Mafunzo ya Jkt na Athari Zake Kwa Waislamu
بسم الله الرحمن الرحيم
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limekuwa likiendesha mafunzo ya kijeshi ndani ya miezi mitatu punde tu baada ya mitihani ya utimilifu ya kidato cha sita.
Mpango huu wa serikali upo kwa mujibu wa sheria, na ni mkakati unaolenga kumfinyanga mlengwa katika upande wa kifikra kama uzalendo, kuwa mbali na dini nk. na pia huhusisha mafunzo ya kijeshi kwa kiasi fulani.
Kuna kambi kadhaa za kijeshi kupokea makundi ya wahitimu wa kidato cha sita kutoka maeneo mbalimbali nchini hususan shule za Tanzania bara kwa ajili ya mafunzo hayo.
Hassan Mabena, Brigedia Jenerali wa jeshi hilo amenukuliwa akisema :
“Mkakati huu ulianzishwa kwa lengo la kujenga hisia za kizalendo, umoja wa kitaifa na kufundisha maadili pamoja na stadi za kazi kwa vijana wa kitanzania”. https://youtu.be/8AuRyd2xylo
Kihistoria mkakati wa JKT ulibuniwa na Joseph Kuzurira Nyerere (Katibu mkuu vijana TANU) mnamo miaka ya 1963-64 ili kutoa mafunzo kwa vijana wa TANU, ambapo awali walikusanywa vijana 11 kutoka wilaya 11 za Tanzania bara kupata mafunzo hayo yaliyoendeshwa na makamanda wa kijeshi kutoka Israel katika kambi ya jeshi ya Mgulani (DSM).
Baada ya kuonekana tija ya mafunzo ya awali serikali ya Tanzania ikapitisha sheria mwaka 1964 kuwataka watumishi na vijana wanaohitimu kidato cha nne na cha sita wakati huo kujiunga na mafunzo hayo chini ya udhamini wa serikali.
Hivyo, mwaka 1967 rasmi mafunzo yakaanza katika kambi kadhaa za kijeshi. https://www.google.com/url?sa=t&source=web&rct=j&url=https://lukwangule.blogspot.com/2013/03/kikwete-azindua-mafunzo-ya-jkt-kwa.html%3Fm%3D1&ved=2ahUKEwiCgrCrzev_AhUoVKQEHWHDDqkQFnoECBAQAQ&usg=AOvVaw2qzfyUG8cUkysZ7EipT8S4
Kutokana na changamoto za kifedha mkakati wa mafunzo ya JKT ulisitishwa mnamo mwaka 1992 hadi uliporejeshwa tena Machi 26 mwaka 2013 na raisi Jakaya Mrisho Kiketwe na waziri wake wa ulinzi wa wakati huo Hussein Ali Mwinyi.
Tangu kurejeshwa kwake serikali ya Tanzania imekuwa ikitumia kiasi cha sh. bilioni 7.5 na zaidi kila mwaka ili kudhamini mafunzo hayo. https://www.mwananchi.co.tz/…/atakayekacha-mafunzo-jkt…
Kwa sasa kambi za jeshi zimeongezwa kutoka 6 hadi 20 ili kupokea maelfu ya wanafunzi wanaohitimu kila mwaka. Miongoni mwa kambi zilizoorodheshwa na Brigedia generali Hassan Mabeni ni Rwamkoma, Sange, Ruvu, Mpwapwa, Makutopora, Mafinga, Mlale, Mgambo, Maramba, Makuyani, Bulombora, Kanebwa, Mtabila, Itaka, Luwa, Milundika, Nachingwea, Kibiti, Oldonyo nk… Kwa makadirio mwaka huu wa 2023 wanafunzi wanaotaraji kujiunga na mafunzo hayo ni wanafunzi elfu 90 kutoka shule zote za Tanzania bara. Hii ni idadi kubwa zaidi ya wale mwaka 2013 ambao walikuwa wanafunzi elfu 5 tu kati ya elfu 41.
Mkakati na mpango huu wa JKT umekuwa ukipigiwa chapuo sana na wabunge na wanasiasa mbalimbali wa kidemokrasia nchini na kuona kuna faida nyingi kwa vizazi vya kitanzania. Baadhi ya wabunge wakitamani muda uongezwe hadi kufikia miezi sita, japo kumekuwa na malalamiko ya chini chini na uwoga kwa wazazi na watu wengi kupinga mkakati huu.
Sisi Waislamu hasa wabebaji daawa tuna mengi ya kusema dhidi ya mkakati huu kwani sio tu unagongana na nidhamu ya Kiislamu, bali umekuwa ukiharibu haiba na shakhasia ya vijana wa Kiislamu pindi wanapojiunga katika mafunzo hayo.
Miongoni mwa athari za mkakati wa JKT ni hizi:
Awali, kumakinishwa zaidi kwa fikra hatari na batili ya kizalendo kwa Ummah wa Kiislamu. Uzalendo ni miongoni mwa mafungamano maovu na fikra potofu katika Uislamu na ni haramu Waislamu kuibeba, kuipigia debe nk. Ni fungamano duni lisilofaa kuwafungamanisha watu, kwani ni fungamano lenye kuibuka na kuendeshwa na mihemko ya kihisia ili kulinda watu wa kitaifa au taifa lao. Fungamano hilo hupotea punde tu hisia zao zitakapoyeyuka au kupotezwa kwa jambo lengine.
Kwahivyo, endapo fungamano hili likabebwa ndani ya mioyo ya Waislamu litawarejesha nyuma kihisia juu ya aqida yao, na zaidi ni kujitenga na kijiweka mbali na Ummah wa Kiislamu, kwani hawatohisi huruma, maumivu au madhila yanayowakuta Waislamu wenzao ndani ya nchi na hata walio nje ya mipaka ya Tanzania. Zinapokufa hisia za Muislamu na fungamano lake na Waislamu wenzake, hatoona aibu kupanga njama au hata kushiriki katika mipango dhidi ya Waislamu wenzake ili kuonesha uzalendo kwa taifa lake ilhali Muislamu anatakiwa awe mstari wa mbele kuwahami Waislamu wenzake kwa vitendo na kauli kama alivyosema Mtume Muhammad (s.aw).
“المسلم من سلم المسلمون من لسانه و يده”
“Muislam ni yule ambae wamesalimika Waislamu wenzake kutokana na ulimi wake na mikono yake…” Sahih Bukhari 6484
Historia pia inatukumbusha namna fikra hizi za kizalendo zilivyokoleza moto katika kuangushwa dola ya Kiislamu ya Khilafah ya Uthmaania, kwa kupelekea kumeguka meguka kwa dola ya Kiislamu na kuvunja hisia za Waislamu juu ya dini yao na kukosekana umoja na nguvu moja ya Waislamu ulimwenguni.
Waislamu wana wajibu wa kujitenga na fikra hii adui katika maisha yetu kwani uzalendo wa nchi, chama cha siasa, timu za mipira nk. vyote huleta mtengano ndani ya Ummah na kurejesha nyuma jitihada za kurejesha maisha ya Kiislamu.
Pili, kuharibiwa kwa shakhasia/utambulisho wa Kiislamu; Mkakati huu wa JKT umekuwa na athari kubwa katika fungamano la Waislamu na Muumba wao. Shakhsia ya vijana wa Kiislamu imekuwa ikivunjwa kwa makusudi kiasi imewarejesha nyuma vijana hao katika kuchunga maamrisho ya Mwenyezi Mungu.
Mafunzo katika kambi za JKT yamefinyangwa katika hali ya kuwa mbali na Muumba. Hivyo, maadili wanayofinyangwa nayo vijana wetu yanakinzana kabisa na hukmu za kisheria za Kiislamu. Mambo kama uvaaji wa kaptura na t-shirt, kukaa vichwa wazi kwa mabinti, zinaa nk. yamesheheni katika kambi hizo na yote haya hayakubaliki katika Uislamu.
Vijana wa Kiislamu wamewekewa ugumu katika kutekeleza ibada za swala, funga kwa kipindi chote, na hata wale wanaofanya jitihada hulazimika kukusanya swala kipamoja na kuzitekeleza wakiwa wamevalia kaptura. Yote haya ni muendelezo wa fikra na njama fisidifu za ubepari dhidi ya Ummah wa Kiislamu, na kwa masikitiko makubwa hata vyombo vya kidini ndani ya nchi havijapaza sauti kukemea mkakati huu ambao unabomoa imani za vijana wa Kiislamu.
Tatu, kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na mateso makali. Kume kuwa na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wazazi dhidi ya mkakati huu juu ya vitendo vya kingono na mateso wanayopata mabinti katika kambi hizo, lakini mara kadhaa jeshi hilo hutoka mbele ya vyombo vya habari kukanusha tuhuma hizo na kutoa kauli za vitisho kwa watu wanaotoa tuhuma hizo kuwa watashughulikiwa vikali. Ni kweli kwamba mabinti wamekuwa wakipata manyanyaso mengi hasa pindi wanapoonesha msimamo wa kukataa zinaa.
Akieleza binti mmoja wa Kiislamu Bint Thabit (tumeficha jina) kuwa baadhi ya wanajeshi wamekuwa wakiwataka mabinti na kuwalaghai kuwa watapunguziwa mazoezi makali endapo watakubali kufanya nao mapenzi. Binti huyo amefika mbali na kusema katika kambi hizo hakuna ufaragha baina yao na vijana wa kiume, na kunaa nyakati katika mabweni yao wanaingia askari wa kiume. Akisimulia shuhuda mwengine kuwa, iliwahi kutokea katika kambi yao binti kubakwa na askari watatu. Hii ni mifano michache tu ya madhila wanayopitia vijana na mabinti wa Kiislamu. Kimsingi vitendo vichafu ni vingi, kiasi kwamba hata nyimbo za matusi ndio zimekuwa chachu katika mazoezi yao.
Wazee, wazazi na walezi wa Kiislamu waamke kutoka usingizini na wajue kuwa wana dhima ya kulinda imani na maadili ya watoto wao kama Allah Taala alivyoamirisha :
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ
“ Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na ahli zenu kutokana na moto ambao kuni zake ni watu na mawe…” (Qur’an 66:6)
Kwa upande mwengine, tukichunguza kwa makini kama tuna msimamo upo uwezo wa kujitenga na mpango wa JKT bila hata kutumia nguvu au kudhurika kutokana na hali zifuatazo:
Ajenda ya mafunzo ya JKT imekuwa ukiendeshwa na kuratibiwa na jeshi kwa mujibu wa sheria ila umekuwa ikiendeshwa kimaeneo. Mfano, wanafunzi wa Tanzania visiwani (Unguja na Pemba) au wale waliofeli kidato cha nne hawakujumuishwa katika mkakati huu.
Aidha, agizo la sheria la kuwataka wanafunzi kujiunga na mpango huu limekuwa likitekelezwa pasipo na vitisho vyovyote kwa wale ambao hawakufika katika mafunzo hayo. Kwa hivyo, jambo hili limebeba sura ya ukhiyari kwa mtu kwenda au kutokwenda. Na zaidi, hakuna chombo chochote cha serikali kinachoweka vikwazo vya kimasomo au kuwawajibisha wazazi au wanafunzi ambao hawakufika katika mafunzo hayo. Kuna maelfu ya wanafunzi ambao hawakushiriki katika mafunzo hayo katika miaka kadhaa, na bado wakaendelea na elimu ya juu. Kwa mfano, mwaka 2013 wanafunzi walioshiriki katika mafunzo hayo ni wanafunzi 5000 kati ya wanafunzi 41,000 waliohitimu kidato cha sita ndani ya mwaka huo 2013. Pia hata mpango ulipowataka watumishi na wabunge vijana kushiriki katika mafunzo hayo, ni wabunge 24 tu ndio walioshiriki kati ya wabunge 47, huku wawili kati ya 24 waliondoka katika mafunzo hayo ndani ya wiki mbili na kutorejea tena.
Kumekuwa na kauli zisizo sahihi kuwa endapo kijana hatokwenda JKT atawekewa ngumu katika kupata ajira serikalini, kitu ambacho hakijathibitishwa na serikali kwani serikali imekuwa ikiajiri watu wengi ambao hata katika mafunzo ya JKT hawakupita.
Viwe viwavyo, yote hayo hayawezi kumtia Muislamu wasiwasi au kumyumbisha Muislamu mwenye kutaka radhi za Mola wake kuwa na khofu juu ya suala la ajira au rizik, kwani Muumin wa kweli daima ana yakini bila ya tembe ya shaka kuwa Mtoaji rizk ni Allah Taala, Ambaye Ameshamkadiria kila mtu fungu lake.
Amesema Allah SWT.
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلاَةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا لاَ نَسْأَلُكَ رِزْقًا نَحْنُ نَرْزُقُكَ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَى (طه: 132).
“Na waamrishe watu wako kuswali na uendelee mwenyewe kwa hilo. Hatukuombi riziki bali Sisi ndio Tunaokuruzuku. Na mwisho mwema utawathubutikia wamchao Mungu” (Qur’an 20:132)
Hivyo, itoshe kwa Muislamu kujua ni haramu kushiriki katika mafunzo hayo yaliyosheheni maadili kinyume na Uislamu.
Mwisho, Uislamu ukiwa mfumo kamili wa maisha una misingi ya kuleta ustawi kwa kwa wanadamu kwa kutunza imani, heshima na mali zao. Aidha, vijana wakakamavu na mahodari ni tunu na rasilmali muhimu katika Uislamu lakini hilo liende sambamba na kufungamana na vipimo vya ‘halali’ na ‘haramu’ na si vyenginevyo.
Dola ya Kiislamu (Khilafah) itafinyanga vijana wake wawe imara kwa kuwa kuna faradhi ya vita vya jihadi, lakini haitokwenda kinyume na Uislamu wala haitolazimisha wanawake katika mafunzo ya kijeshi, kwa kuwa kupigana jihadi ni faradhi kwa wanaume na sio wanawake.
Risala ya Wiki No. 162
10 Safar 1445 Hijria / 26 Agosti 2023 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.