Mauaji ya Khashoggi: Fedheha kwa Saudia, Sera ya Nje ya Marekani na Ubepari

Tangu tarehe 2.10.2018 vyombo vya habari vya kilimwengu na kimaeneo vimekuwa vikiangazia taarifa mbalimbali zinazohusu kifo cha bwana Jamal Ahmad Khashoggi. Tangu siku hiyo mpaka sasa bado habari zake hazijaondoka japo zimepungua katika vyombo vya habari.

Khashoggi aliyezaliwa katika mji wa Madina, Saudi Arabia, mpaka kifo chake kinamkuta alikuwa akiishi nchini Marekani, akifanya kazi ya uandishi wa habari katika gazeti la Washington Post la nchini humo ambapo alitengewa ukurasa maalum kwa makala zake, nyingi zikipigania demokrasia kwa Waislamu.

Makala zake nyingi zikielekezwa kuishambulia Saudia, hususan kukosoa utawala wa kifalme na kupigania demokrasia. Pia ameandika sana kuhusu hitajio la demokrasia katika nchi za Waislamu.

Serikali ya Uturuki ndiyo ya kwanza kuielekezea kidole Saudi Arabia kwamba imemuua Khashoggi katika ubalozi wake nchini Uturuku. Awali Saudi Arabia ilikataa, lakini baadae tarehe 20.10.2018 ilikubali kutokea kwa tukio hilo katika eneo hilo na kwa kudai kuwa ni ugomvi binafsi baina yake (Khashoggi) na maafisa wa ubalozi huo baada ya kutokea sintofahamu.

Saudi Arabia na Uturuki ni mataifa ambayo hayapo katika hali nzuri ya kimahusiano hususan baada ya mgogoro wa kidiplomasia wa Qatar, ambapo Uturuki inaiunga mkono Qatar dhidi ya Saudia na washirika wake. Pia katika mgogoro wa Syria wakiwa kila mmoja upande tofauti lakini wakicheza kwa namna moja ya kuimarisha sintofahamu iliyopo ambayo kimkakati ni manufaa kwa mabwana zao, hususan Marekani.
Wakichonganishwa na fikra mbovu za uhasama wa kibinafsi wameweza kuunda pande mbili katika mgogoro wa Syria kukiwa na Iran upande mmoja akisaidiwa na Urusi na Uturuki na upande wa pili ni Saudi Arabia na wenzake wakisaidiwa na Marekani. Japo kidhahiri, pande zote mbili ni vibaraka wa Marekani. Kama wanavyoendelea kutumika katika maeneo ya Iraq na Israel.

Kwa upande wa pili, Marekani inakiri kwamba Saudi Arabia ni nchi muhimu sana katika kusimamia maslahi yake katika Mashariki ya Kati, inaisifu kwamba siasa yake, utamaduni wake, uchumi wake na nafasi yake katika mataifa ya kiarabu na kijiografia kumeifanya iwe na umuhimu huo (www.state.gv).

Aidha, Saudia imekuwa miongoni mwa masoko makubwa ya silaha za Marekani, pia imekuwa muingizaji mkubwa wa mafuta yake Marekani. Na zaidi ya hapo inatozwa ghrama kubwa kulipia ulinzi inaoupata kutoka Marekani. Kwa hiyo ili kuendelea kuwa na ‘amani’ haIna budi Saudia kumsikiliza Marekani katika mipango, maamuzi na utekelezaji.

Sera ya nje ya Marekani na Mataifa mengine ya kimfumo ndani ya nchi za Waislamu ni “kila kitu dhidi ya Uislamu”. Kwa hiyo kila panapowezekana kuzuia mwamko wa Uislamu lazima itumike nguvu nyingi kuzima. Kila inapowezekana au hata kwa kulazimishwa lazima mfumo wanaouunga mkono uingizwe katika ardhi za Waislamu. Mojawapo ni utamaduni wa kimagharibi (kutembea uchi, ulevi, kupinga ndoa, ushenzi wa kitabia nk) na siasa ya kidemokrasia inayotaka ‘uhuru’ jumla wa binadamu na kutupilia mbali muongozo wa Mwenyezi Mungu, Muumba.

Kwa hiyo, kila atakaye simama, ima kibinafsi au maalum kwa wao kumuandaa, kusaidia kuenea na kuimarika kwa siasa hii ya nje, lazima atalindwa na kuwezeshwa kwa muda wote yatakapohakikishwa maslahi ya Marekani.

Mbinu iliyotumiwa na ambayo bado inatumiwa kuiweka Saudi Arabia mikononi mwa Amerika ni kuijengea vitisho vya ndani kwanza, kisha vya nje na kuionesha kwamba bila Marekani, Saudia hawezi kupambana na hali hizo. Mazoea yakajenga tabia hiyo, na sasa imekua ndiyo maumbile ya ushirikiano wao, kama baba na mtoto.

Kwa kazi ya Khashoggi ya uwanahabari na jukumu alilojitwika la kukosoa tawala za Mashariki ya Kati (nchi za Waislamu) na kushaajiisha demokrasia badala ya Uislamu, alikuwa ni mtu muhimu sana kwao na ‘adui’ kwa Saudia. Alikubaliwa kuishi Marekani kwa kuwa alikuwa ni chombo chao kinachosaidia kutimia na kuendelea na mkakati wao wa kuwa mkuu wa hadhara/itikadi ya kibepari kwa mujibu wa sera yao ya nje.

Serikali ya Uturuki, ambayo kidhahiri inaonekana ni mpinzani wa Saudia na Marekani, ndiyo wa kwanza kuishutumu Saudia kwa mauaji ya Khashoggi, (na Saudia awali ilikataa), mataifa mengi ya kimfumo yakaunga mkono wazo hilo kupitia vyombo vyao vya habari na waandishi wao wakubwa.

Marekani katika kuendeleza nafasi yake ya ubaba kwa Saudia, na kuichuma zaidi katika fursa hii, ndipo Trump kiawali akaiunga mkono Saudia, akakataa kwamba Saudia haihusiki. Kisha akampigia simu Mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz Al-Saud, ili apate ufafanuzi, na bila ya shaka kumuwekea maazimio na kumtisha kwamba nchi yake itatengwa, hivyo (inavyoonekana) akubali uhalisia, lakini hatafanywa chochote maana baba (Marekani) yupo upande wake.

Saudia ikakubali kosa, na kauli ya pili kwa Marekani hadharani ni kuilaumu nchi hiyo kwa kuchelewa kukiri kosa walilofanya. Ni lawama ya kiini macho kwani kwao wao ni mafanikio ya kimkakati.

Hii ndiyo hali halisi ya aibu ya vibaraka katika nchi za Waislamu, namna wanavyodhuru raia wao kwa khofu ya viti vyao vya utawala, Khashoggi akiwa mmoja, ilhali kuna mamia ya wanavyuoni, wengine wakifa kwa mateso, na wengine wakiendelea kusota mahabusu, huku dunia ikiwa kimya cha mfu. Huku nchi hizi za vibaraka hulazimika kimkakati kufuata kila linalowapendeza mabwana zao ili nao kujihakikishia maslahi yao.

Pia tukio hili ni aibu kubwa kwa mataifa makubwa hususan Marekani na mfumo wao wa ubepari kwa jumla. Wao hutumia kila fursa kuendeleza unyonyaji, kujiongezea maslahi na kuimarisha athari zao, hata kama ni kwa gharama ya uhai wa mtu.

Risala ya Wiki No. 18

21 Safar 1440 Hijri | 30-10- 2018 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.