Mafunzo Kutoka Uzushi Dhidi ya Mama Aisha (r.a)

Miongoni mwa matukio muhimu kuchukuwa mafunzo ya kijamii ni tukio kubwa la ‘Ifk ‘lilotokea mwezi kama huu wa Shaaban mwaka 6AH. Tukio hili lilitokea wakati jeshi la Waislamu pamoja na Mtume SAAW lilipokuwa likirudi katika Vita vya Bani Mustaliq. Katika msafara huo Waislamu walipitisha usiku mahala karibu na Madina, na msafara ulipoondoka Mama Aisha (Ra ) kwa bahati mbaya aliachwa nyuma kutokana na kushughulika kutafuta mkufu wake uliompotea. Na hatimae Bi Aisha akachukuliwa na sahaba Safwan bin Mu’attal aliyekuwa nae kabakia nyuma. Hali hiyo ilipelekea kukashifiwa Mama wa Waumini Bibi Aisha bint Abuu Bakar (ra) kwa kuzushiwa uongo kwa kunasibishwa kufanya uchafu wa zinaa na sahaba huyo.

Wanafiki ndani ya Madina wakiongozwa na Abdulla bin Ubayy bin Salul walifanikiwa kwa muda kuzishawishi nyoyo za baadhi ya Waislamu kuamini kwamba Mama Aisha ra. kazini na Safwan bin Mu’attal kupitia uvumi na propaganda chafu walizoeneza dhidi ya mke huyo wa Mtume SAAW.
Allah Taala kwa Uwezo wake akakanusha uvumi, uzushi na masingizio hayo ya uwongo yaliokusudiwa kupandikiza shaka katika nyoyo za Waumini, kushusha hadhi ya mke wa Mtume SAAW, kumdhalilisha Mtume SAAW na Uislamu kwa jumla. Vitimbwi hivi vya maadui vikashindwa na kuondoka patupu kwa kuteremshwa Aya zilizomsafisha Mama Aisha (ra) na uchafu na tuhuma alizonasibishwa nazo.

Pamoja na hayo baada ya tukio hilo ovu, Allah Taala kwa Rehma zake akateremsha ufafanuzi rasmi wa suala la ya Al-qadhf kwalo hupatikana kulindwa heshima ya wanawake wema, wachamungu na wanaojitakasa na kashfa ya masingizio. Al-Qadhf ni masingizio ya kutenda vitendo vichafu hususan zinaa ambapo msingiziaji hushidwa kuthibitisha kwa kuleta ushahidi. Tendo hili ni haramu, na Uislamu umeweka adhabu kali/hadd maalum inayotekelezwa ndani ya dola ya Kiislamu pale mtu atakapomsingizia mwenzake, na mhalifu akithibitika kuwa na hatia hulazimika achapwe viboko themanini.

Kinyume na mfumo wa kidemokrasia ambao unamkandamiza mwanamke katika kila hali kuanzia kumuweka uchi, kumlazimisha kufanya kazi, kumfanya karagosi wa kutangazia biashara, kumuuza ili kumalizia matamanio nk. Uislamu umeleta ukombozi wa kweli kwa mwanamke kuanzia katika kumiliki, kurithi, kulazimisha mume kuhudumia mkewe na mwanamke akiwa mjane ahudumiwe na mawalii wake nk. Pia Uislamu umekuja kulidha hadhi, haiba na heshima ya mwanamke kwa kuharamisha kutumiwa kama chombo cha kutangazia biashara, kuuza mwili wake, bali umeharamisha hata kusingiziwa uongo wa vitendo vichafu, licha ya kuwa mwanamke mchamungu wa Kiislamu hatarijiwi kamwe kujiingiza katika mazingira yenye kutia shaka kuwafanya watu kumpa tuhuma chafu kama hizo.

Ni wajibu wanawake na wanaume wa Kiislamu kujipinda katika kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah ili sheria hii ya Al-qadhf ipate kuchukuwa mkondo wake kulinda heshima, hadhi na haiba ya Waislamu na kujenga jamii yenye heshima na maadili mema.

Na Masoud Msellem
16 Aaprili 2019

Maoni hayajaruhusiwa.