Mazingatio Ya Kurudi Khilafah Kutoka Vita Vya Tabuk
Rajab 9 Hijria
Katika purukushani za Vita vya Tabuk vilivyotokea mwezi kama huu wa Rajab , mwaka 9 hijria, ngamia wa mtukufu wa darja Mtume SAAW aitwae Al-Qas-waa alipotea. Masahaba wakajituma kwa jitihada kubwa kumtafuta kila mahala lakini hawakufanikiwa kumpata.
Wanafiki kama kawaida yao kwa haraka wakalidandia tukio hili kwa lengo la kumdhalilisha Mtume SAAW na kutia shaka Waislamu na Uislamu. Mmoja kati ya wanafiki hao kwa jina la Zayd Bin Lusayt akasema:
“Ni kiroja hiki…. Muhammad anasema ati ni Mtume na anasimulia mambo ya wahyi kutoka mbinguni lakini hajui hata alipo ngamia wake” (makubwa hayaa!!!!)
Matamshi haya ya kuudhi yalimfikia Mtume SAAW nae akajibu kwa kusema:
“Wallah ! Mimi najua kile tu Allah anachonijuza, siwezi kujua kingine chochote”.
Kisha papo hapo akaongeza Mtume SAAW kwa kutamka:
“Sasa Allah ameshanijuza kwamba Al-Qas-waa (ngamia wangu) yupo katika bonde baina ya hapa na mlima ule, kamba (hatamu) yake imekwama kwenye mti. Nendeni mkamlete kwangu”.
Masahaba walipokwenda mahala walipofahamishwa na Mtume SAAW wakamkuta yule ngamia, huku kamba yake ikiwa imekwama kwenye mti kama alivyotamka Mtume SAAW. Wakamchukuwa na kumleta kwa Mtume SAAW.
Mkasa huu na mithili yake unathibitisha kuwa, asili ya elimu ya ghaibu imo mikononi mwa Allah Taala. Lakini huwapa Mitume wake As. kiasi Atakacho, katika mambo Atakayo na katika wakati Atakao. Hayo Allah Taala hutenda kwa elimu ya Uungu wake.
Mtume SAAW kataja mambo mengi ya ghaibu/yaliyofichikana ambayo yametokea na hakuna lilokwenda kombo, na kamwe hayatokwenda kombo. Kwa kuwa hii huwa sio elimu au ujuzi wa yoyote, bali ni ujuzi wa Muumba wa mbingu na ardhi ambae elimu Yake imezingira kila kitu.
Kwa mfano, Mtume SAAW alitamka kuhusu kumuuwa kwa mkono wake Ubay bin Khalaf, kafiri mkubwa wa kiqureish, na akamuua kafiri huyo kwa mkono wake katika Vita vya Uhud.
Pia Mtume SAAW alibashiri kwa Suraqa bin Malik kupata kofia ya kikuku ya thamani (crown) ya mtawala wa Fursi, na ilipofunguliwa Bilad Fursi katika zama za Khilafah ya Umar ra. bishara hiyo ikatimu kama alivyobashiri.
Aidha, Mtume SAAW alibashiri kufunguliwa kwa mji wa Istanbul kwa kupitia mtu mwenye jina lake, na bishara hiyo ikasibu kwa Muhammad Al-Fathi. Haya ni machache katika mengi aliyobashiri Mtume SAAW, baadhi yameshatokea, na yaliyobaki yatatokea Inshaa Allah, kwa kuwa hii ni elimu ya Allah Taala ambayo haina shaka.
Zaidi ya hayo pia tukumbuke kuwa Mtume SAAW kabashiri kurudi tena utawala wa Kiislamu wa Khilafah kwa Manhaj ya Utume ( Khilafah ala Minhaj Nubuwah) baada ya mchafukuge na mashaka kutoka kwa watawala waovu na madhalimu katika biladi za Waislamu.
Kwa kuwa bishara zote asili ni elimu iliyofichikana kutoka kwa Allah Taala Ambayo kwa Rehma zake ametujuza sisi kidogo kupitia kwa mtukufu wa darja Mtume wetu SAAW, huwa ni wajibu katika upande wa kiaqida/kiimani, kuyaamini hayo kwa yaqini na kutuliza nyoyo zetu.
Licha ya kuwepo bishara hizo za kurudi Khilafah, tukumbuke imani yetu juu ya bishara hizo haina maana tukae tu, bali tunatakiwa na sharia tutende matendo fulani, basi huwa ni wajibu kuyatenda kama tuliyoamrishwa. Tuyatende kwa njia ya kisharia na kwa mbinu zisizokhalifu Uislamu. Na katika kujiri bishara tumwachie Allah Taala alete bishara zake kwa namna Atakavyo na muda Atakao.
Tuamini kwa yaqini kabisa kwamba yote tuliyobashiriwa yatatukia, amma ikiwa yanaingia akilini mwetu au tunaona hayaingii. Kwa kuwa hiyo ni elimu iliyofichikana kwetu.
Masoud Msellem
23/03/2019
#RajabFarajaKwaWalimwengu
Maoni hayajaruhusiwa.