhidi ya wote wanaoshikilia ukale. Wakakipinga kila kilichohusiana nao iwe imani au elimu, sayansi au maadili. Wakajenga uadui kwanza na dini ya
Kikristo, halafu na dini zote bila kubagua; na mapambano kati ya wanasayansi na hoja dhidi ya viongozi wa Dini ya Kikristo yakawa ni mapambano kati ya sayansi na dini kwa ujumla. Wanamapinduzi wakahitimisha kuwa sayansi na Dini havipikiki chungu kimoja. Mtu ilimpasa achague moja na asuse jingine. Dini kwao ilileta kumbukizi za damu za mashahidi waliopoteza maisha yao kwa ajili ya sayansi na utafiti na kumbukizi za watu wasio na hatia waliouliwa kwa sababu ya ukatili wa mapadri na kwa sababu ya kutoamini kwao. Katika akili zao Dini ilileta taswira ya nyuso zilizosawajika, zenye ukali na mapaji ya uso yenye makunyazi, ghadhabu isiyo na subira na ujinga usio kiasi. Walichukizwa katika nyoyo zao na wakaamua kuchukia na kupigana dhidi ya Kanisa na kila walilowakilisha au walilohubiri. Vizazi vilivyofuata vilirithi hisia na kumbukizi hizi chungu”. . Kibaya zaidi ni matoekeo yake; kwani Ulaya yote ilipuuza au karibu kuikana kabisa Dini.
Hili lilikuwa pigo la mwisho kwa kanisa kwa sababu katika makosa makubwa waliyoyatenda mapadri wa Ulaya dhidi ya Dini ni kule kuingiza katika vitabu vyao vitakatifu baadhi ya nadharia za elimu ya kisayansi juu ya historia, jeografia na maumbile ya ulimwengu. Habari hizo za sayansi zilizoingizwa wakati huo zilionekana sahihi kabisa na ikadhaniwa kuwa ni kweli zisizo shaka na zisizoweza kutengulika.
Lakini walikosa ufahamu wa kuwa imani za kisayansi siku zote hujengwa juu ya msingi wa udhanifu (speculation), na hivyo ni rahisi kuweza kutenguliwa kwa majaribio mepesi tu ya kitafiti yatakayothibitisha udhaifu wake.
Pia makasisi hawa walitakiwa wajue kuwa kilele cha elimu ya utafiti wa kisayansi katika kipindi/zama fulani si kauli ya mwisho ya kukata (qatiy) na elimu ya kisayansi na utafiti haituami, kwa sababu upeo wa akili ya mwanadaamu daima huongezeka na hukua katika masuala ya utafiti na uvumbuzi..
Vilevile muhimu zaidi la kuwajuza ni kuwa lau kama Dini itajengwa juu ya msingi unaotokamana na ufahamu wa akili ya mwanaadamu, basi jengo hilo limesimama katika mchanga unaodidimia kwa sababu akili ya mwanadamu ina udhaifu na pia ina kikomo cha kufikiri.
Amma kupotoka kwa hawa wanasayansi na wanafalsafa ni kutokana na kule kushindwa kutofautisha Dini na wale waliohodhi uongozi wa Dini. Kwa vile Ukiristo (dini) huo kule Ulaya ndio ulikuwa ukiongoza mafundisho juu ya kuwepo kwa Mungu Muumba na kwa vile chuki ilishamea dhidi ya dini, wanafalsafa na wanasayansi wengi walioathiriwa na hali hiyo walijitoa kwenye dini na kujitenga nayo hivyo basi wakapatikana wakanushaji/wanaokana imani juu yakuwepo kwa Mungu Muumba.
Na Salim Abass
Mwanachama Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.