Mama wa Kiislamu Itumie Vyema Fursa ya Ramadhani

Allah Ta’ala amemjaalia mama wa Kiislamu jukumu kubwa na adhimu linalowafikiana na maumbile yake la ulezi wa watoto, uangalizi wao na utunzaji wa nyumba yake. Pamoja na ukweli kwamba pia huruhusiwa (mubaha) kufanya kazi nyengine za halali nje ya nyumba yake bila ya kuathiri jukumu lake la msingi

Jukumu lake hilo la uangalizi wa nyumba na watoto humfanya mama kimaumbile kuwa na athari muhimu na ushawishi mkubwa ndani ya nyumba yake kwa watoto wake na mume wake kijumla. Kwa ufupi, mama huwa malkia ndani ya nyumba yake. Kwa hivyo, ni jambo la busara na fursa ya aina yake katika mwezi huu wa Ramadhani kwa mama wa Kiislamu kuutumia vyema ushawishi wake huo kwa lengo la kuhamasisha ibada, kuunga udugu na kuifikisha daawa ya Kiislamu kwa ujumla.

Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, mama atumie ushawishi wake kama mama, kwa watoto wake hususan watoto wake wadogo kwa kuanza kuwafundisha na kuwahamasisha kufunga Ramadhani kwa kuwapa moyo na kuwashawishi kwa zawadi ndogondogo ili waendelee kufunga. Hilo ni kutokana na ukweli kwamba Uislamu unatutaka tuanze kuwafundisha watoto wetu ibada mapema katika maisha yao, ili waweze kuzizoea ibada hizo katika umri wao wa mapema.
Na mama wa Kiislamu ana nafasi zaidi na ushawishi mkubwa zaidi kwa jambo hili.

Aidha, mama wa Kiislamu kwa kushirikiana na mumewe katika mwezi huu wa Ramdhani waitumie fursa kwa kuihamasisha familia yao kwa kila aina ya ibada kama swala za jamaa, tarewehe, swala za usiku, kutoa sadaka, kusoma Quran, kutembelea jamaa na kuhudhuria darsa na mihadhara mbalimbali ya kidini, na sio kuwaachia watoto kushiriki katika kuangalia michezo ya upuuzi katika Tv au kuutumia muda kwa michezo kama karata nk . Mama wa Kiislamu ana uwezo wa kulifanya hilo kwa ushawishi wake kama mama, na kutokana na kukaa kwake muda mwingi na watoto wake nyumbani.

Katika mwezi huu mtukufu, pia mama wa Kiislamu anaweza kuitumia fursa ya kuunga udugu zaidi, kwa kushauriana na mumewe kuwaalika ndugu na jamaa mbalimbali katika mwaliko wa futari kwa lengo la kuimarisha mahusiano zaidi ya kuunga udugu. Jambo hili la kuunga udugu ni ibada kubwa na miongoni mwa faradhi katika dini yetu.

Mwisho, mama wa Kiislamu aitumie fursa ya mwezi huu kwa kutekeleza jukumu kubwa, tukufu na faradhi la ulinganizi wa Kiislamu/daawa. Hili ni kwa kuwafafanulia ndugu, jamaa na marafiki ufaradhi wa kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah ambayo hutekeleza sheria zote za Kiislamu. Jukumu la ulinganizi ni la kila siku lakini kinamama wanaweza kuutumia usahali wa mwezi huu wa Ramadhani ambao nyoyo za Waislamu hujikurubisha zaidi kwa Allah Ta’ala.

Wanaweza kutumia mbinu mbalimbali na mbinu adhimu zaidi ni ya mwaliko wa chakula cha futari. Mbinu ambayo aliwahi kuitumia Mtume SAAW alipowaalika watu mbalimbali mwaliko wa chakula ili kuwalingania Uislamu. Mbinu hii ni fursa muhimu ya kiurafiki na ya kimaumbile inayoweza kutumika kuwajenga Waislamu fikra thabiti juu ya Uislamu na kuasisi majadiliano ya kirafiki ili kuwaonesha ufaradhi wa kutawaliwa na dola ya Kiislamu ya Khilafah.

Ufanisi wa haya yote humpasa baba wa Kiislamu kuwa mstari wa mbele kwa kutoa mashirikiano yake kwa dhati. Kwa sababu majukumu hubebwa kwa mashirikiano ya baba na mama.
Allah Ta’ala anasema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنْ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّهُ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao. Huamrisha mema na kukataza maovu, na husimamisha Swala, na hutoa Zaka, na humtii Allah na Mtume wake. Hao Allah atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikma”. [TMQ 9:71]

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.