Mazingatio Katika Uchaguzi Wa Marekani

بسم الله الرحمن الرحيم

Katika makala yetu tuliyoandika karibuni, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania yenye anuani : ‘kwanini katika nchi changa kuna vurugu katika uchaguzi’ katika sababu ya pili tulieleza ni kutokana na ndani ya nchi changa kukosekana taasisi thabiti kusimamia uchaguzi, licha ya uwepo ‘taasisi majina’ lakini udhati taasisi hizo huwa ni maamuzi ya mtu mmoja au wawili watatu.
Tukiunganisha hilo na uchaguzi unaoendelea Marekani, tunaona raisi Trump ambaye ndie mwenye mamlaka ya kuwa mtendaji mkuu wa muhimili wa serikali (executive) analalama kwamba kaibiwa kura na anapeleka kilio chake Mahakama ya Juu ya Marekani (Supreme Court). Labda hapa tujiulize ni raisi gani katika nchi changa anaweza kulialia kwamba kaibiwa kura katika chaguzi ? Vilio kama hivyo siku zote ni kwa vyama vya upinzani peke yao.
Watu wengi wanayachukulia malalamiko ya Trump kwa uoni finyu sana na kama kichekesho, kwa kuwa raisi Trump daima ni ‘jitu la vioja’. Lakini kwa upana, hatua hiyo ya Trump inaonesha wazi wazi mambo yafuatayo:
1. Raisi Trump hana mamlaka ya kuziamuru na kuzitumia taasisi za uchaguzi kwa maslahi yake.
2. Yale matamko ya raisi Trump ambayo watu wengi wameona kana kwamba yana ukweli kwamba Trump hata akishindwa uchaguzi hatotoka ikulu, hayana ukweli wala uhalisia wowote. Ni wazi Trump anaamini kwamba ili abakie ikulu anahitaji kushinda uchaguzi.
3. Kama raisi Trump anakusudia na kuamini kubakia ikulu hata akishindwa uchaguzi, mbona anakimbilia Mahakama ya Juu (Supreme Court) kuzuiya matokeo yasiendelee kutangazwa? Si angenyamaza tu, muda wa kutoka ikulu utakapofika asitoke?
Tunaposema nchi zenye kubeba mfumo zina taasisi ni kama hivi, haina maana kwamba hakuna matatizo, vurugu, changamoto nk. kwa kuwa hayo ni mambo ambayo huwezi kuepukika kwa wanadamu, na hususan kwa mfumo wao batil wa kibepari, lakini nchi huwa na nyenzo na taasisi zenye uwezo wa kukabiliana kwa kiwango cha juu na changamoto zinazoibuka. Na hiyo ndio tabia ya nchi iliyobeba mfumo, hata kama mfumo huo ni batil. Tabia ya mfumo hukupa muono mpana na kujenga utaasisi thabiti.
Marekani ni nchi iliyojengwa juu ya utaasisi, na sio mtu mmoja kuwa ndio taasisi kama nchi changa zilivyo. Katiba ya Marekani imempa raisi mamlaka fulani lakini imemfunga kwenye mabano na kumdhibiti.
Kwa mfano, raisi wa Marekani ndio Amiri Jeshi Mkuu, lakini ni Bunge la Congress ndilo lenye haki ya kutangaza vita, na kutafuta fedha kwa ajili ya vita hivyo. (Artcle I, Section VIII)
Aidha, raisi wa Marekani ana mamlaka ya kufunga mikataba mbali mbali, lakini mikataba hiyo lazima ikubaliwe na kuridhiwa na thuluthi mbili za wajumbe wa Bunge la Senate. (Artcle II, Section II)
Pia, raisi wa Marekani ana mamlaka ya kuteua mawaziri, mabalozi, majaji wa Mahakama Kuu, lakini baada ya uteuzi wake kupata idhini ya Bunge la Senate. (Artcle II, Section II)
Hata wakati wa Khilafah kulizuka mashaka mbalimbali kama watu kurtadi kwa makundi, uasi, kujitenga na dola nk. lakini kwa kuwa dola ilikuwa na taasisi na vyombo thabiti kukabiliana nayo, ilikabiliana na changamoto hizo kwa uwezo na umakini mkubwa.
05 Novemba 2020

Maoni hayajaruhusiwa.