Mauaji Ni Zaidi Ya Watoto Mkoani Njombe
Awali, tunalaani kwa nguvu zote matukio ya kikatili ya kuuwawa watoto wasio na hatia mkoani Njombe na kutoa pole kwa wafiwa na wahanga wote kiujumla.
Vitendo hivi vya kuwadhulumu watoto wadogo mkoani humo vinavyofanywa na watu “wasiojulikana” ambavyo vinahusishwa na ushirikina ni jambo la kuhuzunisha na kutia simanzi kubwa, ambapo watoto kadhaa wenye umri kati ya miaka sita na mitatu wameshapoteza maisha yao na miili yao kupatikana imetolewa baadhi ya viungo kama meno, masikio na viungo vya siri.
Mauaji hayo yamezua taharuki na kunapazwa sauti na kada mbalimbali katika jamii kitaifa na kimataifa ya kutaka hatua kabambe zichukuliwe kuwapata wahalifu na kuzuiya mauaji hayo yasiendelee.
Hata hivyo, lazima tukumbuke kuwa mauaji haya ni muendelezo wa mauaji mengi ya kiholela yanayoendelea kutokea kila kukicha Tanzania, huku kukikosekana majibu sahihi kuhusu uhakika wa wauaji kukamatwa, na haki kutendeka kwa wahanga wa matukio haya. Miaka ya hivi karibuni kumeibuka wimbi kubwa la utekaji pia mauaji ya watu wazima, huku haya mauaji ya watoto hawa ni matukio ziada.
Matukio kama kuokotwa kwa maiti zikielea katika mto Ruvu, ufukwe wa Coco, kupotea watu karibu 400 mkoa wa Pwani, kuuawa watoto katika mikoa ya Arusha, Mwanza nk. ni miongoni mwa matukio machache miongoni mwa mengi yaliyotokea hapa Tanzania. Ni wazi suala hili la mauaji ya watoto na wananchi kwa ujumla limekuwa limeshamiri na kujitokeza mara kwa mara na kusababisha watu kuishi kwa hofu na mashaka makubwa.
Aidha, mauaji haya kuhusishwa na imani za kishirikina za kupata utajiri na madaraka na kuaminika kutokea zaidi kipindi karibia na uchaguzi kama masharti ya kishirikina katika kupata madaraka yanaakisi athari ya mfumo wa kibepari ambao msingi wake ni kujiongezea maslahi bila ya kujali utu, uhai au ustawi wa binadamu kiujumla.
Baadhi ya wasiasa wa kidemokrasia hupewa masharti ya kishirikina kwa matarajio ya kuweza kushinda chaguzi na kupata vyeo vya kisiasa, pia watu wa kawaida hupewa masharti kama hayo ili kwa matarajio ya kupata utajiri.
Matukio haya pia yanaashiria udhaifu wa vyombo vya usalama katika kulinda raia, uhai na mali zao. Kwa kuwa yanatukia katika hali ya kujirudiarudia bila ya kupatiwa ufumbuzi madhubuti. Hali hii inazidisha kuondoa imani ya raia kwa vyombo vya ulinzi na inadhihirika wazi kwa upande mmoja kuwa kazi ya vyombo vya usalama katika mfumo fisidifu wa kibepari ni kulinda tabaka la watawala na sio raia wa kawaida.
Uislamu msingi wake wa kutenda na kuacha kutenda matendo ni ‘halali’ na ‘haramu’. Hivyo ni mwiko mambo kama haya kutokea. Aidha, Uislamu umeweka adhabu kali kwa makosa kama haya ili kuhifadhi Ummah na majanga kama haya.
Kupitia utabikishwaji wa Uislamu, uadilifu wa sheria zake na utabikishaji wake katika tareekh ilishuhudiwa kudhibiti uhalifu na mauaji ya kiholela kwa kiasi kikubwa, na Waislamu na wasiokuwa Waislamu waliishi kwa amani na utulivu chini ya kivuli cha dola ya Kiislamu ya Khilafah .
Matukio kama haya ni tafakuri muhimu kwa jamii ya kuhoji kuhusu uhalali wa mfumo fisidifu wa kibepari na siasa zake za kidemokrasia kuendelea kumtawalia mwanadamu. Jamii lazima itambue kuwa ubepari kamwe hauwezi kupambana na mila potofu za kishirikina kwa sababu kipimo chake cha ‘maslahi’ kimaumbile kinaukosesha nishati hiyo. Ni Uislamu pekee ndio unaoweza kukabiliana na matendo hayo na kurejesha imani, usalama na utulivu kwa wanadamu wote.
09 Jumada al-Thanni 1440 Hijri | 14-02- 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.